

Watuhumiwa wawili wa mauaji, uporaji wauawa Arusha
Arusha. Watuhumiwa wawili waliokuwa wakitafutwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu, yakiwamo mauaji na uporaji wa pikipiki, wamefariki dunia wakati wakipatiwa matibabu kutokana na majeraha waliyopata katika mapambano na polisi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, tukio hilo lilitokea jana Oktoba 21, saa 3:30 usiku, eneo la Kijenge jijini Arusha.
Taarifa hiyo imewataja watuhumiwa hao ni Yusuph Hamis, maarufu Yuzo na Dickson Livingstone, anayefahamika kama Ndessa, ambao walijeruhiwa wakati wakikabiliana na polisi.
“Walijeruhiwa na askari wakati walipokuwa wanajihami kwa silaha kuzuia kukamatwa, katika eneo ambalo walikuwa wamejipanga kutekeleza tukio lingine la uhalifu,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imedai kuwa watuhumiwa hao walikutwa na silaha walizokuwa wakitumia kujihami ili wasikamatwe, zikiwemo bastola na panga.
Pia, walikutwa na pikipiki moja mpya isiyokuwa na namba za usajili, hali inayodaiwa kuwa ililenga kuficha utambulisho wake ili isijulikane kwa urahisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Yusuph alikuwa akituhumiwa kuongoza genge la uhalifu lililohusishwa na matukio mbalimbali, yakiwemo mauaji ya madereva wa bodaboda na uporaji wa pikipiki zao.
Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya Erasto Losujaki, dereva bodaboda aliyeuawa Aprili 28, 2026, katika Kitongoji cha Olkaria, Kata ya Mateves, wilayani Arumeru, ambapo pikipiki yake pia iliporwa.
Taarifa hiyo imetaja tukio lingine kuwa ni mauaji ya Adiel Thomas, dereva bodaboda mkazi wa Ngaramtoni, ambaye inadaiwa aliporwa pikipiki yake kabla ya kuuawa Septemba 15, 2026, katika Kijiji cha Likamba, Kata ya Musa, wilayani Arumeru.
“Uchunguzi wa tukio hili unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia watuhumiwa wengine waliokuwa wakishirikiana nao na kufuatilia mali nyingine walizopora, zikiwemo pikipiki,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza watuhumiwa hao waliwahi kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba na kuiba.
Imeelezwa walitumikia vifungo mbalimbali, huku Dickson akitajwa kuwa alikuwa bado anaendelea kutumikia kifungo cha nje.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo pamoja na kuwafuatilia watu wengine wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo wa uhalifu na kurejesha mali zinazodaiwa kuporwa.




Leave a Reply