

Tanzania, Zambia na China zaweka mkakati mpya wa Tazara
Dar es Salaam. Miaka 50 baada ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kuanza shughuli za kibiashara, mataifa matatu yaliyoijenga yamekutana kujadili namna ya kuibadilisha kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara ya kikanda.
Katika mkutano wa kwanza wa uratibu wa pande tatu uliofanyika Dar es Salaam, Novemba 24, 2026, Tanzania, Zambia na China zimejadili utekelezaji wa mradi wa kuifufua reli hiyo kupitia mpango wa kuanzisha Ukanda wa Ustawi wa Tazara (Tazara Railway Prosperity Belt).
Mpango huo unalenga kuunganisha miundombinu ya usafiri na uwekezaji katika sekta za madini, kilimo, umwagiliaji, viwanda, nishati, maghala na biashara, ili maeneo yanayopitiwa na reli yanufaike na uzalishaji na ajira.
Akizungumza katika mkutano huo, leo Jumanne, Novemba 24, 2026, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe, aliyewakilisha Tanzania, amesema nchi inataka ufufuaji wa Tazara ulete matokeo yanayogusa uchumi na maisha ya wananchi, badala ya kuishia kwenye ukarabati wa miundombinu.
“Tunataka Tazara iwe zaidi ya njia ya kupitisha mizigo. Iwe kichocheo cha uzalishaji, biashara ya kuvuka mipaka, uwekezaji na ujenzi wa uwezo wa wananchi katika maeneo yanayopitiwa na reli,” amesema.
Tanzania yaweka vipaumbele vitatu
Maghembe amesema Tanzania imeweka vipaumbele vitatu katika ushirikiano huo, kikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa ufufuaji kwa kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatafsiriwa katika hatua zinazoonekana, ratiba na mifumo ya pamoja ya kusimamia maendeleo yake.
Kipaumbele cha pili ni kuhakikisha Ukanda wa Ustawi unajumuisha wananchi na kuleta manufaa kwa pande zote, kupitia uwekezaji unaochochea uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa, kukuza biashara ya mipakani na kuimarisha ujasiriamali.
Kipaumbele cha tatu ni kuimarisha mashauriano na uratibu wa nchi hizo kwa kuzingatia uwazi, kuaminiana, kuheshimu mamlaka ya kila nchi na kufanya maamuzi kwa umiliki wa pamoja.
“Ufanisi wa mradi huu hautapimwa kwa urefu wa reli iliyokarabatiwa au tani za mizigo pekee, bali pia kwa ajira zitakazozalishwa, biashara zitakazokua na namna wananchi watakavyoboresha maisha yao,” amesema.
Zambia yataka Kapiri Mposhi iwe kitovu
Kwa upande wa Zambia, matarajio ni kutumia reli hiyo kusafirisha ongezeko la uzalishaji wa madini na kufungua fursa mpya katika kilimo na viwanda.
Naibu Katibu wa Baraza la Mawaziri anayeshughulikia Fedha na Maendeleo ya Uchumi, Siazongo Davie Siakalenge, aliyewakilisha nchi hiyo, amesema Zambia inalenga kuongeza uzalishaji wa shaba kutoka kiwango cha chini kidogo ya tani milioni moja kwa mwaka hadi takribani tani milioni tatu ifikapo mwaka 2031.
Amesema Tazara inapaswa kuwa njia muhimu ya kusafirisha shaba hiyo, pamoja na kuingiza pembejeo na bidhaa nyingine nchini humo ili kuongeza mizigo ya pande zote na kupunguza safari za mabehewa yakiwa matupu.
“Tunapoongeza uzalishaji wa shaba, tunahitaji reli yenye uwezo wa kusafirisha bidhaa hizo, lakini pia kuingiza pembejeo zinazohitajika katika uzalishaji. Hapo ndipo matumizi ya reli yatakuwa na tija katika pande zote mbili,” amesema.
Siakalenge ameziomba Tanzania na China kuridhia kituo cha Kapiri Mposhi nchini Zambia kifanyiwe usanifu upya na kuboreshwa, akisema miundombinu yake ya sasa haitoshi kutekeleza nafasi inayotarajiwa katika mpango huo.
Ametaka kituo hicho kiendelezwe kuwa kitovu cha usafirishaji kinachoweza kuhudumia ukanda wa Kusini, Mashariki na Kati mwa Afrika, kupitia miunganiko ya barabara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Angola, Zimbabwe na Afrika Kusini.
China yasisitiza ushirikiano
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Miao Deyuz, amesema mkutano huo ni hatua muhimu ya kuimarisha uratibu wa kisiasa na kiutendaji kati ya mataifa hayo.
Amesema uamuzi uliofikiwa Septemba 2024 na Rais Xi Jinping wa China, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia uliweka msingi wa hatua zinazojadiliwa sasa.
Ameongeza kuwa mwaka uliofuata mataifa hayo yalitoa tamko la pamoja kuhusu kujenga Ukanda wa Ustawi wa Tazara na kwamba kazi za ujenzi zimeanza na zinaendelea.
“Jukumu letu sasa ni kugeuza maafikiano ya viongozi hao kuwa hatua za pamoja. Mkutano huu unatupa nafasi ya kuoanisha mitazamo, kuimarisha imani na kuweka mazingira ya kisera yatakayowezesha mradi kusonga mbele,” amesema.
Tazara ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kwa mkopo usio na riba kutoka China na kuanza shughuli za kibiashara mwaka 1976.
Mwaka 2025, Tanzania, Zambia na China zilizindua rasmi mradi wa kufufua reli hiyo kupitia mkataba wa uwekezaji wa Dola za Marekani 1.4 bilioni (takribani Sh3.6 trilioni) kwa kipindi cha miaka 31.
Mradi huo unahusisha ukarabati wa kilomita 1,860 za reli, ununuzi wa injini 34 za treni, mabehewa 760 ya mizigo na 16 ya abiria.
You may also like

Tanesco yatekeleza agizo la Ndejembi la Novemba 15

Chadema issues conditions before reconciliation


Leave a Reply