

Madaktari 100 kutoa huduma za afya bure Zanzibar
Unguja. Baada ya kuwahudumia wananchi zaidi ya 30,000 katika mikoa yote mitano ya Zanzibar tangu mwaka 2023, Kampeni ya Afya Bora Maisha Bora ya taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) inaanza rasmi awamu yake ya pili kwa kambi kubwa ya siku tano itakayofanyika Kinduni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kambi hiyo ya sita inatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 3 hadi 7, 2026, ikishirikisha zaidi ya wataalamu 100 wa afya, wakiwemo madaktari bingwa kutoka India.
Kambi hiyo inaendeshwa na ZMBF kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo leo Jumatatu, Novemba 2, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Rehema Tukai, amesema kambi ya Kinduni inafungua rasmi awamu ya pili ya mpango endelevu unaolenga kuendesha angalau kambi mbili kila mwaka hadi mwaka 2029.
“Baada ya kambi zilizotangulia kufanikiwa, inaanza kambi mpya ambayo inalenga kuwafikia wananchi 50,000,” amesema Rehema.
Amesema wananchi watanufaika na huduma za kibingwa, zikiwamo za matibabu ya macho, meno, ngozi, moyo, mifupa, afya ya wanawake na watoto, masikio, pua na koo, pamoja na magonjwa ya mfumo wa njia ya mkojo.
Pia, kutakuwa na uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo ya shinikizo la damu na kisukari, pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake.
Katika huduma za afya ya uzazi, amesema zitatolewa chanjo za kawaida, huduma za utunzaji wa ujauzito, huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana, huduma za afya ya akili, elimu ya maisha na ushauri nasaha.
“Kambi pia itatoa huduma za utambuzi na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, elimu ya lishe na matumizi ya mwani kama lishe endelevu, pamoja na zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya hospitali,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya ZMBF, Makame Machano Haji, amesema kambi hiyo itashirikisha timu ya wataalamu wa afya zaidi ya 100 walioidhinishwa na Wizara ya Afya, wakiwamo madaktari bingwa kutoka India.
“Huduma zitatolewa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kila siku bila malipo yoyote,” amesema Makame.
Amesema ZMBF itatumia mfumo wa kidijitali wa Wizara ya Afya, Zan-EMR, kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu za wagonjwa kwa lengo la kulinda usiri na faragha zao.
Ameongeza kuwa mwananchi atakayebainika kuwa na tatizo linalohitaji matibabu ya rufaa, ZMBF itagharamia na kusimamia mchakato huo hadi katika hospitali kuu au hata nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Galos Nyimbo, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kaskazini B, mkoa huo na mikoa jirani ya Kusini na Mjini Magharibi kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma hizo.
Amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kupima afya zao mapema, kwa kuwa huduma za vipimo, dawa na miwani zitatolewa bila malipo.
“Kambi hii iko wazi kwa wananchi wote kutoka sehemu yoyote ya Zanzibar bila ubaguzi wowote wa kimaeneo,” amesema.
Meneja wa Kampuni ya Yas, Mohamed Wakid Mohamed, ambaye ni mdhamini mkuu wa kampeni hiyo, amesema nia ya kampuni hiyo ni kuleta mabadiliko chanya na kurejesha kwa jamii.
Ufunguzi rasmi wa kambi hiyo utafanywa kesho Jumanne, Novemba 3, na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui.
Kambi hiyo itahitimishwa Novemba 7 kwa matembezi ya kilomita tano yatakayoanzia saa 12:00 asubuhi katika Uwanja wa Kitope. Matembezi hayo yataongozwa na Mama Mariam Mwinyi pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah.
You may also like

Tanzania – Fire Damages Six Hotels in Zanzibar

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund


Leave a Reply