

Vijana wa JKU wadai kucheleweshewa mishahara hadi miezi 22
Unguja. Vijana walioajiriwa kwa mikataba kupitia Wakala wa Ulinzi wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) wanadai kucheleweshewa malipo yao kwa muda mrefu, baadhi wakitaja kufikisha miezi 22.
Hoja hiyo imeibuliwa leo Jumatano, Novemba 25, 2026, Barazani na Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT Wazalendo), aliyehoji sababu za ucheleweshaji huo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa, amekiri kuwapo kwa changamoto ya kuchelewa kwa malipo, lakini akakanusha madai kuwa vijana hao wamekaa miezi 22 bila kulipwa.
Hata hivyo, Waziri huyo hakueleza muda ambao malipo yamekuwa yakichelewa wala idadi ya vijana walioathirika na hali hiyo.
Ametaja sababu kuu ya changamoto hiyo kuwa ni taasisi mbalimbali kushindwa kulipa madeni yanayodaiwa na wakala huo, unaoendesha shughuli zake kibiashara kwa mujibu wa sheria.
“Serikali kupitia OR-Tamisemi imeanza kuziandikia barua taasisi zenye madeni ili zilipe, kwani wakala huo unaendeshwa kibiashara kwa mujibu wa sheria,” amesema Kitwana.
Katika kikao hicho, suala la gharama za kambi za masomo pia limeibuliwa na Mwakilishi wa Ziwani, Mohammed Ali Salim (ACT Wazalendo), aliyehoji kama Serikali inatambua kuwa michango ya kambi imekuwa mzigo kwa wazazi.
Akijibu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mboja Ramadhan Mshenga, amesema Serikali inatambua michango hiyo inayolenga kugharamia chakula na malazi ya wanafunzi wakati wa kambi za masomo.
Amesema uratibu wa michango hiyo hufanywa na kamati za shule kwa kushirikiana na wazazi, akisisitiza kuwa kiasi kinachokusanywa kinapaswa kuwa na uhalisia na kukubaliwa kwa pamoja.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa michango hiyo haipaswi kuwa kikwazo kwa mwanafunzi kupata elimu au kufanya mitihani.
“Michango lazima iwe na uhalisia na kukubaliwa kwa pamoja, na kutolipa mchango wa kambi haitakiwi kabisa kuwa sababu ya kumzuia mwanafunzi kuhudhuria masomo au kufanya mitihani,” amesema Mshenga.




Leave a Reply