

Sh1.27 bilioni kujenga shule, LNG kuipa Lindi sura mpya
Lindi. Wananchi wa Lindi wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kuchakata na kusafirisha gesi asilia (LNG), ambao Serikali imesema maandalizi yake yamefikia hatua nzuri, huku ikiendelea kutekeleza miradi ya kijamii kabla ya uwekezaji huo kuanza rasmi.
Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ikizindua Shule ya Msingi Likong’o iliyojengwa kwa gharama ya Sh1.27 bilioni kupitia ushirikiano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za kimataifa za nishati za Shell na Equinor, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Akizungumza leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, wakati wa uzinduzi wa shule hiyo iliyopo Manispaa ya Lindi, Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera, amesema Serikali itahakikisha uwekezaji unaofanywa chini ya wizara hiyo unaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Amesema mradi wa LNG utakapotekelezwa, Lindi inatarajiwa kupata sura mpya kiuchumi, hivyo kuwataka wananchi kujiandaa kutumia fursa zitakazojitokeza.
“Mradi wa LNG upo mbioni kuanza kutekelezwa. Wananchi waanze kutunza ardhi zao kwa sababu watu watakuja kununua maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, ikiwamo viwanda vya mbolea,” amesema.
Dk Homera amesema mabadiliko yanayotarajiwa kutokana na mradi huo yataifanya Lindi kuwa tofauti na ilivyo sasa, akisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandaa kunufaika na uwekezaji huo.
Ameagiza shule hiyo ianze kutumika kesho Jumanne, Oktoba 27, ili wanafunzi waanze kupata elimu katika mazingira bora yanayotokana na uwekezaji wa sekta ya gesi asilia.
Shule hiyo imejengwa ikiwa na madarasa tisa, madarasa ya elimu ya awali, jengo la utawala, nyumba mbili za walimu, vyoo pamoja na meza na madawati. Inatarajiwa kuhudumia wanafunzi kati ya 350 na 400.
Mazungumzo yafikia hatua nzuri
Akizungumzia maendeleo ya mradi wa LNG, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, James Mataragio, amesema mazungumzo kati ya Serikali na wawekezaji yamefikia hatua nzuri, huku baadhi ya masuala muhimu yakiwa yamekubaliwa.
Amesema mradi huo unatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 50 na kuwa na mchango katika kukuza uchumi wa eneo hilo kupitia ajira na uwekezaji katika huduma za kijamii.
“Mradi huu utaanza mapema iwezekanavyo. Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na tumefikia hatua nzuri. Tumeshakubaliana mambo ya kikodi na kibiashara. Kilichobaki ni kujadiliana kuhusu sheria ya mradi ambalo ni jambo muhimu zaidi,” amesema.
Alifafanua Serikali inapanga kuwasilisha bungeni sheria maalumu itakayoweka mfumo wa kusimamia mradi huo, kwa kuzingatia masilahi mapana ya Watanzania na usalama wa uwekezaji.
Mataragio amesema licha ya mradi huo kutokuwa umeanza rasmi, Serikali na wawekezaji wameona umuhimu wa kuanza kuwanufaisha wananchi kupitia miradi ya kijamii, ikiwamo ujenzi wa shule hiyo.
Alitaja sekta za afya, maji, miundombinu na ajira kuwa miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kunufaika na uwekezaji huo.
Ikiwasilisha taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, TPDC imesema miradi inayotekelezwa kwa mfumo wa CSR inaendelea kusaidia jamii katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya, michezo na ardhi.
Ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o umegharimu Sh1.27 bilioni, ambapo TPDC imechangia huku Shell na Equinor zikichangia kila moja.
Uwekezaji huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, huku manufaa yake yakitarajiwa kuendelea kuonekana kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, amesema wananchi wamekuwa wakisubiri utekelezaji wa mradi wa LNG kwa takribani miaka 15, wakitarajia uwekezaji huo ulete maendeleo katika mkoa huo.
Aidha, upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji na barabara ni miongoni mwa mambo yatakayochochea uwekezaji na kuifanya Lindi kuwa eneo lenye mvuto zaidi kwa shughuli za kiuchumi.
Wananchi waandaliwe kunufaika
Akieleza changamoto za jimbo lake, Mbunge wa Lindi Mjini, Mohamed Utaly amesema kukatika kwa umeme ni mojawapo ya matatizo yanayohitaji ufumbuzi, akiiomba Wizara ya Nishati kushirikiana na wadau kuboresha hali hiyo.
Pia, aliiomba wizara kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi wa LNG, ili waelewe utakaotekelezwa, fursa zitakazopatikana na namna wanavyoweza kunufaika.
“Gesi ya Likong’o inapaswa kuwa chanzo cha nishati, ajira na maendeleo kwa familia za Lindi na jamii kwa ujumla,” amesema.
Naye, Meya wa Manispaa ya Lindi, Twahili Mpuruji, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuipatia shule hiyo mradi wa nishati safi ya kupikia ili kuboresha huduma za chakula shuleni na kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira.
Kwa upande wake, Dk Homera alisema mafuta na gesi nchini yanapatikana kwa kiwango cha kutosha, akisisitiza dhamira ya Serikali kuhakikisha uwekezaji katika sekta hiyo unachangia maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo, pamoja na matarajio makubwa yaliyowekwa kwa mradi wa LNG, wananchi wa Lindi bado wanasubiri kukamilika kwa mazungumzo na taratibu za kisheria zitakazowezesha kuanza kwa utekelezaji wake rasmi.
You may also like

Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha

Waziri Ulega awataka watendaji kutumia madaraka kwa uadilifu


Leave a Reply