

Wakulima 400,000 Nyanda za Juu Kusini kunufaika na biashara ya hewa ukaa
Njombe. Takriban wakulima 400,000 kutoka Nyanda za Juu Kusini wanatarajia kunufaika na mradi wa biashara ya hewa ukaa, kufuatia makubaliano ya kibiashara kati ya Serikali na Kampuni ya Kaderes, inayoshirikiana na Uholanzi.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma, ukiwa na lengo la kuwawezesha wakulima kuongeza kipato kupitia shughuli zinazochangia kupunguza hewa ukaa na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka wakati wa utiaji saini makubaliano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda amesema mradi huo ni fursa muhimu kwa wakulima kuongeza kipato na kuboresha maisha kupitia biashara ya hewa ukaa.
Amewataka wadau wote watakaohusika na utekelezaji wa mradi huo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi, huku akisisitiza umuhimu wa uwazi katika mikataba itakayosainiwa ili kuondoa malalamiko kwa wanufaika.
“Kupitia mradi huu, mkulima atavuna parachichi, lakini pia atapata fedha kupitia hewa ukaa huku akitunza mazingira, kipato kitapaa kwa wananchi na niombe uwapo wa uzingatiaji sheria, kanuni na taratibu za nchi,” amesema Sweda.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa hewa ukaa wakifuatilia mada zilizokuwa zikiendelea huko mkoani Njombe
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga amesema Serikali iko tayari kuupokea mradi huo, akieleza kuwa unatarajiwa kuwa na tija kiuchumi na kuingiza fedha kwa wanufaika.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa wananchi.
“Niwahakikishie kwamba sisi tupo tayari, kama watumishi, mtu mmoja mmoja na sekta binafsi, kufanya jambo hili na kuvuna fedha nyingi,” amesema Mfanga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kaderes, Leonard Kachebonaho amesema mradi huo utawapa wakulima fursa ya kushiriki katika biashara ya hewa ukaa na kunufaika kiuchumi kutokana na juhudi zao za kuhifadhi mazingira.
Amesema mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 20, huku mazungumzo yakiendelea na washirika wao wa Uholanzi kuhusu uwezekano wa kuongeza muda huo.
“Mradi huu ni wa miaka 20 kwa kuanzia, tunaendelea na mazungumzo na wenzetu wa Uholanzi kuona kama tunaweza kurefusha zaidi, tunatarajia kuona fursa kubwa kwa wananchi hasa upande wa uchumi,” amesema Kachebonaho.
Mwenyekiti wa Redcross Mkoa wa Njombe, Edger Mtitu amesema mradi huo utasaidia kuongeza kipato cha wananchi na kupunguza matukio ya moto misituni ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
“Nishauri mradi huu uambatane na teknolojia za kusaidia kukabiliana na majanga ya moto ili kuimarisha uhifadhi wa misitu na kuongeza manufaa kwa wananchi.
“Mradi kama huu ungeweza kuja na teknolojia ya kusaidia kupambana na majanga ya moto ili tuweze kunufaika,” amesema Mtitu.
You may also like

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola

Tanzania mwenyeji mkutano waa maadili ya biashara Afrika

Leave a Reply