

Malaria kwa wajawazito yashuka Tanzania, sababu zatajwa
Dar es Salaam. Idadi ya wajawazito wanaobainika kuwa na malaria wanapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza imepungua kutoka asilimia 7.7 mwaka 2020 hadi asilimia 3.9 mwaka 2025, huku matumizi ya dawa kinga, vyandarua vyenye viuatilifu na huduma za mapema yakitajwa kuchangia mafanikio hayo.
Ripoti ya Mapitio ya Mkakati wa Kitaifa wa Mpango wa Malaria wa mwaka 2021–2025 iliyotolewa na Wizara ya Afya inaonesha kuwa, kiwango cha upimaji wa malaria kwa wajawazito kiliongezeka kutoka asilimia 96 mwaka 2020 hadi asilimia 97 mwaka 2025.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, ongezeko la upimaji linaonesha kuimarika kwa uzingatiaji wa miongozo kwa watoa huduma za afya, inayowataka kuwapima wajawazito malaria wanapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza.
Akizungumzia na Mwananchi hivi karibuni, sababu za kupungua kwa wajawazito wanaobainika kuwa na malaria, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi na Matibabu ya Malaria wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), Dk Abdallah Lusasi amesema matumizi ya dawa kinga ya SP ni miongoni mwa sababu kuu.
Amesema kuwahi kliniki kunawawezesha wajawazito kupata elimu kuhusu kujikinga na malaria, kupatiwa vyandarua vyenye viuatilifu na kuanza kutumia dawa kinga mapema.
“Wajawazito wanapowahi kliniki mapema sana, inatoa fursa ya kuzungumzia changamoto ya maambukizi kwa jumla. Pia, tunawapatia vyandarua vyenye viuatilifu mapema. Vyandarua hivi huwasaidia na dawa kinga tunazotoa za SP ni bure nchi nzima,” amesema.
Dk Lusasi amesema matumizi ya dawa kinga kwa wakati yanaweza kupunguza hatari ya mjamzito kupata malaria, hivyo kuongeza nafasi ya kujifungua mtoto mwenye afya njema.
Amesema afua nyingine inayotekelezwa na Serikali ni kunyunyizia dawa za kuua mazalia ya mbu katika jamii, hatua inayosaidia kupunguza maambukizi.
Aidha, amesema wajawazito wanapopata dalili za malaria wanahimizwa kuwahi hospitalini kwa ajili ya kupimwa na kupata matibabu mapema, jambo linaloonyesha matokeo chanya katika udhibiti wa ugonjwa huo.
Madhara ya malaria kwa wajawazito
Mtaalamu wa afya, Dk Ernest Winchislaus amesema malaria wakati wa ujauzito inaweza kusababisha kuzaliwa watoto wenye uzito pungufu, vifo vya watoto wachanga na matatizo mengine ya kiafya.
“Ili kuzuia malaria, wajawazito lazima wapewe tiba kinga ya vipindi dhidi ya malaria, angalau dozi tatu za dawa ya SP (Fansidar) katika mahudhurio yao ya kliniki,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo ya kiafya yaliyonukuliwa katika Jarida la The Lancet, malaria wakati wa ujauzito inaweza kusababisha upungufu wa damu, kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini na hata kifo kwa mama.
Jarida hilo linaeleza kuwa, kwa upande wa ujauzito, maambukizi yanayosababishwa na vimelea vya Plasmodium falciparum na Plasmodium vivax yanaweza kuongeza hatari ya ujauzito kuharibika, mtoto kufia tumboni, kujifungua kabla ya wakati na mtoto kutokua vizuri tumboni.
Linaeleza kuwa, mtoto anayekabiliwa na maambukizi ya malaria akiwa tumboni anaweza pia kuwa katika hatari ya kudumaa kwa ukuaji na kupata madhara katika mfumo wa fahamu wakati wa utoto.
Kwa mujibu wa maelezo ya jarida hilo, ingawa idadi ya mimba zilizo katika hatari ya maambukizi ya P. falciparum na P. vivax ilipungua kwa asilimia 17.2 Kusini Mashariki mwa Asia na asilimia 52.6 katika eneo la Pasifiki Magharibi tangu mwaka 2000, malaria bado ni tishio kwa wajawazito katika maeneo mbalimbali duniani.
Linaeleza kuwa, mwaka 2020, mimba milioni 56.8 zilikuwa katika hatari ya maambukizi ya P. falciparum, huku mimba milioni 65.5 zikiwa katika hatari ya P. vivax katika nchi 20 zilizofanyiwa mapitio.
Matumizi ya kinga yaongezeka
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS 2022) unaonesha kuongezeka kwa matumizi ya kinga dhidi ya malaria miongoni mwa wajawazito.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wajawazito waliopata dozi tatu au zaidi za dawa kinga dhidi ya malaria wakati wa ujauzito (IPTp) waliongezeka kutoka asilimia tatu mwaka 2004–2005 hadi asilimia 32 mwaka 2022.
Hata hivyo, utafiti huo ulionesha kuwa asilimia 58 ya wajawazito walilala chini ya chandarua chenye dawa ya kuua mbu usiku uliotangulia siku ya utafiti.
Utafiti huo ulihusisha wanawake 15,254 wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kutoka kaya 15,705 zilizochaguliwa. Pia, wanaume 5,763 wenye umri huo kutoka nusu ya kaya zilizochaguliwa walifanyiwa mahojiano.
Mikoa yenye viwango vya juu
Ripoti ya Mapitio ya Mkakati wa Kitaifa wa Mpango wa Malaria wa mwaka 2021–2025 inaonesha kuwa Katavi ilikuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu zaidi cha wajawazito waliobainika kuwa na malaria.
Mikoa mingine iliyotajwa kuwa na viwango vya juu ni Mara, Geita, Mtwara, Kigoma na Kagera.
Kwa upande mwingine, Arusha, Kilimanjaro na Manyara iliripoti viwango vya chini zaidi vya malaria miongoni mwa wajawazito, hali inayoonesha tofauti za maambukizi kati ya maeneo nchini.
Malaria bado ni changamoto
Katika hotuba yake kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema maambukizi ya mfumo wa hewa yaliongoza kwa asilimia 36.8 yaliyowaathiri zaidi wagonjwa wa nje walio chini ya miaka mitano.
Magonjwa mengine yaliyotajwa ni kuharisha kwa asilimia 8.2, malaria kwa asilimia 7.2 na maambukizi ya njia ya mkojo kwa asilimia 6.2.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, pamoja na hatua zinazochukuliwa kudhibiti malaria, kuimarisha kinga, upimaji wa mapema na upatikanaji wa matibabu bado ni muhimu katika kupunguza madhara ya ugonjwa huo, hususan kwa wajawazito na watoto.
You may also like

Wapiga kura wa Netanyahu waanza kumgeuka

Kapinga ataka mikopo izalishe viwanda, ajira


Leave a Reply