

Sh2.04 trilioni zilivyogusa kilimo,elimu,afya na ajira
Dar es Salaam. Changamoto ya kupata mtaji wa kukuza biashara, kukosa fedha za kuendeleza kilimo na ukosefu wa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ni miongoni mwa vikwazo vinavyokabili wananchi katika kujikwamua kiuchumi, hali inayoweka umuhimu wa uwekezaji unaounganisha huduma za kifedha na mahitaji halisi ya jamii.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Equity Group Holdings imeripoti kuwekeza dola za Marekani milioni 771 (takribani Sh2.04 trilioni) katika maendeleo endelevu na ustawi wa jamii mwaka 2025, fedha zilizolenga maeneo ya biashara, kilimo, elimu, afya na uhifadhi wa mazingira katika nchi inazofanyia shughuli zake.
Matokeo ya uwekezaji huo yanaonesha kuwa wajasiriamali 962,924 wamepatiwa mafunzo ya biashara, wakulima wadogo na wa kati 622,525 wamefikiwa kupitia ufadhili na mafunzo, huku wanawake na vijana zaidi ya milioni 2.49 wakinufaika na elimu ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Group, Dk James Mwangi amesema mafanikio ya kibiashara yanaimarisha uwezo wa taasisi kuwekeza katika maendeleo ya jamii.
“Kadiri biashara yetu inavyoimarika ndivyo uwezo wetu wa kuwekeza kwa watu, biashara na jamii unavyoongezeka, sambamba na kujenga ustahimilivu katika masoko tunayohudumia,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Prosper Nambaya amesema maendeleo endelevu yanapaswa kupimwa kwa uwezo wake wa kubadilisha maisha ya wananchi.
Amesema kwa Tanzania maendeleo endelevu yanapaswa kupimwa kwa uwezo wake wa kubadilisha maisha ya wananchi kwani wanapowezesha biashara kupata mitaji, wakulima kuimarisha uzalishaji na wanawake pamoja na vijana kupata fursa za kiuchumi, tunachangia kujenga uchumi jumuishi na wenye ustahimilivu.
“Kutokana na umuhimu huo tunaendelea kuweka msisitizo katika suluhisho za kifedha zinazochochea uzalishaji, ajira na ukuaji wa biashara,” amesema Nambaya.
Katika eneo la biashara, Equity Group imetoa mikopo yenye thamani ya dola 3.11 bilioni za Marekani (takribani Sh8.22 trilioni) kwa biashara ndogo na za kati katika masoko yake huku kupitia Equity Group Foundation, wajasiriamali wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuimarisha uwezo wao wa kusimamia biashara.
Kwa wanawake na vijana, elimu ya fedha inaweza kuwasaidia kuelewa matumizi ya huduma za kifedha, kupanga matumizi na kufanya maamuzi kuhusu mitaji na shughuli zao za kiuchumi.
Katika kilimo, wakulima 622,525 wamefikiwa kupitia ufadhili, mafunzo na programu za kuimarisha minyororo ya thamani kutokana na umuhimu kwa wakulima wadogo ambao wanahitaji huduma za kifedha na maarifa ili kuimarisha uzalishaji na kushiriki katika masoko.
Uwekezaji huo pia umehusisha elimu na ajira, ambapo wanufaika 60,009 wamepatiwa ufadhili wa masomo na vijana 9,772 wamepata mafunzo ya vitendo yenye malipo.
“Kwa vijana wanaotafuta fursa za ajira, mafunzo ya aina hiyo yanaweza kuwasaidia kujenga ujuzi na uzoefu unaohitajika katika mazingira ya kazi. Katika mazingira, zaidi ya Sh529 bilioni zimeelekezwa katika ufadhili endelevu na miradi inayohusiana na tabianchi, huku bidhaa 75,855 za nishati safi zikisambazwa na miti milioni 9.1 ikipandwa mwaka 2025,” amesema.
Akizungumzia kuhusu uwezeshaji wa mitaji, Leokadia Marwa amesema miongoni mwa vitu vinavyowakwamisha wajasiriamali wengi wadogo ni kukosa uhakika wa kukuza mitaji yao.
“Unaweza kuwa na ndoto kubwa lakini mtaji ukakuangusha, benki pia huwa na masharti mengi lakini inapotokea unaweza kupata fedha ili kukuza shughuli zako inakuwa ni ahueni katika kufikia soko kubwa zaidi unalohitaji,” amesema.



Leave a Reply