

Kamati ya Bunge yashauri TADB kuwafikia wakulima wadogo
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeishauri Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuongeza juhudi za kuwafikia wakulima wadogo kupitia mikopo inayolenga mahitaji yao, huku ikiitaka benki hiyo kutafuta vyanzo mbadala vya mitaji badala ya kutegemea fedha za Serikali pekee.
Kamati hiyo, pia, imeitaka TADB kuelekeza uwekezaji wake katika maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya wakulima, yakiwamo umwagiliaji, uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao, ili kuimarisha mchango wa benki hiyo katika maendeleo ya sekta ya kilimo.
Ushauri huo ulitolewa Novemba 6, 2026, wakati wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea makao makuu ya TADB na kupokea taarifa kuhusu utendaji, mafanikio na changamoto za benki hiyo tangu ilipoanzishwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Akizungumza baada ya kupokea wasilisho la TADB, Mwenyekiti wa PIC, ambaye pia ni Mbunge wa Kivule, Ojambi Massaburi amesema benki hiyo inapaswa kuoanisha mipango yake ya ukuaji na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kutafuta vyanzo mbalimbali vya mitaji.
Amesema ingawa azma ya benki hiyo kupata angalau Sh800 bilioni kutoka serikalini ni muhimu, inapaswa pia kuimarisha mikakati ya kupata fedha kutoka vyanzo vingine.
“Nimeona mnataka angalau Sh800 bilioni kutoka serikalini, ni sawa, lakini naomba mpangilio wa mipango yenu ulingane na Dira 2050 inayotutaka kutafuta vyanzo vingine vya mapato,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Ojambi Massaburi akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Awali, akiwasilisha taarifa ya benki hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TADB, David Nghambi, amesema mtaji wa wanahisa wa benki hiyo umeongezeka kutoka Sh76.7 bilioni mwaka 2020 hadi Sh553.22 bilioni kufikia Septemba 2026.
Amesema katika juhudi za kukusanya mitaji, benki hiyo imefanikiwa kupata Sh1.41 trilioni hadi Septemba 2026, huku ikitarajia kupata Sh759 bilioni zaidi katika kipindi cha mwaka 2025 hadi 2027.
Aidha, amesema mapato ya benki yameongezeka zaidi ya mara tatu, kutoka Sh28.1 bilioni hadi Sh106.4 bilioni, huku gharama za uendeshaji zikiongezeka kutoka Sh12.8 bilioni hadi Sh51.2 bilioni katika kipindi hicho.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilionyesha kuwa zaidi ya nusu ya mikopo iliyotolewa na benki hiyo imeelekezwa katika ununuzi wa mazao, ikifuatiwa na uwekezaji katika viwanda vya uchakataji, pembejeo za kilimo, maghala, hifadhi baridi na maeneo mengine ya mnyororo wa thamani wa kilimo.
Mgawanyo huo wa mikopo uliibua mjadala miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, ambao walitaka kufahamu kwa kiwango gani wakulima wadogo wananufaika na huduma za benki hiyo, ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa makundi muhimu yanayopaswa kunufaika na uwepo wake.
Mjumbe wa PIC na Mbunge wa Viti Maalumu wa Singida, Martha Nehemia Gwau, amesema mafanikio ya TADB hayapaswi kupimwa kwa kuongezeka kwa mitaji na mapato pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea kilimo.
Amesema benki hiyo inaonekana kuelekeza nguvu nyingi katika ufadhili wa ununuzi wa mazao, badala ya kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji zinazowanufaisha wakulima wadogo moja kwa moja.
“Focus yenu ipo sana kwenye ununuzi wa mazao, badala ya kwenye mnyororo wa thamani unaowalenga wakulima wadogo,” amesema.
Ameshauri benki hiyo kuongeza mikopo kwa shughuli kama umwagiliaji na uwekezaji mwingine unaoweza kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima wadogo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Magu na mjumbe wa kamati hiyo, Boniventura Kiswaga, ameipongeza TADB kwa hatua iliyopiga tangu ilipoanzishwa mwaka 2015, akibainisha kuwa wakati huo benki hiyo ilikuwa na mtaji wa Sh60 bilioni pekee.
Amessema benki hiyo imeonyesha maendeleo makubwa ikilinganishwa na kipindi cha mwanzo, ambapo kulikuwa na mijadala kuhusu uwezekano wa kuifuta au kuiunganisha na taasisi nyingine za kifedha.
“Kwa sasa inaendelea vizuri. Pale mwanzo tulikuwa tunajadili kuifuta au kuiunganisha benki hii na nyingine,” amesema.
Naye, Mbunge wa Mlalo, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Rashid Shangazi amesema Serikali inapaswa kuendelea kuongeza fedha katika TADB, lakini benki hiyo inapaswa pia kuelekeza mikopo katika mazao ya kimkakati yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, uchakataji na thamani ya bidhaa za kilimo.
Ametolea mfano zao la michikichi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, hususan mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, akisema uwekezaji katika zao hilo unaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Ametaja pia korosho, mkonge na pamba kuwa miongoni mwa mazao yanayohitaji uwekezaji zaidi, akisisitiza umuhimu wa kuchagua mazao yenye mchango mkubwa kiuchumi na uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wakati wajumbe wa kamati hiyo wakisisitiza umuhimu wa kuongeza ufadhili kwa wakulima wadogo na mazao ya kimkakati, TADB imetaja mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa dhamana za mikopo na uhaba wa mitaji kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri shughuli zake za utoaji mikopo.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TADB, Ishmael Kasekwa, amesema benki itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kuandaa taarifa inayoeleza mikakati yake ya kuongeza mitaji na kupanua wigo wa kuwafikia wakulima wadogo.
Amesema bodi itajadili masuala hayo na kuwasilisha mpango kamili kwa kamati ili kuonyesha hatua ambazo benki imejipanga kuchukua katika kukabiliana na changamoto zilizoibuliwa.
“Tutajadili na kutuma taarifa kamili ya mpango huu kwa kamati,” amesema Kasekwa.




Leave a Reply