

Moshi: Walalamikia uhaba wa maji, wanunua ndoo Sh1,000
Moshi. Baadhi ya wananchi wa kata za Longuo B, Msaranga na Ng’ambo, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kukosekana kwa maji safi na salama kwa siku kadhaa hali inayowalazimu kununua ndoo moja kwa Sh500 hadi Sh1,000 ili kukidhi mahitaji ya kila siku.
Wananchi hao wamesema kukosekana kwa huduma hiyo kwa muda mrefu kumewaathiri katika shughuli za nyumbani, ikiwemo kupika, kuoga na kutumia vyoo vya ndani vinavyohitaji maji, huku baadhi yao wakilazimika kuamka usiku wa manane kutafuta huduma hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika maeneo hayo leo, Oktoba 26, 2026 umebaini baadhi ya kaya kukosa maji, huku wakazi wa Longuo B wakisema wamekuwa na changamoto hiyo kwa takribani wiki tatu, wakati baadhi ya wakazi wa Msaranga wakieleza kukosa huduma hiyo kwa siku kadhaa mfululizo.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Longuo B, Marry Mbowe, amesema hali hiyo imekuwa ikiathiri hata kipato chake kwa kuwa sehemu ya fedha anazopata kupitia biashara yake huitumia kununua maji.
“Changamoto tunayopata hapa ni maji, yanasumbua sana. Tuna muda mrefu maji hayatoki, wakati mwingine tunanunua maji kwa Sh500 kwa ndoo, na kwa siku naweza kununua ndoo tatu au nne.
Amesema “Mabomba hayatoi maji, kwa hiyo tunapata shida, tunaomba Serikali ituletee maji, maana kila mwaka kipindi kama hiki maji yanakuwa shida, na kwa mfano, faida ninayopata kwenye biashara yangu ndiyo ninayotumia kununua maji.”
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Happy Joseph amesema hata maji yanapopatikana, hutoka kwa kiwango kidogo kisichokidhi mahitaji ya kaya.
Amesema kwa takribani mwezi mmoja wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo, hali inayowalazimu kununua maji au kutafuta maeneo mengine wanapohitaji huduma hiyo.
“Changamoto ya maji ni kubwa. Hata yakitoka, yanatoka tone kwa tone, wakati mwingine hata kuoga inakuwa shida kwa sababu hakuna maji, hki ndicho kitu kinachotusumbua sana,” amesema.
Kwa upande wake, Mercy Msaki, mkazi wa Msaranga, amesema wamekuwa wakiamka saa nane usiku kutafuta maji hadi saa 11 alfajiri, bila uhakika wa kuyapata.
“Tuna changamoto ya maji, ni wiki ya pili sasa hatuna maji. Tumekuwa tukiamka saa nane usiku kutafuta huduma hiyo hadi saa 11 alfajiri, na hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa mamlaka ya maji kuhusu changamoto iliyopo,” amesema.
Naye, Lucy Mmary, mkazi wa Msaranga, amesema ukosefu wa maji umekuwa ukisababisha familia kushindwa kutekeleza mahitaji muhimu, ikiwemo kupika na kutumia vyoo vya ndani.
“Tunakwenda kuomba maji kwa watu wenye visima, wakati mwingine tukikosa maji tunashindwa hata kupika chakula, kwa sababu ukipata ndoo mbili tu haitoshi kuhudumia familia,” amesema.
Mwananchi mwingine, Agatha Joseph, amesema hali huwa mbaya zaidi mwishoni mwa wiki, ambapo wananchi hulazimika kutembea na ndoo kutafuta maji katika maeneo mbalimbali.
“Maji ni shida sana, hasa Jumamosi na Jumapili. Watu wanatembea na ndoo barabarani kutafuta maji, lakini mamlaka hazisemi chochote mpaka sasa,”amesema
Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Longuo B, Benedict Mwashambwa, amesema eneo hilo limekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa takribani wiki tatu, licha ya miundombinu ya kusambaza huduma hiyo kuwepo.
Amesema amekuwa akiwasiliana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kutafuta suluhisho, lakini hadi sasa wananchi wameendelea kukabiliwa na adha hiyo.
“Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Muwsa, ambaye aliniambia kuwa wataalamu wako eneo la tukio kushughulikia tatizo. Nami nimewaeleza wananchi hali ilivyo, kwa sababu wamefikia hatua ya kununua maji kwa watu wenye visima kwa hadi Sh1,000 kwa ndoo ya lita 20,” amesema.
Mwashambwa amesema ukosefu wa maji unaweza kuongeza hatari ya kiafya kwa wanafunzi, hasa kwa kuzingatia kuwa kaya nyingi zina vyoo vya ndani vinavyohitaji maji, huku wanafunzi wa shule ya msingi katika eneo hilo wakilazimika kutembea umbali wa takribani mita 900 hadi kilomita moja kutafuta huduma hiyo.
Ameiomba Serikali kulichukulia suala hilo kuwa la dharura na kuhakikisha huduma inarejeshwa haraka ili kuondoa adha inayowakabili wananchi.
Diwani wa kata ya Longuo B, Benedict Mwashambwa akizungumzia changamoyo ya maji katika kata yake.
“Wananchi hawahitaji maneno mengi, wanahitaji huduma. Kukaa karibu mwezi mzima bila maji ni hatari kwa afya na maisha yao, tunaomba jambo hili lichukuliwe kwa uzito na hatua zichukuliwe haraka,” amesema.
Naye Diwani wa Kata ya Msaranga, Alhaji Ally Pendo (Dunga), amesema baadhi ya maeneo ya kata hiyo yamekosa maji kwa takribani siku nne, huku akieleza kuwa amefanya mawasiliano na mamlaka husika na kuambiwa kuwa tatizo linafanyiwa kazi.
Amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuhifadhi miti, kuepuka ukataji ovyo wa misitu na kufanya usafi katika maeneo yao, akieleza kuwa utunzaji wa mazingira ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Muwsa, Kija Limbe amesema tatizo hilo limesababishwa na kuziba kwa bomba na kwamba tayari changamoto hiyo imebainika na wataalamu wanaendelea kuishughulikia ili kurejesha huduma ya maji.
Amesema hatua zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha maji yanapatikana tena kwa wananchi walioathirika na tatizo hilo.
“Kuna changamoto ya bomba kuziba na imeshajulikana, naifanyia kazi na maji yatapatikana,”amesema Limbe
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations

Leave a Reply