

Chadema yaweka masharti kushiriki maridhiano
Dar es Salaam. Hatima ya ushiriki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mchakato wa maridhiano ya kitaifa sasa inaonekana kutegemea masharti mawili ambayo chama hicho kimesema ni lazima yatimizwe kabla ya kuingia katika mazungumzo.
Chama hicho kimetaka Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, aachiwe huru bila masharti, kesi zinazowakabili viongozi na wanachama wake zifutwe na kupatikana kwa msuluhishi wa kimataifa atakayekubalika na pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa nchini.
Kwa mtazamo wa Chadema, Lissu ndiye kiongozi anayebeba matumaini ya chama hicho na anapaswa kuwa sehemu ya mchakato huo, badala ya mazungumzo kufanyika akiwa gerezani.
Msimamo huo umetolewa leo Jumanne, Novemba 24, 2026, na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuunda Tume ya Maridhiano itakayoratibu maandalizi ya mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Heche amesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko na wasiwasi mwenendo wa maandalizi ya mchakato huo, akieleza maridhiano ya kweli hayawezi kufikiwa kwa kuhusisha vyama ambavyo havijawahi kuwa katika mgogoro na Serikali, huku chama kinachohusika moja kwa moja na mgogoro huo kikiachwa nje.
Amesema Chadema haiwezi kukubali kushiriki mazungumzo wakati viongozi na wanachama wake wakiendelea kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ambayo chama hicho kinayapinga.
“Ili tuweze kushiriki mazungumzo ya aina yoyote, Mwenyekiti wetu Tundu Lissu lazima awe nje, zaidi ya hapo hakuna na mtu asijidanganye popote kwamba Chadema inaweza kushiriki maridhiano na viongozi wengine wanaoshikiliwa waachiwe,” amesema.
Kwa mujibu wa Heche, hali hiyo inakinzana na dhana ya maridhiano, kwa kuwa Serikali haiwezi kutoa mwaliko wa mazungumzo kwa upande mmoja huku ikiendelea kuchukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wa upande mwingine.
Ametaja pia madai ya utekaji, vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu ni miongoni mwa masuala yanayopaswa kushughulikiwa katika mchakato huo.
“Maridhiano ya kweli hayawezi kuwa mazungumzo ya jumla, mikutano ya kupiga picha, kauli za kisiasa wala hotuba za kuonyesha jumuiya ya kimataifa kwamba kuna mchakato unaendelea,” amesema.
Amesisitiza mazungumzo hayo yanapaswa kuhusisha pande zinazokinzana, akieleza mgogoro wa kisiasa uliopo nchini unahusisha Chadema na CCM, pamoja na wananchi na Serikali inayoongozwa na chama hicho.
Katika kufafanua sharti la kwanza, Heche amesema Lissu anapaswa kuachiwa huru na kushiriki moja kwa moja katika mazungumzo hayo, akisisitiza chama hakiwezi kukubali kiongozi wake mkuu kubaki gerezani huku mazungumzo yanayohusu hatima yake yakiendelea.
“Hakuna mazungumzo ya aina yoyote ambayo chama hiki kitafanya huku mwenyekiti wetu akiwa gerezani. Mazungumzo yatakayofanyika lazima yaongozwe na mwenyekiti wetu mwenyewe,” amesema.
Ili kusisitiza msimamo huo, Heche ametumia mifano ya mapambano dhidi ya utawala wa makaburu nchini Afrika Kusini na harakati za ukombozi nchini Zimbabwe, akieleza kuwa mazungumzo ya kisiasa katika mataifa hayo yalihusisha viongozi wakuu wa harakati hizo baada ya kuachiwa huru.
Ametoa mfano wa Afrika Kusini, ambako mazungumzo ya kumaliza mfumo wa ubaguzi wa rangi yalifanyika baada ya Nelson Mandela kuachiwa huru, akisisitiza kuwa ni vigumu kufanya mazungumzo yenye tija huku kiongozi mkuu wa upande mmoja akiwa kizuizini.
Sharti la pili, kwa mujibu wa Heche, ni kupatikana kwa msuluhishi wa kimataifa ambaye atakuwa na imani ya pande zote zinazohusika katika mgogoro huo.
Amesema Chadema haiwezi kushiriki mazungumzo yatakayoongozwa na upande mmoja wa mgogoro huo, akieleza kuwa msuluhishi anapaswa kuwa mtu au taasisi isiyohusika moja kwa moja na mgogoro unaotakiwa kutatuliwa.
“You cannot be a judge of your own cause,” amesema, akimaanisha mtu hawezi kuwa mwamuzi wa mgogoro ambao yeye mwenyewe ni sehemu yake.
Heche amedai CCM na Serikali yake ni miongoni mwa pande zinazohusika katika mgogoro huo, kutokana na kile alichokitaja kuwa ni vitendo vya ukandamizaji, utekaji, mauaji na kufungwa kwa viongozi wa Chadema.
Amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha mchakato wa maridhiano unashughulikia chanzo cha mgogoro wa kisiasa nchini, badala ya kuishia katika mazungumzo yasiyogusa kiini cha tofauti zilizopo.
“Mgogoro huu unahitaji kutatuliwa mara moja na Watanzania wapate Katiba,” amesema.
Katika hatua nyingine, Heche amewataka wanachama wa Chadema kutokuwa na wasiwasi kuhusu hali ya Lissu, akisema mwenyekiti huyo yuko imara licha ya kuendelea kuzuiliwa gerezani na kukosa nafasi ya kushiriki mazishi ya kaka yake.
Amesema chama hicho kitaendelea kufuatilia mwenendo wa kesi zinazomkabili Lissu, akidai zimekuwa na dosari nyingi ambazo Chadema itazieleza kwa wakati mwafaka. Akirejea kiini cha tofauti zilizopo kati ya chama hicho na Serikali, Heche amesema Chadema kinataka nchi iwe na Katiba mpya itakayowezesha mageuzi ya kisiasa, hususan katika mfumo wa uchaguzi, akidai Serikali imekuwa ikipuuza hitaji hilo.
Kwa msingi huo, amesema ni kujidanganya kuamini kuwa mchakato wa maridhiano unaweza kufanikiwa bila Chadema kushirikishwa, akitolea mfano wa Zanzibar mwaka 2001, ambako mazungumzo yalihusisha pande zilizokuwa katika mgogoro wa kisiasa.



Leave a Reply