

Wadau washauri Oktoba 29 iwe siku ya kusaka amani
Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeitaka Serikali kutenga Oktoba 29 ya kila mwaka kuwa siku ya kitaifa ya kumbukizi ya waathirika wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mtandao huo umemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kulifanyia kazi pendekezo hilo, ukisema siku hiyo itatoa fursa kwa taifa kuwakumbuka waliopoteza maisha, kutambua maumivu ya familia zilizoathirika na kujifunza kutokana na matukio hayo ili yasijirudie.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 23, 2026, Mratibu wa kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema mtandao huo ulitoa pendekezo hilo mwaka 2025 na kulirejesha Februari 2026, ukisisitiza umuhimu wa kumbukizi, kutafuta ukweli na haki, uwajibikaji na uponyaji wa kitaifa.
Amesema kumbukizi hiyo haipaswi kuishia katika maombolezo pekee, bali iwe fursa ya kujifunza kutokana na historia, kuimarisha haki za binadamu na kuchukua hatua za kuzuia ukiukwaji wa haki na matumizi yasiyo halali ya nguvu.
“Lengo kuu la kumbukizi hii si kuwakumbuka wahanga pekee, bali kuhakikisha kwamba matukio yanayosababisha upotevu wa maisha, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na matumizi yasiyo halali ya nguvu hayajirudii tena nchini Tanzania,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Olengurumwa amesema pendekezo hilo linazingatia pia mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Kwa mujibu wa THRDC, tume hiyo ilipowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ilipendekeza Serikali kutenga siku maalumu ya maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya kuwakumbuka waliopoteza maisha katika matukio hayo.
Mtandao huo umesema Oktoba 29, 2026 inapotimia mwaka mmoja tangu matukio hayo, ni muhimu kutafakari namna ya kuponya majeraha, kuzuia yasijirudie na kushughulikia visababishi vilivyobainishwa na wananchi pamoja na tume hiyo.
“Kumbukizi hiyo inapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kujenga maridhiano ya kitaifa, bila kugeuka chanzo cha chuki, uhasama au kulipiza kisasi. Badala yake, iwe fursa ya kutafuta ukweli, kuimarisha haki na kujenga mshikamano miongoni mwa Watanzania,” imeeleza taarifa hiyo.
Shughuli zitakazoambatana na kumbukizi
Katika mapendekezo yake, THRDC imeshauri kumbukizi ya kwanza kufanyika Oktoba 29, 2026, kwa kuwashirikisha familia za waathirika, taasisi za umma, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi katika shughuli za kitaifa, kimkoa na kiwilaya.
Shughuli hizo zinapendekezwa kujumuisha ibada, sala na dakika za ukimya kuwaenzi waliopoteza maisha, pamoja na majukwaa salama yatakayowezesha familia za waathirika kutoa ushuhuda kwa hiari na kueleza mahitaji yao.
Pia, mtandao huo umependekeza kongamano la kitaifa kuhusu ukweli, haki, maridhiano na hatua za kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na maonyesho ya nyaraka za kihistoria zilizothibitishwa.
Mapendekezo mengine ni kutoa elimu kwa vijana na wanafunzi wa shule na vyuo kuhusu uhai, haki za binadamu na amani, na kuweka utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu sahihi za matukio hayo kwa kuzingatia ridhaa, faragha na usalama wa wahusika.
THRDC imetaka pia kuanzishwa kwa makumbusho rasmi ya matukio hayo ili kuhifadhi historia na kuwezesha vizazi vijavyo kujifunza kutokana na yaliyotokea. Aidha, imependekeza kutolewa kwa taarifa ya kila mwaka ya kutathmini utekelezaji wa mapendekezo na maboresho yanayofanyika.
Mtandao huo umesisitiza kuwa kumbukizi hiyo inapaswa kwenda sambamba na uchunguzi wa kuaminika, upatikanaji wa haki kwa wahanga na uwajibikaji pale makosa yatakapothibitishwa. Umeeleza kuwa maridhiano hayapaswi kutumika kama mbadala wa ukweli na haki.
Vilevile, umetaka kutathmini namna vyombo vya usalama vinavyotekeleza wajibu wa kulinda raia, matumizi halali na yenye uwiano ya nguvu na mifumo huru ya kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Demokrasia na kumbukumbu za kihistoria
Kuhusu demokrasia na uchaguzi, THRDC imesema siku hiyo inaweza kuwa fursa ya kujadili maboresho ya mifumo ya uchaguzi, elimu ya uraia, uvumilivu wa maoni tofauti na utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na kisheria.
Mtandao huo umetaja mifano ya nchi na taasisi zinazotenga siku maalumu kwa ajili ya kumbukizi. Rwanda huadhimisha kumbukizi ya mauaji ya kimbari kuanzia Aprili 7, huku Afrika Kusini ikiadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Machi 21, inayohusishwa na mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1960. Umoja wa Mataifa nao hutambua Desemba 9 kwa ajili ya kumbukizi na utu wa waathirika wa mauaji ya kimbari na kuzuia uhalifu huo.
THRDC imesema mifano hiyo inaonyesha umuhimu wa kumbukizi katika kuwaenzi waathirika, kuhifadhi historia na kuzuia ukatili usijirudie.
Kaulimbiu inayopendekezwa ni: “Kumbukizi, Ukweli, Haki, Uwajibikaji na Uponyaji, Kamwe Yasijirudie Tena.”
Taarifa hiyo imesema uongozi wenye maono haupaswi kufuta kumbukumbu za nyakati ngumu, bali unapaswa kuzikabili kwa ujasiri na kuzitumia kujenga Taifa lenye umoja, haki na maridhiano ya kudumu.
“Tunawakumbuka wahanga, tunajifunza kutokana na historia, na tunachukua hatua kuhakikisha yasijirudie tena,” imesema taarifa hiyo.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations

Leave a Reply