

Zungu: Uwekezaji siyo kuuza nchi
Unguja. Mlezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu amesema uwekezaji nchini sio kuuza nchi kama wanavyodhani baadhi ya watu, bali ni kuingia ubia wa kimkakati ili kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya ndani.
Zungu ameyasema hayo leo Novemba 7, 2026 wakati wa ziara na kikao cha tathmini mkoani humo, ambapo alitoa mwelekeo kuhusu fursa za uwekezaji, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, pamoja na nidhamu ndani ya chama.
“Wawekezaji katika sekta za bandari, kilimo, viwanja vya ndege, utalii na mahoteli wanasaidia sana kuzalisha nafasi za kazi kwa vijana,” amesema Zungu.
Pia, amebainisha kuwa uwekezaji huo unawezesha Serikali kuongeza mapato ya ndani, ambayo kisha yanaelekezwa kwenye huduma za kijamii zisizowavutia wawekezaji moja kwa moja.
Kama vile miradi ya maji safi, elimu bora, makazi bora, mishahara mizuri na kuwahudumia wazee.
Zungu amewasilisha maelekezo kutoka Kamati Kuu ya CCM yanayotaka kufanyika kwa tathmini ya kina ya uhai wa chama na mapenzi ya wananchi.
Ameeleza kuwa tathmini hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma msingi kama vile maji na barabara zilizojengwa chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Hata hivyo, amekemea vikali suala la wanachama kutolipa ada za chama ambazo ni Sh100 pekee kwa mwezi.
Amebainisha kuwa kati ya wanachama 106,169 wa CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ni wanachama 6,000 pekee waliolipa ada zao kuanzia Januari hadi Septemba, na kuwataka wanachama kuacha tabia ya kukimbilia kulipa ada wakati wa uchaguzi pekee.
“Hili tunapaswa kulisisitiza, ada ya wanachama ndio msingi wa chama, hapa naona kuna ulegevu kidogo, tunatakiwa kulisimamia,” amesema.
Kuhusu nidhamu na umoja ndani ya chama, Zungu amepiga marufuku makundi ya mbio za urais wa mwaka 2030 kabla ya wakati, akisisitiza kuwa Kamati Kuu na mapenzi ya Mungu ndivyo vitakavyoamua uongozi.
Pia, amewataka wanachama na viongozi kuacha tabia ya kukibeza chama pale wanapokosa au kuondolewa kwenye nafasi za uongozi.
“Tunajua kuna makundi, kwa sasa tunatakiwa kuwa wamoja badala ya kutengeneza makundi ndani ya chama,” amesema.
Pia, amewaagiza wabunge na wawakilishi kushuka chini kukaa na wananchi kwenye baraza na vikundi, kunywa nao kahawa na kukagua miradi.
Ametumia fursa hiyo kuwataka kupiga picha na kutangaza mafanikio ya miradi mikubwa kama flyover, barabara, huduma za afya ya mama na mtoto, na usambazaji wa maji na umeme ili wananchi waone kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ali Ame, amethibitisha kuwa kuna ushirikiano mkubwa na wa kindugu kati ya Chama na Serikali katika mkoa huo.
Amesisitiza kuwa CCM imepata ushindi wa kishindo mkoani humo kwa kushinda wadi zote, pamoja na nafasi zote za masheha.
Kuhusu maombi ya vyama vya upinzani katika serikali ya kitaifa vinavyotaka kupewa nafasi za usheha, wakuu wa wilaya wakuu wa mkoa na wakurugenzi, Ame ameeleza kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa inaendelea kujadiliana nao.
“Lakini msimamo wa mkoa ni kwamba walioshinda ndio wanaopaswa kushika dola, huku wakisubiri miongozo zaidi kutoka Kamati Kuu,” amesema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chaani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, amempongeza Zungu kwa umahiri na ueledi wake katika kuongoza Bunge na vikao vya chama.
“Halmashauri Kuu ya Mkoa imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na mlezi huyo na tunaahidi kuyatekeleza kikamilifu, ikiwemo kuimarisha ulipaji wa ada na kutatua kero za wananchi,” amesema.
Pia, ametangaza mafanikio ya mkoa kwa kuwasajili wanachama wapya 8,000 wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kupitia kadi zenye thamani ya zaidi ya Sh2milioni akisisitiza kuwa viongozi wote watahakikisha kila utekelezaji unagusa maslahi binafsi ya mwananchi mmoja mmoja.
You may also like


Sababu noti za Sh1,000 na Sh2,000 kuchakaa mapema


Leave a Reply