

Nkasi kuweka mfumo wa kielektroniki kudhibiti utoro wa watumishi
Rukwa. Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mohamed Mtulyakwaku, ameagiza ofisi zote za umma wilayani humo kuweka mifumo ya kielektroniki ya kusajili mahudhurio ya watumishi wanapoingia na kutoka kazini, akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kutohudhuria kazi bila sababu za msingi.
Mtulyakwaku ametoa agizo hilo wakati wa kikao kazi na watumishi wa umma wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, akisisitiza kuwa nidhamu na uwajibikaji ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema mifumo hiyo inapaswa kuwekwa katika kila ofisi, kuanzia ngazi ya kata, ili kufuatilia mahudhurio ya watumishi na kudhibiti utoro kazini.
Aidha, amewaagiza maofisa elimu kata kudhibiti mara moja taasisi zinazotoa mikopo ya kausha damu kwa walimu, akionya kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya maafisa watakaobainika kuruhusu taasisi hizo kuwakopesha walimu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Oktoba 26, 2026, Mtulyakwaku amesema mikopo hiyo imekuwa janga kwa walimu wengi wilayani humo kutokana na riba kubwa wanazotozwa na athari zake kwa maisha yao na utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema uchunguzi unaonyesha baadhi ya walimu wamekopa katika taasisi zaidi ya tatu kwa wakati mmoja, huku wakitozwa riba inayozidi asilimia 30 kwa mwezi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka walimu kujiepusha na mikopo hiyo na badala yake kutumia huduma za taasisi za kifedha zinazotambulika kisheria na zinazotoa mikopo yenye riba nafuu.
Mwalimu mmoja wa shule ya msingi katika Kata ya Kirando, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia aibu, amesema maisha yake yamekuwa magumu baada ya kuingia katika mtego wa mikopo hiyo.
“Nilianza kwa kukopa Sh200,000 kwa ajili ya matibabu ya mtoto. Riba ikawa kubwa, nikakopa sehemu nyingine kulipa ile ya kwanza. Sasa nakatwa Sh700,000 kila mwezi, nimeshindwa kulipa ada ya watoto wangu, nyumba yangu imefilisika na nashindwa hata kwenda darasani vizuri kwa mawazo,” amesema mwalimu huyo.
Walimu wengine wamesema madeni hayo yameathiri uwezo wao wa kuhudumia familia, huku baadhi yao wakikabiliwa na msongo wa mawazo.
Pia, wapo wanaodaiwa kukosa utulivu wa kufundisha kutokana na mawakala wa taasisi hizo kufika shuleni kuwadai, hali ambayo baadhi ya walimu wamesema inawadhalilisha mbele ya wanafunzi.
Wazazi wilayani humo wamelalamikia utoro na kutokuwepo kwa walimu darasani, wakisema hali hiyo inaathiri masomo na ufaulu wa watoto wao.
Akizungumzia hatua za kukabiliana na tatizo hilo, Mtulyakwaku amesema maofisa elimu kata wana wajibu wa kusimamia ustawi wa walimu katika maeneo yao na kuhakikisha taasisi hizo haziendelei kuwaingiza katika mikopo yenye masharti yanayowatesa.
Amesisitiza kuwa maofisa watakaobainika kuruhusu mawakala wa mikopo hiyo kuingia shuleni na kuwashawishi walimu kukopa watakabiliwa na hatua za kinidhamu.
Ameongeza kuwa watumishi wote wa umma wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, akionya kuwa kutokuwepo kazini bila sababu za msingi hakutavumiliwa.
You may also like

Moshi: Walalamikia uhaba wa maji, wanunua ndoo Sh1,000

Sh1.27 bilioni kujenga shule, LNG kuipa Lindi sura mpya


Leave a Reply