

Waziri Shemdoe aruhusu bajaji kurejea barabara kuu Mbeya
Mbeya. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, ameondoa zuio la bajaji kuondolewa katika Barabara Kuu ya Tanzam jijini Mbeya, huku akielekeza kuundwa kwa timu itakayopanga maeneo na ruti za vyombo hivyo ndani ya siku 14.
Pia, ameelekeza kusitishwa kwa usajili mpya wa bajaji, akisema idadi iliyopo ya takribani 6,000 inatosha kwa sasa wakati Serikali ikiendelea kupanga utaratibu wa usafiri jijini humo.
Maelekezo mengine ni kuchunguza malalamiko dhidi ya uongozi wa madereva bajaji, kuandaa kanzi data ya machinga na bajaji, pamoja na kuwapa kipaumbele wafanyabiashara waliokuwa na vibanda katika eneo la Old Airport kwenye soko jipya litakalojengwa.
Akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, baada ya kutembelea eneo la Old Airport, ambako soko la Machinga Complex linajengwa, Shemdoe amesema upangaji wa bajaji na machinga ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema changamoto iliyojitokeza ni kutokuwapo kwa mazungumzo na makubaliano ya pamoja kati ya Serikali na makundi yaliyoathiriwa na mpango huo kabla ya kuanza kutekelezwa.
Bajaji zikiendelea na kazi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa upande wa machinga, wenye vibanda ambavyo havitumiki hapa Old Airport waandikwe majina. Baadaye jengo likikamilika wapewe kipaumbele, kwa kuwa linajengwa Machinga Complex,” amesema.
Kuhusu bajaji, Shemdoe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, kuunda timu itakayojumuisha wawakilishi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), halmashauri, madereva bodaboda, bajaji, daladala na machinga.
Amesema timu hiyo itakuwa na jukumu la kutathmini mazingira ya usafiri na biashara, kubaini maeneo yatakayotumiwa na bajaji na daladala, pamoja na kupanga ruti zinazofaa ndani ya siku 14.
“Kwa upangaji wa bajaji, kazi iliyokuwa imefanyika ilikuwa nzuri, isipokuwa ilipata mushkili kidogo kwa kuwa hatukuwashirikisha. Mkuu wa Mkoa, unda timu ambayo ndani ya siku 14 itazunguka kuangalia bajaji zitakaa wapi, daladala zitapita wapi na ruti,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho cha wiki mbili, Latra itaendelea kupanga bajaji chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, huku ruti mpya zikitarajiwa kubainisha maeneo yatakayotumiwa na kundi hilo.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuandaa kanzi data ya bajaji na machinga ili kuondoa sintofahamu wakati wa kuwahamishia katika maeneo yatakayopangwa.
Akizungumzia hali ya barabara, Shemdoe ameuagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoani humo, kurekebisha maeneo korofi ili kurahisisha shughuli za usafiri.
Amekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni kwamba machinga wa Old Airport wanatakiwa kuondolewa, akisema si ya kweli na kuwataka wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, akizungumza wakati wa ziara yake jijini Mbeya kufuatia sintofahamu iliyoibuka ya Bajaji kuondolewa barabara kuu jijini humo.
“Kuna barabara ambazo zinapaswa kurekebishwa. Meneja Tarura Mkoa na Wilaya, hakikisheni mnapitisha gereda ili kuruhusu shughuli ziendelee, lakini ile barua ya mtandaoni ni feki. Nyie endeleeni kufanya biashara zenu,” amesema.
Kuhusu uongozi wa bajaji, Shemdoe amesema Serikali imepokea malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha na mali za chama hicho.
Amemtaka Sagini kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza madai hayo, huku akielekeza kuangaliwa kwa uwezekano wa kusimamisha uongozi uliopo na kuweka wa muda wakati uchunguzi ukiendelea.
“Nendeni na vyombo vyako, wakiwamo Takukuru, mkachunguze matumizi ya fedha. Ikibainika kuwapo kwa ubadhilifu, hatua zichukuliwe, lakini wakati huohuo uongozi angalia namna ya kuusimamisha kwanza, utafutwe wa muda kwa kuwa watakuwa wanachunguzwa,” amesema.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amesema hali imetulia baada ya taharuki iliyojitokeza, akiahidi kuwa maelekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Sagini amesema atatekeleza maelekezo hayo, akieleza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha Mbeya inakuwa na amani, utulivu na mazingira yanayowezesha wananchi kujipatia kipato.
Amesema atawasiliana na Tanroads kuhusu uwezekano wa kutenga njia za bajaji ili kuepusha migogoro na magari makubwa, huku timu ya kupanga ruti ikitarajiwa kuanza kazi kesho.
“Nia yangu ni kuona Mbeya yenye amani na utulivu. Tutawasiliana na Tanroads ili kuweka uwezekano wa njia za bajaji badala ya kupambana na lori. Suala la kuunda timu litafanyika kuanzia kesho mapema ili kubaini maeneo na ruti za magari. Wafanyabiashara hatuwezi kuwapeleka pabaya,” amesema.
Naye Jane Raphael, machinga wa soko la Old Airport, amesema maelekezo ya Waziri na Mkuu wa Mkoa yamewarejeshea matumaini ya kuendelea na shughuli zao za kujipatia riziki.
Oktoba 12, RC Sagini alielekeza bajaji kuondolewa katika Barabara Kuu ya Tanzam kwa lengo la kupanga matumizi ya barabara, kuimarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine.
Utekelezaji ulianza Oktoba 20, jambo ambalo ambalo halikuwaridhisha baadhi ya madereva wa bajaji na kususia kutoa huduma hivyo, kusababisha changamoto ya usafiri kwa wananchi.
You may also like

Wapiga kura wa Netanyahu waanza kumgeuka

Kapinga ataka mikopo izalishe viwanda, ajira


Leave a Reply