

Kapinga ataka mikopo izalishe viwanda, ajira
Kahama. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameitaka Serikali na wadau wa maendeleo ya viwanda nchini kuelekeza nguvu katika kuwawezesha wajasiriamali wenye uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa, kuanzisha viwanda na kutengeneza ajira.
Amesema tathmini ya uwezeshaji wa mitaji haipaswi kuishia katika idadi ya watu wanaopata mikopo, bali pia kuangalia uwezo wa miradi kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha uzalishaji na kutoa ajira kwa watu wengine.
Kapinga ameyasema hayo Jumamosi, Oktoba 24, 2026, wakati akifungua maonyesho ya tano ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Magufuli, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Amesisitiza kuwa mikopo kwa wajasiriamali inapaswa kuleta matokeo yanayopimika katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya tano kitaifa ya shirika la maendeleo ya viwanda vidogo (SIDO) yanayoendelea wilayani Kahama. Picha na Amina Mbwambo
“Msisubiri ajira iwafuate, bali anzeni na mlicho nacho, anzisheni biashara na tengenezeni ajira, tumieni fursa zilizopo kujiletea maendeleo,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mikopo yenye thamani ya Sh14.372 bilioni ilitolewa kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali, huku wanawake wakinufaika kwa asilimia 52 ya mikopo hiyo na kuzalisha ajira 384,482.
Akizungumzia maonyesho hayo, Kapinga amesema yanapaswa kuwa daraja la kudumu kati ya wazalishaji na wanunuzi, badala ya kuwa jukwaa la kuonyesha bidhaa kwa siku chache pekee.
Pia amewahimiza wajasiriamali kutumia teknolojia za kidijitali kutangaza bidhaa zao na kuwafikia wateja wengi zaidi.
Kapinga amezitaka taasisi na kampuni kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini, akieleza kuwa soko la ndani ni msingi wa kuimarisha uzalishaji na kujenga uwezo wa bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akipokea zawadi ya kofia kutoka kwenye banda la wajasiriamali kutoka nchini Burundi waliohudhuria maonyesho ya tano kitaifa ya shirika la kukuza viwanda vidogo (SIDO), yanayoendelea wilayani Kahama. Picha na Amina Mbwambo
Kuhusu kongani za viwanda, Kapinga amesema haridhishwi na kasi ya utekelezaji wa mpango wa kuanzisha kongani za viwanda katika wilaya nchini.
Amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia Sido, kuharakisha maandalizi ya mpango huo na kuwasilisha mkakati mpya ndani ya miezi mitatu.
“Kongani ni agizo la Mheshimiwa Rais, na Sido tulikubaliana vizuri katika eneo la kongani, hususan za wilaya. Sifurahishwi na kasi yenu. Naomba nikutake, Katibu Mkuu, mjitafakari upya ndani ya miezi mitatu, mkakati uje upya, liweze kupatikana jambo la kongani kwenye wilaya,” amesema.
Amesema maeneo hayo yanahitaji miundombinu wezeshi, ikiwemo maji, umeme, teknolojia na mifumo bora ya usafirishaji, ili kuimarisha shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika uzinduzi wa maonesho ya tano kitaifa ya shirika la kukuza viwanda vidogo (SIDO), yanayoendelea katika viwanja vya Magufuli, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo
Shinyanga yaongeza viwanda
Awali, akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dk Fransis Mlacha, amesema idadi ya viwanda mkoani humo imeongezeka kutoka 1,457 Juni 2021 hadi 1,840 Juni 2025, sawa na ongezeko la viwanda 383.
Dk Mlacha amesema ongezeko hilo linaonyesha juhudi za kuimarisha sekta ya uzalishaji, ambayo ina mchango muhimu katika kukuza uchumi, kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua fursa za ajira kwa wananchi.
Amesema mkoa huo umeendelea kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji yenye ukubwa wa takribani hekta 5,477 katika halmashauri zake, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Miongoni mwa maeneo aliyoyataja ni Buzwagi Special Economic Zone, lenye ukubwa wa ekari 1,333, pamoja na maeneo ya Nyashimbi na Chapula katika Manispaa ya Kahama.
“Ongezeko hili limechangia kuongezeka kwa viwanda vya kati, vidogo sana na viwanda vikubwa sana. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi, Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuhamasisha uwekezaji ndani ya mkoa,” amesema.
Sido yazalisha viwanda vipya 1,760
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Sido, Ahmed Kitara, amesema shirika hilo linaendelea kusaidia wajasiriamali kwa kuwapatia teknolojia, mafunzo na ushauri wa kitaalamu unaolenga kuboresha uzalishaji na kuimarisha biashara zao.
Amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2025/2026, Sido imesaidia kuanzishwa kwa viwanda vipya 1,760 vilivyozalisha ajira 60,700. Katika kipindi hicho, wajasiriamali 51,000 walipatiwa mafunzo, huku wengine 71,000 wakipata ushauri wa kitaalamu kuhusu biashara.
“Tunajua kwamba tukiwa na teknolojia, uzalishaji utaimarika, lakini uzalishaji pekee bila soko hatuwezi kusonga mbele. Hivyo, Sido kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, hutoa mafunzo ya uchakataji bidhaa, uzalishaji na teknolojia pamoja na uratibu na utengenezaji wa viwanda,” amesema Kitara.
Amesema maonyesho hayo yana malengo mawili makuu, ambayo ni kueneza teknolojia na kupanua masoko, akisisitiza kuwa uzalishaji pekee hautoshi bila kuwepo kwa masoko ya uhakika ya bidhaa zinazozalishwa.
Ameongeza kuwa kupitia maonyesho hayo, wajasiriamali wanapata fursa ya kutangaza bidhaa zao, kujifunza teknolojia mpya, kuboresha ubora na kuongeza thamani ya bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kitara amesema matarajio ya Sido ni kuona maonesho hayo yakichangia kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira, kukuza kipato cha wananchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Maonyesho ya tano ya Sido kitaifa, yaliyoanza Oktoba 21, 2026, katika Viwanja vya Magufuli, wilayani Kahama, yanatarajiwa kumalizika Oktoba 30, 2026. Maonyesho hayo yanawakutanisha wajasiriamali, wazalishaji, wanunuzi na wadau wa maendeleo ya viwanda kwa lengo la kukuza biashara na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.
You may also like

Malaria kwa wajawazito yashuka Tanzania, sababu zatajwa

Wapiga kura wa Netanyahu waanza kumgeuka


Leave a Reply