
Maingilio 106 yalivyopunguza foleni barabara kuu Mbeya
Mbeya. Kero ya msongamano wa magari katika Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) imeanza kupungua baada ya kufunguliwa kwa maingilio 106 ya barabara za pembezoni, huku kazi ya kumwaga lami ikianza katika mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne Nsalaga hadi Songwe.
Mradi huo wenye urefu wa kilomita 29 unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ukiwa na thamani ya Sh138.7 bilioni.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumatatu, Novemba 2, 2026, baadhi ya madereva wamesema kufunguliwa kwa njia hizo kumepunguza muda wa safari na usumbufu waliokuwa wakikabiliana nao.
Dereva Bajani, Hashim Issa amesema maelekezo ya Serikali kwa Tanroads kufungua njia za pembezoni katika maeneo yenye msongamano mkubwa yamekuwa msaada kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Amesema awali foleni ilikuwa kubwa na kusababisha baadhi ya magari kukwama kwa muda mrefu, hali iliyoongeza hatari ya ajali, hasa malori yaliyokuwa yakipata hitilafu za breki.
Amesema kasi ya sasa ya utekelezaji wa mradi inatoa matumaini ya kupungua zaidi kwa changamoto hizo.
Kwa upande wake, dereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Soko Matola, Kabwe na Uyole, Emily Emily, amesema kufunguliwa kwa njia za pembezoni na kuanza kumwagwa lami ni hatua muhimu katika kuboresha usafiri jijini Mbeya.
“Kwanza tunapongeza usimamizi wa Tanroads kwa sababu tunaona wanavyomsimamia mkandarasi. Kazi zinafanyika usiku na mchana, lakini pia kufunguliwa kwa maeneo 106 kumesaidia kupunguza foleni kwa kiwango kikubwa tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Seleman Bishanga, akieleza maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne Nsalaga–Songwe na hatua ya kumwaga lami katika urefu wa kilometa 1.3 jijini Mbeya.
Akizungumzia hali hiyo, mfanyabiashara wa bidhaa za majumbani, Salome Aloyce, amesema awali safari yake kutoka Soko Matola hadi Igawilo kununua bidhaa zilikuwa zikichukua saa kadhaa kutokana na foleni.
Amesema kwa sasa ameanza kuona tofauti baada ya kufunguliwa kwa njia za pembezoni, akieleza kuwa anaweza kwenda na kurudi kwa muda mfupi zaidi.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Seleman Bishanga, amesema kasi ya sasa imetokana na maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara yake mkoani humo Oktoba 16 na 17, 2026.
Amesema maelekezo hayo yalitolewa baada ya kubainika kuwa mradi ulikuwa unasuasua, huku mojawapo ya hatua zilizotakiwa kuchukuliwa ikiwa ni kufungua maingilio ya barabara za pembezoni katika maeneo yenye msongamano.
“Mpaka sasa maingilio 106 yamefunguliwa na kuanza kutumika. Pia, alielekeza kuongeza kasi ya mradi, ambao awali baadhi ya maeneo yalikuwa hayajawekewa lami, lakini sasa tayari tumemwaga lami umbali wa kilometa 1.3 katika awamu ya kwanza,” amesema Bishanga.
Amesema baada ya maelekezo hayo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads pamoja na Wizara ya Ujenzi waliendelea kutoa maelekezo kwa mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha ujenzi unafanyika usiku na mchana.
Amesema katika eneo la Mbeya Mjini, bado kuna kilometa tatu zinazopaswa kukamilishwa, huku kazi mbalimbali za ujenzi zikiendelea.
Bishanga amesema Makamu wa Rais amekuwa akifuatilia maendeleo ya mradi na kupata taarifa za kila siku kuhusu hatua zinazofikiwa.
“Nimhakikishie Makamu wa Rais kazi zinafanyika usiku na mchana kuhakikisha kipande cha kilomita tatu kilichopo Mbeya Mjini kinakamilika. Tunaendelea na hatua mbalimbali za ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa Watanzania,” amesema.
Mradi huo ulisainiwa Februari 14, 2023, ukiwa na thamani ya Sh138.7 bilioni na ulitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24. Unatekelezwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co Ltd (CHICO), chini ya usimamizi wa TANROADS.
You may also like

Tanzania: What Two Global Outages Mean for Tz’s Digital Finance

Ushahidi mtoto wa miaka mitatu wamfunga maisha

Leave a Reply