

Kamati ya Bunge yataka wanaopita daraja la Tanzanite kuanza kulipia
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu, imeshauri ni wakati sasa daraja la Tanzanite watu waanze kupita kwa kulilipia.
Ushauri huo umetolewa leo Jumamosi Novemba 7,2026 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso, walipofanya ziara ya kutembelea miradi ya daraja la Jangwani, Tanzanite na Mradi wa Mabasi Yendayo Haraka awamu ya nne.
Daraja hilo lenye Kilomita 1.03 likiwa na njia nne za magari linaunganisha eneo la Hospitali ya Aga Khan (Upanga) na barabara za Obama, Kenyatta na Toure (kuelekea Osterbay na Masaki) jijini Dar es Salaam.
Katika ujenzi wake takribani Sh243 bilioni, fedha zilizofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia kampuni ya ujenzi ya GS E&C na lilizinduliwa rasmi Machi 2022.
Lengo kuu la ujenzi wake ilikuwa ni kupunguza msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi na eneo la daraja la zamani la Selander
Akilizungumzia daraja hilo, Kakoso amesema kuna haja ya Serikali sasa kuweka tozo kwa sababu wengi wanaotumia kupita hapo ni watu wenye nafasi zao.
“Utozaji huo wa hela, mapato yake yataweza kusaidia kujenga madaraja katika maeno mengine ya nchi na hivyo Serikali kuacha kutegemea tu bajeti yake katika kujenga madaraja,”amesema Kakoso.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Sheria ineweka wazi kwamba eneo ambalo kuna daraja na miundombinu mingine mbadala ya kuweza kutumiwa tozo hizo zinaweza kuanzishwa.
“Hivyo kwa pale licha ya kuwepo kwa daraja hilo la Tanzanite pia lipo lile la Salenda ambalo kwa wale wasio na uwezo wa kupita kwa kulipia, watalitumia hilo,”amesema.
Katika hili, amesema pia wataendelea kuishauri Serikali na ile barabara ya kutoka Dar es Salaam, kuelekea Kibaha hadi Chalinze kushirikishwa sekta binafsi ili kuwa pia na barabara za kulipia.
“Duniani kote, Barabara zinajengwa kwa kushirikishwa sekta binafsi, pia madaraja ambapo zikikamilika zinalipiwa na ndio ujenzi wa kisasa.
Kuhusu daraja la Jangwani, Mwenyekiti huyo amesema wameridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wak huku akishauri Serikali kumsimamia ipasavyo mkandarasi ili kuweza kumaliza kwa wakati.
Pia, katika mradi huo, ameshauri utakapokamilika kuhakikisha wanaacha kitu ambacho kitakua ni kumbukumbu kwa wakazi wa maeneo hayo ikiwemo kuwajengea shule au kituo cha afya.
Amesema katika daraja hilo zaidi Sh90 bilioni zimetolewa na Serikali kwa ufadhili wa benki ya dunia ambapo baadhi ya wananchi walipisha mradi.
“Hivyo ni vema kujenga hata kituo cha afya au shule kwa wananchi ambao wametoa ushirikiano na hii inapaswa kufanywa kwa nchi nzima ambako miradi mbalimbali mikubwa inatekelezwa,” amesema Kakoso.
Kwa upande wa mradi wa BRT, Mwenyekiti huyo amesema wana mashaka nao kwani unaenda kwa kusuasua ukizingatia kwamba hadi sasa ulikuwa uwe umekamilika na kuitaka serikali kuhakikisha wanasimamia mkandarasi ili aweze kumaliza kwa wakati..
Pia, amesema kama mkandarasi kakiuka masharti waliongia naye mkataba katika muda wa kuumaliza ni vema akatozwa faini kama ambavyo Serikali imekuwa ikilipia fidia pale inapochelewesha malipo kwa wakabdarasi.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa moja ya sababu zilizotajwa ni kuchelewa kwa kwa uondoshwaji wa miundombinu ya nguzo za umeme na mabomba ya maji, ameishari Serikali kuhakikisha kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi ya aina hiyo miundombinu hiyo iwe inaondolewa kwa wakati ili kuepusha kazi kuchelewa kuanza.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema mradi wa BRT awamu ya nne unatekelezwa kwa sehemu mbili(yaani LOT 1 na LOT 2) ambapo wakandarasi wake ni wawili tofauti na ilikuwa ikamilike ndani ya mwaka huu 2026, lakini sasa utakamilika Januari mwakani.
Amesema katika hilo LOT 2 inayohusisha kipande kutoka Mwenge hadi Tegeta ndio imechelewa sababu kubwa ikiwa ni hiyo uondoshaji wa miundombinu.
Kasekenya amesema LOT 1 ujenzi wake umefika asilimia 70 huku LOT 2 ujenzi wake ukiwa asilimia 40.
Hata hivyo, amesema katika maelekezo yao kwa mkandarasi, tayari wamewaambia waongeze muda wa kufanya kazi (usiku na mchana) na kuongeza wataalam ili kuweza kumaliza kwa wakati.
Aidha Waziri huyo, amesema wamepokea ushauri wa Kamati katika kuwasimamia wakandarasi kuweza kumaliza kwa wakati.
Kuhusu suala la ulipaji wa daraja la Tanzanite amesema kwa kuwa kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, hivyo wao kama Serikali imelipokea na kilichobaki ni kulifanyia kazi ya namna ya kulitekeleza.
Katika hatua nyingine Kasekela amegusia mpango wa kupunguza foleni Dar es Salaam ambapo amesema watajenga Barabara ya njia sita itakayotoka bandarini kupitia Kisarawe na kwenda kutokea Chalinze mpango ambao amesema wanatamani uanze hata mwakani.
‘Kwa hiyo itakuwa ni barabara ya mzunguko wan je ya Dar es Salaam, ambapo magari mengi yanayotoka Dar es Salama kwenda Bara hayatalazimika kupita tena mjini na hivyo kupunguza foleni,” amesema Waziri Kasekenya.
You may also like

Sababu noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa mapema

Zungu: Uwekezaji siyo kuuza nchi


Leave a Reply