

11 kortini kwa tuhuma za kutakatisha Sh1.4 bilioni
Dar es Salaam. Watu 11 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 13 ya uhujumu uchumi, yakiwemo kuongoza genge la uhalifu, kuingilia mifumo ya kibenki na kutakatisha fedha zinazozidi Sh1.4 bilioni.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa, Oktoba 23, 2026, na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Mbiling’i aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Godfrey Mbuva, Tahaa Farouq, James Bonga, Alex Ng’owe, Waji Ramadhani, Johnson Shoo, Sirili Massawe, Zephania Monge, Aisha Bakar, Richard Mbogo na Abdulrazak Mzava.
Kabla ya kusomewa mashtaka, Hakimu Mushi aliwaeleza washtakiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi bila kibali husika. Pia aliwaeleza kuwa shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana, hivyo baada ya kusomewa mashtaka wangepelekwa mahabusu.
Baadhi ya washtakiwa 11 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuingilia mifumo ya kubeki na kutakatisha fedha zaidi ya Sh1.4bilioni, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Baada ya maelekezo hayo, hakimu aliruhusu upande wa mashtaka kuendelea kuwasomea washtakiwa mashtaka yao.
Wakili Mbiling’i alidai kuwa kati ya Machi na Juni 6, 2026, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa kuingilia mifumo ya kibenki.
Alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ya kuingilia mifumo ya benki za Access na Akiba Commercial Bank Plc, katika matukio yanayodaiwa kutokea katika tarehe tofauti mwaka huu.
Katika shtaka jingine, upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa wote isipokuwa Mbogo, kati ya Machi 1 na Aprili 30, 2026, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliingilia mfumo wa benki ya Access na kujipatia kwa njia ya udanganyifu Sh224 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.
Pia, ilidaiwa kuwa washtakiwa wote isipokuwa Massawe, kati ya Mei 25 na Juni 6, 2026, waliingilia mfumo wa Akiba Commercial Bank Plc na kujipatia kwa njia ya udanganyifu Sh1.4 bilioni kutoka akaunti ya benki hiyo.
Baadhi ya washtakiwa 11 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuingilia mifumo ya kubeki na kutakatisha fedha zaidi ya Sh1.4bilioni, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa Mbuva, Farouq, Bonga, Mbogo na Mzava, kati ya Machi 1 na Aprili 30, 2026, walitakatisha Sh224 milioni huku wakijua kuwa fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la kuingilia mfumo wa kibenki na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Washtakiwa hao pia wanadaiwa kutakatisha Sh1.4 bilioni kati ya Mei 25 na Juni 30, 2026, wakijua kuwa fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa udanganyifu baada ya kuingilia mfumo wa kibenki.
Katika mashtaka mengine, Aisha anadaiwa kutakatisha Sh32 milioni kati ya Juni 1 na Julai 27, 2026.
Baadhi ya washtakiwa 11 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuingilia mifumo ya kubeki na kutakatisha fedha zaidi ya Sh1.4bilioni, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Mzava naye anadaiwa kutakatisha Sh60 milioni kwa kununua gari aina ya Land Rover. Aidha, Juni 16, 2026, anadaiwa kuficha uhalisia wa umiliki wa gari hilo kwa kubadili umiliki na kuliandikisha kwa jina la mama yake, Bibiana Cherumbe.
Vilevile, Farouq anadaiwa kutakatisha Sh25 milioni Mei 26, 2026, kwa kununua gari aina ya Toyota Crown kwa nia ya kuficha uhalisia wa fedha hizo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa Jamhuri ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 3, 2026, kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
You may also like

Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha

Waziri Ulega awataka watendaji kutumia madaraka kwa uadilifu


Leave a Reply