

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola
Dar es Salaam. Mjasiriamali wa teknolojia kutoka Tanzania, Julius Mbungo ametambuliwa miongoni mwa vijana 100 waliochaguliwa kupokea tuzo za mwaka 2026 za Queen Elizabeth II Commonwealth Trust, kutokana na juhudi zake za kutumia teknolojia kupanua fursa kwa mafundi na wafanyakazi wenye ujuzi katika sekta isiyo rasmi.
Mbungo, mwanzilishi wa majukwaa ya teknolojia ya Toolboksi na Spana, ambaye amezungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026 kihusiana na tuzo hiyo, amesema kutambuliwa huko kunahusiana na juhudi za kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi hao, zikiwamo za kupata wateja, taarifa za kitaalamu na zana za kusimamia biashara zao.
Tuzo hizo zinatambua vijana wanaotumia ubunifu na juhudi zao kutatua changamoto katika jamii za nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola. Tuzo za mwaka huu zinaambatana na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Malkia Elizabeth II.
Mbali na tuzo hiyo, Mbungo alialikwa kwa amri ya Mfalme Charles III kuhudhuria mapokezi yaliyoandaliwa na Mfalme na Malkia Camilla katika Kasri la St James’s jijini London, Uingereza, ambako alikutana na viongozi hao wa kifalme.
“Utambuzi huu una maana kubwa kwangu kwa sababu unatambua kazi inayogusa maisha ya kila siku ya wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi nchini Tanzania. Kupitia Toolboksi na Spana, lengo langu ni kuwasaidia watu wenye ujuzi kupata fursa, kuboresha kazi zao na kujenga maisha bora,” amesema.
Amesema tuzo hiyo na mwaliko wa kuhudhuria mapokezi ya kifalme vimeimarisha imani kuwa ubunifu unaotokana na changamoto za ndani ya Tanzania unaweza kutambuliwa kimataifa.
Akizungumzia ujumbe wake kwa vijana wengine nchini, Mbungo amesema hawapaswi kusubiri hadi wawe na majibu ya kila changamoto kabla ya kuanza kutekeleza mawazo yao.
“Nina tumaini utambuzi huu utawatia moyo vijana wengine wa Tanzania kuyachukulia kwa uzito mawazo yao na kuanza kutatua changamoto zinazowazunguka. Si lazima usubiri hadi uwe na kila kitu ndipo utoe mchango wenye manufaa. Jamii zetu zinahitaji ubunifu, ujuzi na dhamira yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa heshima hiyo inampa wajibu mkubwa zaidi wa kuendeleza kazi yake, kushirikisha wengine maarifa anayopata na kusaidia kufungua fursa kwa watu wengine.
Kupitia Toolboksi, Mbungo anawaunganisha mafundi wenye ujuzi na kaya pamoja na biashara zinazohitaji huduma za ukarabati, matengenezo, ufungaji na kazi nyingine maalumu. Jukwaa hilo linalenga kuwasaidia mafundi kupata wateja zaidi na kupanua wigo wa fursa za kazi nje ya mitandao yao ya kawaida.
Spana inalenga mafundi wa magari kwa kutumia teknolojia ya akili unde kutoa mwongozo wa kutambua hitilafu na kufanya matengenezo. Mfumo huo pia una vipengele vya kusaidia usimamizi wa wateja, historia ya huduma zilizotolewa na kumbukumbu za fedha kwa njia ya kidijitali.
Baada ya mapokezi hayo, Mbungo alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki, kujadili uwezekano wa kupata msaada zaidi wa kuendeleza shughuli zake kupitia Toolboksi na Spana.
Balozi Mbelwa amesema mpango wa tuzo hizo pia huwapa washindi fursa za kupata ushauri wa kitaalamu, kuimarisha uwezo wa taasisi au miradi yao na kuunganishwa na wadau, washirika na wafadhili wanaoweza kusaidia kuendeleza kazi zao.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply