

Kamati ya Bunge yataka udhibiti michezo ya kubahatisha, kulinda fursa kwa jamii
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) imetaka udhibiti imara wa michezo ya kubahatisha ili fursa za ajira, mapato na maendeleo zinazozalishwa na sekta hiyo zinanufaisha wananchi bila kuwaingiza kwenye uraibu, hasara na matatizo ya kiuchumi.
Wito huo umetolewa leo, Novemba 7, 2026, na viongozi wa kamati walipotembelea ofisi za Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Dar es Salaam, kujifunza mchango na usimamizi wa sekta hiyo.
Akizungumza katika kikao na mamlaka za GBT Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ojambi Masaburi, ambaye pia ni Mbunge wa Kivule, amesema pamoja na kufurahishwa na ajira na mapato yanayotokana na michezo ya kubahatisha, ni muhimu kuangalia uwiano kati ya wanaonufaika na wanaopata hasara ili wananchi wasifilisike.
“Nimefarijika kuona mnavyozalisha ajira, lakini angalieni watu wanafanikiwa na kuliwa kwa kiasi gani, maana lengo ni kufanya watu wapate fursa siyo wafirisike. Pia, udhibiti kwa vijana wasiingie uraibu wa kubeti kupitiliza,” amesema.
Masaburi amesema udhibiti unapaswa pia kulinda uadilifu wa mashindano kudhibiti upangaji matokeo.
“Kwa uzoefu wangu upangaji matokeo ni kweli. Nimecheza mpira wa miguu na mwisho nilikuwa nikicheza African Lion, binafsi nimebeti mara kadhaa na kuhusu kupanga matokeo ni dhahiri mimi nimeshuhudia,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa PIC, Elibariki Kingu, ambaye pia ni Mbunge wa Ikungi Magharibi, amesema mchango wa sekta hiyo kwenye huduma za jamii unaonesha inaweza kuwa sehemu ya maendeleo, iwapo mapato yatasimamiwa na kuelekezwa kwenye vipaumbele vya wananchi.
“Mimi binafsi mmenipa sababu ya kwenda kuwasemea Bungeni kwa kugusa eneo muhimu la mfuko wa afya. Tulipopitisha Mpango wa bima kwa wote tulifanya ambalo ni ajenda ya Rais wetu na Chama chetu, kwa kuchangia kwenye mfuko huu, GBT mnafanya jambo muhimu sana,” amesema.
Akieleza mafanikio ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT), Mwenyekiti wake Balozi Modest Mero, amesema mwaka wa fedha uliopita sekta hiyo ilikusanya Sh307 bilioni kutoka kampuni zilizosajiriwa 64.
“Kupitia Michezo ya kubahatisha nchini zaidi ya Watanzania 30,000 wamepata ajira mpaka sasa,” amesema.
Amesema michezo ya kubahatisha mtandaoni nayo ina fursa, lakini ukuaji wake unahitaji udhibiti wa waendeshaji na mitaji yao ili kuongeza mapato na kudhibiti uraibu.
“Katika kudhibiti uendeshaji, Bodi hukagua rekodi za uhalifu, uwezekano wa utakatishaji fedha, uwezo wa kifedha, chanzo cha fedha, washirika wa biashara na vifaa vya waombaji leseni. Bodi pia hushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Polisi kupambana na uendeshaji usio halali,” amesema.
Amefafanua kuwa GBT inazuia watoto na watu wasiostahili kushiriki, kwa kuwa michezo hiyo inaweza kusababisha uraibu na upotevu wa fedha.
Mero amesema bodi inafanya kazi kuhakikisha kampuni zinafuata masharti ya leseni na viwango vilivyowekwa, huku ikifuatilia mwenendo wa soko.
Amesema usimamizi huo ni muhimu ili ukuaji wa biashara usipunguze usalama wa washiriki na imani ya wananchi.
“Kwaupande wa maslahi ya umma, asilimia tano ya mapato ya michezo ya kubahatisha imeidhinishwa kusaidia sekta ya michezo nchini na asilimia saba imeidhinishwa kusaidia mfuko wa afya kwa kuwezesha mpango wa bima ya afya kwa wote,” amesema.
Ili kuleta manufaa zaidi, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida (CCM) ambaye ni Mjumbe wa kamati hiyo, Martha Gwau, amesema mapato ya sekta hiyo yanahitaji uwekezaji wa ndani na kuwawezesha Watanzania kuingia kwenye biashara hiyo.
“Sisi tumesha cheza sana michezo ya kubahatisha na tumeshaliwa na kula sana. Licha ya changamoto zake, kwa faida inazozalisha sekta hii ni muhimu na lazima tuiwezeshe ifanye kazi kama inavyofanya kazi kwenye nchi za wenzetu,” amesema.
“Ili kufikia mafanikio hayo, lazima wazawa wawezeshwe kuingia humo ili tujue zaidi yabayifanyuka humo,” amesema, akiunga mkono pendekezo la kubakiza asilimia moja ya mapato ya Bodi hiyo ili kuiwezesha bodi kutekeleza majukumu yake.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dk Jasson Rweikiza, akisema hakufahamu ukubwa wa fursa za sekta hiyo na kutaka iungwe mkono na Serikali.
“Sikufahamu kama Sekta hii inafursa namna hii. Mchango wake kwenye mfuko wa afya na mapambano dhidi ya Ukimwi ni jambo muhimu sana,” amesema.
Upangaji matokeo udhibiwe
Kwa upande wake, Mbunge wa Mwera, Zanzibar, Suleiman Mohamed Rashid, ameonya kuwa kuongeza mapato hakupaswi kuathiri soka, ambako washiriki wanaweza kuwa na maslahi kwenye michezo ya kubahatisha.
“Tusije kujikuta tunaendesha michezo hii kwa kuangalia mapato tu huku inaua mpira wetu. Ukifuatilia watu wanaobeti wengi wanaohusika moja kwa moja na michezo hali inayoweza kusababisha upangaji matokeo,” ameonya.
Maoni hayo yanafanana na msisitizo wa Mnyekiti wa Kamati hiyo, aliyedokeza kuhusu uzoefu wake kwenye soka na kutaka Udhibiti imara wa washiriki wa michezo hiyo.
Kwa hoja za Wabunge na uongozi wa Bodi hiyo, ziara ya PIC imeweka mkazi katika kuimarisha usimamizi na kuwawezesha Watanzania kunufaika, ili michezo hiyo iwe chanzo cha maendeleo badala ya mzigo kwa wananchi zaidi.
You may also like

Sh2.04 trilioni zilivyogusa kilimo,elimu,afya na ajira



Leave a Reply