Tanzania yaanzisha kituo cha kuwaandaa vijana wa Afrika kujadili tabianchi

Tanzania yaanzisha kituo cha kuwaandaa vijana wa Afrika kujadili tabianchi

Dar es Salaam. Tanzania imeanzisha Kituo cha Mafunzo ya Vijana wa Afrika kuhusu majadiliano ya tabianchi, kinacholenga kuwajengea uwezo vijana kushiriki katika maamuzi ya kimataifa yanayohusu mazingira na maendeleo.

Uzinduzi wa kituo hicho umefanyika jijini Dar es Salaam, leo Jumanne, Oktoba 20, 2026, ukiwa na lengo la kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kutetea masilahi ya nchi zao.

Mtaalamu wa nishati, mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa majanga wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, Dk Abbas Kitogo, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa muda mrefu wa Afrika kushiriki katika majadiliano yanayoamua mwelekeo wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema bara hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo ukame, mafuriko, mabadiliko ya misimu ya mvua na mmomonyoko wa ardhi, ambazo zinaathiri maisha ya watu, miundombinu na uchumi.

Hata hivyo, amesema kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kimataifa kunahitaji uelewa wa kitaalamu wa nyaraka, sera na misimamo ya nchi, pamoja na uwezo wa kujadiliana na kufikia makubaliano.

“Majadiliano haya yanaamua mambo muhimu kama upatikanaji wa fedha za kukabili  tabianchi, teknolojia, rasilimali za kukabiliana na athari zake na namna nchi zinavyoweza kuendeleza uchumi usiozalisha hewa ukaa kwa kiwango kikubwa,” amesema Dk Kitogo.

Amesema baadhi ya nchi za Afrika zina idadi ndogo ya wataalamu wenye uzoefu wa kutosha katika majadiliano hayo, huku vijana wakikosa fursa za kupata mafunzo ya vitendo yanayowawezesha kushiriki katika michakato hiyo.

Kupitia kituo hicho, amesema vijana watapata mafunzo ya kuandaa misimamo ya nchi, kuandika nyaraka za sera na kushiriki katika majadiliano ya mfano. Pia watapata ushauri kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu.

Katika awamu ya kwanza, vijana 33 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamepangwa kushiriki mafunzo ya ana kwa ana ya siku tano, yatakayofuatiwa na mafunzo ya mtandaoni kwa wiki nne.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Dk Richard Muyungi akizungumza na washiriki kutoka wa mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi tofauti barani Afrika.

Mshiriki kutoka Zambia, Mwaka Namkunda, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua iliyokuwa ikihitajika kwa muda mrefu kutokana na changamoto ambazo vijana wamekuwa wakikabiliana nazo katika kushiriki majadiliano ya tabianchi.

Amesema licha ya vijana kutajwa kuwa sehemu muhimu ya mustakabali wa bara hilo, wengi wamekuwa wakikosa ujuzi na uelewa wa lugha za kitaalamu zinazotumika katika majadiliano ya kimataifa.

“Tumekuwa tukisikia vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu, lakini imekuwa vigumu kwetu kujiweka katika nafasi ya kushiriki bila mafunzo yanayotupatia ujuzi unaohitajika,” amesema.

Namkunda amesema anatarajia kupata maarifa kuhusu mpito wa haki, ufadhili wa tabianchi na sera zilizopo ili aweze kushiriki katika majadiliano na kutetea masilahi ya nchi yake kwa ufanisi.

Afrika yahitaji wataalamu zaidi

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mazingira, Dk Richard Muyungi, amesema Afrika inakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi licha ya kuchangia sehemu ndogo ya uzalishaji wa gesi chafu duniani.

Amesema kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, Afrika inachangia chini ya asilimia nne ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, lakini inakumbwa na takribani asilimia 75 ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Uamuzi unaofanyika katika majadiliano ya kimataifa una umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa bara hili, hivyo ni muhimu vijana kuandaliwa mapema ili waendelee na juhudi za kutetea masilahi ya Afrika,” amesema Dk Muyungi.

Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza kituo hicho, kinachotarajiwa kuwa jukwaa la kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa majadiliano ya tabianchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Mazingira, Dk Maduhu Kazi, amesema mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maisha ya watu, usalama wa chakula na rasilimali za asili, hivyo ushiriki wa vijana ni muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

Amewahimiza washiriki kutumia mafunzo hayo kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano utakaowawezesha kuchangia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Source link