

Serikali yaimarisha mifumo ya kupambana na ukatili wa kijinsia
Dodoma. Serikali imesema inaendelea kuimarisha mifumo ya kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kuboresha huduma za kisheria, kuongeza ulinzi kwa waathirika na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.
Hatua hizo zinalenga kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi katika mazingira salama, wanapata haki na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoendelea kuwa changamoto katika jamii.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, amesema hayo leo Jumatano, Novemba 25, 2026, wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Amesema mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali, akisisitiza kuwa suala hilo halipaswi kuchukuliwa kama changamoto ya kijamii pekee, bali pia linahusu haki za binadamu na utawala wa sheria.
“Ukatili wa kijinsia si suala la kijamii pekee, bali pia ni suala la haki za binadamu, utawala wa sheria, uwajibikaji na usawa mbele ya sheria,” amesema katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega.
Katimba amesema Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili wa mwaka 2024/25 hadi 2028/29.
Akizungumzia hatua za kisheria, amesema katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2026, jumla ya mashauri 13,411 ya ukatili wa kijinsia yalisajiliwa katika mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo.
Amesema kati ya mashauri hayo, 9,333 yalisikilizwa na kutolewa hukumu, huku washtakiwa 5,562, sawa na asilimia 60 ya waliotajwa katika mashauri yaliyohukumiwa, wakipatikana na hatia na kupewa adhabu mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali imesajili watoa huduma 2,033 na mashirika 275 yanayotoa msaada wa kisheria kwa wananchi, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa makundi yenye uhitaji.
Katika kukabiliana na ukatili unaotokana na matumizi mabaya ya teknolojia, Katimba amesema Serikali inaendesha kampeni ya kitaifa ya ulinzi wa watoto mtandaoni katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (WiLDAF), Dk Monika Mhoja, ameiomba Serikali kuongeza juhudi za kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na mauaji yanayohusishwa na vitendo hivyo.
Amesema hatua muhimu katika mapambano hayo ni kuhakikisha familia zinaishi katika mazingira salama, huku akitaka Serikali kuweka kipaumbele katika kutunga sheria mahususi ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Dk Mhoja pia ameshauri kukamilishwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili kukomesha ndoa za utotoni, pamoja na kufanya mageuzi ya sheria za mirathi kwa lengo la kulinda haki za wanawake na watoto yatima wanaonyimwa haki zao.
Amewataka viongozi wa dini, familia na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii na kupinga vitendo vya ukatili.
You may also like

Finland commits Sh1.45 billion to boost Tanzania’s green enterprises

VP Ndejembi orders review of pharmacy staffing needs


Leave a Reply