

Watu wawili wafariki ajali ya treni Njombe
Njombe. Watu wawili wamefariki dunia baada ya kuruka kutoka ndani ya treni ya mizigo iliyopata ajali katika eneo la Utiga, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, wakati wakijaribu kujiokoa.
Ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo, Novemba 5, 2026, ilisababisha mabehewa 14 yaliyobeba shaba kuanguka, huku mengine tisa yakibaki salama.
Treni hiyo iliyokuwa ikitoka Zambia kuelekea Dar es Salaam, ilikuwa imebeba shehena ya mizigo wakati ajali hiyo ilipotokea.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Zakaria Mwansasu, amesema watu wengine wanne waliokuwa ndani ya behewa lililopata ajali wamenusurika na kupatiwa matibabu, huku hali zao zikiendelea vizuri.
Mwansasu ameliagiza Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) kufanya jitihada za haraka kurekebisha miundombinu ya reli iliyoharibika ili kuwezesha huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria kurejea katika hali ya kawaida.
“Niwashukuru sana askari wetu wa Wilaya ya Wanging’ombe kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Wamekuwepo katika eneo hili tangu walipopata taarifa za ajali,” amesema Mwansasu.
Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Zakaria Mwansasu wa pili kulia akizungumza katika eneo ambalo ajali hiyo imetokea.
Aidha, amewaonya wananchi wa Wanging’ombe na wale wanaotoka nje ya wilaya hiyo dhidi ya kutumia ajali hiyo kama fursa ya kuiba mali zinazohusika na tukio hilo.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kudhibiti vitendo hivyo na kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na wizi atachukuliwa hatua za kisheria.
You may also like


Sababu noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa mapema

Leave a Reply