

Serikali yalipa Sh4.2 bilioni kwa mwaka kuendesha Hospitali ya Lumumba
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inalipa Sh351 milioni kila mwezi kwa Kampuni ya NSK kwa ajili ya kuendesha Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Lumumba, Zanzibar.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 25, 2026 katika Baraza la Wawakilishi, wakati Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub, akiuliza uzoefu wa kampuni hiyo, kiwango cha malipo wanayopokea na mpango wa kuhamisha utaalamu kwa wazawa.
Kiwango hicho ni sawa na takribani Sh4.2 bilioni kwa mwaka.
Akijibu, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, amesema Kampuni ya NSK ina uzoefu wa kuendesha Hospitali ya NSK jijini Arusha yenye hadhi ya Mkoa.
“Serikali inatumia Sh351 milioni kila mwezi katika uendeshaji wa hospitali hiyo,” amesema Hassan Khamis Hafidh.
Amesema uhamisho wa utaalamu kwa wazawa unafanyika kupitia mafunzo kazini (mentorship) na kambi za matibabu.
Katika kikao hicho hicho, Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Moza Mohammed Khamis, amehoji hatua zinazochukuliwa dhidi ya madaktari wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Chake Chake Pemba, wanaotuhumiwa kuwafanyia vitendo visivyo vya kimaadili wagonjwa wa kike.
Naibu Waziri ameihaidi Baraza kuchunguza tuhuma hizo. Amesema endapo zitathibitika, hatua za kisheria na za kinidhamu zitachukuliwa, ikiwemo kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya ulinzi endapo kuna viashiria vya jinai.
Pia Serikali imeahidi kupokea taarifa kutoka kwa waathirika kwa usiri mkubwa.
Kuhusu uuzwaji holela wa dawa za sumu ya panya, Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Chumu Kombo Khamis, ameuliza mpango wa Serikali wa kudhibiti biashara hiyo.
Akijibu, Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa rasimu ya Kanuni mpya za Udhibiti na Usimamizi wa Matumizi ya Sumu Zanzibar, ili kuweka utaratibu thabiti wa uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa za sumu.
Rasimu hiyo imewasilishwa kwa wadau kupata maoni.



Leave a Reply