

DC avunja sherehe ya mahari ya mwanafunzi Bariadi
Bariadi. Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Saimon Simalenga, akiambatana na askari wa Jeshi la Polisi, amevunja sherehe ya kupokea mahari ya mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa akitarajiwa kuolewa kwa mahari ya ng’ombe 16 katika Kijiji cha Igaganulwa, Kata ya Dutwa, wilayani humo.
Mwanafunzi huyo, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama, alikuwa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Igaganulwa na alikuwa amemaliza mitihani ya kidato cha nne akisubiri matokeo.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 25, 2026, nyumbani kwa dada wa mwanafunzi huyo, ambako sherehe ya kupokea mahari ilikuwa ikiendelea.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi,Saimon Simalenga akizungumza na waandishi wa habari(hawako pichani) jinsi alivyovunja sherehe ya utoaji wa mahari kwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika kijiji cha Igaganulwa. Picha na Samwel Mwanga
Mwanaume aliyetaka kumuoa mwanafunzi huyo ni Joseph Lafael, maarufu kama Bonge, ambaye ni wakala wa mabasi katika eneo la Dutwa. Inadaiwa kuwa tayari ana mke mwingine, hivyo mwanafunzi huyo angekuwa mke wake wa pili.
Akizungumza na wananchi waliokuwapo katika eneo la tukio, Simalenga amesema kuwa Serikali haitakubali watoto kulazimishwa kuolewa au kuoa katika umri unaoweza kuathiri haki zao na ndoto zao za kielimu.
Amesema mwanafunzi huyo alikuwa amemaliza mitihani ya kidato cha nne na alikuwa akisubiri matokeo, hivyo hatua ya kutaka kumuozesha kabla ya kuendelea na safari yake ya kielimu haikubaliki.
Afisa Mtendaji Kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi,Jackson Mangu akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya sakata la kutaka kuozeshwa kwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika kijiji cha Igaganulwa. Picha na Samwel Mwanga
“Hatuwezi kukubali mtoto wa kike au wa kiume azuiwe kutimiza ndoto zake. Tumesaini mikataba ya kimataifa inayolinda haki za watoto, na hata Katiba ya nchi inalinda haki hizo. Wote wanaokiuka haki za watoto tutawachukulia hatua za kisheria, kama tulivyofanya hapa leo,” amesema.
Aliongeza kuwa Serikali katika wilaya hiyo itaendelea na misako ili kubaini na kuwachukulia hatua watu wanaohusika na kuwaozesha wanafunzi kabla ya kukamilisha masomo yao.
“Mwanafunzi huyo angewezaje kuendelea na masomo endapo angeolewa na kupata ujauzito baada ya kufaulu mitihani yake,”alihoji.
Kutokana na tukio hilo, Simalenga aliamuru kukamatwa kwa watu wote waliohusika, akiwamo dada wa mwanafunzi huyo na mwanaume aliyetaka kumuoa, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Mwanafunzi alalamika kulazimishwa kuolewa
Esther Manyangu ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, amesema kuwa walipokuwa shuleni, mwenzao huyo alimweleza kuwa hakutaka kuolewa, lakini alikuwa akilazimishwa kufanya hivyo.
Joseph Lafael (wa kwanza kushoto)akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi alituhumiwa kutaka kumuoa mwanafunzi wa kidato cha nne katika kijiji cha Igaganulwa. Picha na Samwel Mwanga
Amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, mwanafunzi huyo alimfuata ili aende kushuhudia shughuli ya utoaji wa mahari iliyokuwa ikiendelea nyumbani kwa dada yake.
Naye Baraka Nzuga, mwanafunzi wa shule hiyo, aliunga mkono hatua ya mkuu wa wilaya hiyo kuvunja sherehe hiyo, akisema watoto wanapaswa kupewa nafasi ya kusoma na kutimiza malengo yao ya baadaye.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dutwa, Jackson Mangu, amesema kuwa hilo si jaribio la kwanza la kutaka kumuozesha mwanafunzi huyo.
Amesema kuwa mwaka 2023, wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akijiandaa kujiunga na kidato cha kwanza, kulikuwa na jaribio la kumuozesha, lakini lilishindikana baada ya uongozi wa Serikali katika ngazi ya kata kuingilia kati na kuhakikisha anarejea shuleni.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia tukio hilo walitaka elimu zaidi itolewe kwa jamii kuhusu madhara ya kuwaozesha watoto katika umri mdogo.
John Martine amesema utoaji wa elimu kwa jamii ni muhimu ili wazazi na walezi waelewe madhara ya kuwalazimisha watoto kuingia katika ndoa kabla ya kukamilisha masomo yao.
Ngombe 16 ikiwa ni mahari kwa ajili ya kumuoa mwanafunzi wa kidato cha nne katika kijiji cha Igaganulwa wilaya ya Bariadi. Picha na Samwel Mwanga
Naye Rebeka Eliakimu alitaka wote waliohusika katika maandalizi ya kumuozesha mwanafunzi huyo wafikishwe katika vyombo vya sheria, akidai kuwa vitendo vya aina hiyo vimekuwa vikijitokeza mkoani Simiyu, hasa katika kipindi ambacho wanafunzi wanamaliza mitihani ya kitaifa.
“Ni muhimu kwa mamlaka husika kuimarisha ufuatiliaji ili kuzuia wanafunzi kuozeshwa baada ya kumaliza mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne,”amesema.
Kwa upande wake, Joseph Mihujo amesema kuwa ni muhimu wazazi na walezi kuwapa watoto nafasi ya kuendelea na masomo badala ya kukatisha ndoto zao kwa masilahi ya muda mfupi.
“Watoto hawa ni sehemu ya kizazi kitakachotoa viongozi na wataalamu wa baadaye, hivyo wanapaswa kulindwa na kupewa fursa ya kutimiza malengo yao,”amesema.
You may also like

Mradi wa umeme Songea –Tunduru kufungua fursa za kiuchumi kusini

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi


Leave a Reply