

Wadau waibana Serikali kuhusu kalenda ya ufadhili
Dar es Salaam. Ndoto ya kijana kusoma katika chuo kikuu cha kimataifa inaweza kukwama kabla hata ya kuanza mchakato wa maombi, si kwa kukosa sifa za kitaaluma, bali kutofahamu fursa zilizopo, muda wa kuomba au kushindwa kumudu gharama za maandalizi.
Changamoto hiyo imeibua umuhimu wa mpango wa Serikali wa kuandaa kalenda ya fursa za ufadhili wa masomo nje ya nchi ili kutoa nafasi ya Watanzania wenye sifa kuzifikia fursa hizo.
Novemba 20, 2026, wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi 90 wanufaika wa Samia Scholarship Extended wanaokwenda katika vyuo mbalimbali nchini Algeria, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alitangaza mpango wa kuandaa kalenda hiyo.
Alisema lengo ni kuwawezesha wananchi kufahamu mapema muda wa kutuma maombi katika programu mbalimbali za ufadhili wa masomo zinazotolewa na nchi na taasisi za kimataifa.
Wakizungumza na Mwananchi leo Novemba 25,2026 wadau wa elimu wamesema kalenda hiyo haipaswi kuwa orodha ya tarehe za kutuma maombi pekee, bali iwe nyenzo ya kuondoa vikwazo vinavyowazuia vijana wenye sifa kupata fursa hizo.
Wamesema pia ni muhimu Serikali kuhakikisha maarifa yanayopatikana kupitia ufadhili huo yanatumika kuimarisha sekta mbalimbali na kuchochea maendeleo ya nchi.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo, mchambuzi wa elimu, Scolastica Maricha amesema moja ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele ni usawa wa upatikanaji wa taarifa, ili fursa hizo zisiwanufaishe zaidi vijana wanaoishi mijini au wenye uwezo wa kufuatilia mitandao ya kimataifa.
Amesema kalenda hiyo inapaswa kuonyesha zaidi ya muda wa kutuma maombi, ikiwemo sifa zinazohitajika, nyaraka za kuandaa, gharama zinazoweza kujitokeza na namna ya kuwasilisha maombi.
“Ushirikishwaji wa shule, vyuo vikuu, ofisi za elimu za halmashauri na vyombo vya habari unaweza kusaidia kuwafikia vijana wengi zaidi, wakiwemo wanaoishi maeneo yenye upatikanaji mdogo wa intaneti.
“Pia, uwepo wa mfumo mmoja wa kidijitali unaokusanya taarifa za ufadhili kutoka nchi na taasisi mbalimbali unaweza kurahisisha ufuatiliaji wa nafasi hizo na kuwawezesha waombaji kupata taarifa kwa wakati,” amesema.
Amesema usambazaji wa taarifa kupitia njia mbalimbali utasaidia vijana wengi kutambua nafasi zinazolingana na uwezo na taaluma zao, badala ya kutegemea mitandao ya kijamii au taarifa zinazopatikana kupitia watu wanaowafahamu.
Kwa upande wake, mhadhiri wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Amina Msuya amesema pamoja na upatikanaji wa taarifa, uwezo wa kifedha ni changamoto nyingine inayopaswa kuangaliwa ili wanafunzi wanaokidhi vigezo wasikose nafasi kutokana na gharama za maandalizi.
Amesema baadhi ya ufadhili hugharamia ada na mahitaji ya mwanafunzi akiwa chuoni, lakini haujumuishi gharama za tiketi za ndege, pasipoti, vipimo vya afya na mahitaji mengine yanayotangulia safari.
Changamoto hiyo, amesema inaweza kuwanyima nafasi vijana wenye uwezo wa kitaaluma lakini wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.
Kwa msingi huo, amesema kalenda ya ufadhili inapaswa kuambatana na taarifa za kina kuhusu gharama zinazohitajika ili waombaji wajipange mapema na Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wale wanaokosa uwezo wa kugharamia maandalizi.
Naye Kenneth Kichogo ambaye ni mdau wa elimu amesema kuanzishwa kwa kalenda ya ufadhili wa masomo ni hatua inayoweza kuongeza uwazi na usawa katika upatikanaji wa fursa za elimu ya kimataifa.
Hata hivyo, amesema Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo huo unakuwa na taarifa za kutosha kuhusu aina za ufadhili, nchi zinazotoa nafasi, kozi zinazohitajika, vigezo vya waombaji na muda wa kutuma maombi.
Amesema changamoto nyingine ni vijana kukosa mwongozo wa namna ya kuomba nafasi hizo licha ya kuwa na sifa zinazohitajika.
“Serikali isiishie kuweka kalenda na kutangaza nafasi, bali iweke pia utaratibu wa kuwaongoza vijana namna ya kuomba, kuandaa nyaraka na kukidhi vigezo vya vyuo vinavyotoa ufadhili. Wapo vijana wenye uwezo mkubwa kitaaluma lakini wanakosa fursa kwa sababu hawajui taratibu za kuomba,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, taasisi za elimu na Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kuongeza idadi ya nafasi za ufadhili na kupanua wigo wa wanufaika.
Kichogo amesema uwekezaji katika ufadhili wa masomo nje ya nchi unapaswa kuangaliwa kwa mtazamo wa maendeleo ya taifa, kwa kuhakikisha wanafunzi wanaporejea wanapata mazingira ya kutumia maarifa na teknolojia walizojifunza.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuhakikisha ufadhili huo hauishii kuwa manufaa kwa mwanafunzi mmoja mmoja, bali unakuwa uwekezaji wa muda mrefu katika rasilimali watu na maendeleo ya Tanzania.
You may also like

Mwabunguru alivyoibuka rais mpya Tucta katikati mgawanyiko

Tanzania PM Nchemba to lead World AIDS Day commemorations in Dodoma


Leave a Reply