

Samuel Sitta na bunge la tisa
Dar es Salaam. Wakati Novemba 7, 2026, aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, akitimiza miaka 10 tangu afariki dunia, familia yake imeandaa kumbukizi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akizungumza na Mwananchi, mtoto wa marehemu Sitta, Benjamin Sitta amesema shughuli ya kumbukizi ya baba yake imegawanyika katika makundi matatu ikiandaliwa kwa ushirikiano wa familia, Bunge na wadau mbalimbali.
Amesema Novemba 3, 2026 kutakuwa na uzinduzi wa kitabu cha Sitta kitakachozungumzia mwenendo mzima wa maisha yake kuanzia utoto, shuleni hadi siasa.
“Ni kitabu kizuri licha ya kuandaliwa kwa haraka na familia pamoja na mwandishi maalumu. Novemba 8 kutakuwa na misa maalumu wilayani Urambo.
” Novemba 9 hadi 13 kutakuwa na shughuli ya upimaji afya bure itakayofanyika pia Urambo,” amesema Sitta.
Samuel Sitta, ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alifariki dunia Novemba 7, 2016, nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwanasiasa huyo, anakumbukwa kwa uongozi uliotambulika kwa ‘kasi na viwango’ katika kuendesha Bunge la tisa (2005–2010), lililojipambanua kwa mijadala na hoja zilizogusa masilahi ya Taifa. Anakumbukwa kwa msimamo wake kuhusu uwajibikaji wa Serikali, uhuru wa wabunge kujadili masuala ya kitaifa na namna alivyosimamia mijadala iliyogusa masilahi ya wananchi.
Sitta katika kipindi chake cha uspika alionesha wazi kuwa hakukusudia kuliongoza Bunge kama chombo cha kupitisha maamuzi ya Serikali bila kuhoji.
Kwake, Bunge lilipaswa kuwa mhimili wenye nguvu ya kuisimamia Serikali, kuhoji matumizi ya madaraka na kuhakikisha matatizo ya wananchi yanapatiwa majibu.
Wakati wa uongozi wake wa Bunge la tisa, Tanzania ilishuhudia mijadala mikubwa iliyowahusisha mawaziri, watendaji wa Serikali na viongozi wa ngazi za juu.
Miongoni mwa matukio yaliyobeba uzito mkubwa katika historia hiyo ni uchunguzi wa mkataba wa kampuni ya Richmond, ambao ulifikia hatua ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa (hayati), kujiuzulu Februari 2008.
Sitta alisimamia mabadiliko ya Kanuni za Kudumu za Bunge yaliyopitishwa mwaka 2007. Mabadiliko hayo yaliimarisha nafasi ya kamati teule za uchunguzi na kuongeza uwezo wa Bunge kuisimamia Serikali.
Pia, yalisaidia kuimarisha kamati za usimamizi wa mashirika ya umma, ikiwemo Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ambayo iliongeza wigo wa Bunge katika kuchunguza utendaji wa taasisi za Serikali.
Mageuzi hayo yalikuwa muhimu kwa sababu yaliwezesha wabunge kutumia taratibu za Bunge kuchunguza masuala yaliyokuwa na uzito wa kitaifa, badala ya kutegemea majibu ya Serikali pekee.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Oktoba 31, 2026 baadhi ya waliowahi kufanya kazi naye na wadau wa masuala ya siasa wanasema Sitta aliacha alama katika historia ya Bunge, ikiwemo kuimarisha uhuru wa wabunge kujadili masuala ya kitaifa bila kujali itikadi za vyama vyao.
Wanamtaja Sitta kama kiongozi aliyesisitiza Serikali kuwajibika kwa wananchi na kutaka Bunge liwe chombo cha kusimamia masilahi yao badala ya kuwa jukwaa la kuunga mkono kila jambo bila kuhoji.
Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu kupitia Chadema (2005–2020), Suzan Lyimo, amesema Sitta alikuwa Spika wa tofauti kutokana na mtindo wake wa kuendesha Bunge, akieleza kuwa enzi zake ndipo Taifa liliposhuhudia Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, akijiuzulu mwaka 2008.
Lowassa, aliyewahi kuwa mbunge wa Monduli mkoani Arusha, alijiuzulu uwaziri Mkuu Februari 7, 2008, kufuatia sakata la mkataba wa kampuni ya Richmond iliyokuwa imepewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura nchini.
Sakata hilo lilihusu tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za zabuni na madai ya kuingilia mchakato wa kuipatia Richmond mkataba wa kuzalisha megawati 100 za umeme.
Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Harrison Mwakyembe, ilichunguza mkataba huo na kuwasilisha ripoti yake Bungeni Februari 2008.
Akikumbuka namna Sitta alivyoendesha Bunge, Lyimo amesema alikuwa na mtindo tofauti wa kushirikisha wabunge katika shughuli za mhimili huo.
“Nakumbuka kwa mara ya kwanza, Spika badala ya kiti chake kuombwa mwongozo, yeye ndiye alikuwa anawaomba mwongozo wabunge.
“Alikuwa kiongozi aliyebadilisha Bunge, ikiwemo Naibu Spika kuvaa joho kwa mara ya kwanza,” amesema Lyimo.
Mbali na hilo, Lyimo, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), amesema wakati wa Sitta ndipo makatibu wa Bunge walianza kuvaa majoho, sambamba na wahudumu wa mhimili huo kuanza kuvaa sare maalumu.
Lyimo amesema Sitta alikuwa na upendo mkubwa kwa wabunge wa Bunge la tisa na alithamini ushirikiano wao kwa masilahi ya Taifa na mhimili huo.
Mbunge mwingine wa zamani kupitia CUF, Magdalena Sakaya, aliyekuwapo bungeni kuanzia mwaka 2005, amesema Sitta alikuwa na misimamo isiyoyumba na aliipenda nchi yake pamoja na Watanzania.
“Alipenda Bunge liwe chombo cha kuhudumia wananchi na Serikali ifanye kazi ya kuwahudumia wananchi, si wananchi wafanye kazi ya kuihudumia Serikali au Bunge liwe la kupigiwa makofi, alikataa.
“Alikuwa Spika ambaye kama Waziri hajajibu ipasavyo swali, anamwambia papo hapo kuwa hajaridhishwa na majibu. Ikiletwa hoja, iwe ya waziri au mbunge, kama haina mashiko kwa Taifa anasema wazi,” ameeleza Sakaya.
Kwa mujibu wa Sakaya, Sitta alikuwa Spika ambaye hakutaka kuwa sehemu ya Serikali, badala yake alibaki kuwa msimamizi wa Bunge ili mhimili huo ufanye kazi kwa uhuru bila kuingiliwa.
“Ndio maana Bunge la tisa lilikuwa likijadili hoja za wananchi na kuzipatia ufumbuzi, si kupigiana makofi au kusema ‘ndiyo mzee’, ndipo ukaja msemo wa Bunge la ‘speed and standard’,” ameeleza Sakaya.
Mchambuzi wa siasa ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema katika uongozi wa Bunge ameacha alama kubwa ikiwemo ya kutoa uhuru kwa wabunge wa chama tawala na upinzani.
“Alileta usawa, ingawa kuna muda mwingine alikuwa mkali. Ndipo hapa alipojitofautisha na maspika waliomfuatia,” amesema Dk Mbunda.
Hata hivyo, Dk Mbunda amesema pamoja na mazuri hayo, Sitta alikuwa na mapungufu yake ikiwemo namna alivyolishughulikia sakata la Zitto na kujiuzulu kwa Lowassa, akidai aliendesha masuala hayo kiuchama.
“Sitta ndiye alikuwa mwasisi wa neno siasa za majitaka, ingawa enzi zake alizifanya pia hasa kesi ya Lowassa,” amedai Dk Mbunda.
You may also like

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund

Mianya ya usajili inavyowalinda matapeli


Leave a Reply