

Tanzania mwenyeji mkutano waa maadili ya biashara Afrika
Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka 2026 wa Mtandao wa Maadili ya Biashara Afrika (BEN-Africa), utakaofanyika Novemba 5 na 6, 2026, katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), kujadili uongozi wenye maadili, utawala bora na uwajibikaji katika biashara.
Mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa Tanzania, BEN-Africa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu isemayo, “Mitazamo tofauti kuhusu maadili ya biashara: mtazamo kiafrika na zaidi ya hapo.”
Lengo ni kuchunguza mchango wa uongozi wenye maadili katika maendeleo endelevu, uwajibikaji wa kibiashara na ustawi wa muda mrefu wa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, Mkurugenzi wa Sheria na Udhibiti wa Absa Tanzania, Alistides Kashasira amesema maadili ni msingi wa kujenga taasisi endelevu, masoko yanayoaminika na jamii zenye ustawi.
“Maadili si suala la kutimiza tu matakwa ya uzingatiaji wa sheria na kanuni, bali ndiyo msingi unaojenga taasisi endelevu, masoko yanayoaminika na jamii zenye ustawi,” amesema Kashasira.
Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Absa Tanzania, Aron Luhanga amesema mkutano huo una maana zaidi ya udhamini, kwani unaakisi imani ya benki hiyo kuwa maadili na uaminifu ni nguzo za ukuaji endelevu.
Amesema mkutano huo pia utaipa Tanzania fursa ya kujitambulisha kama kitovu cha mijadala ya kitaalamu na mawazo bunifu kuhusu mustakabali wa biashara barani Afrika.
Programu itajumuisha hotuba kuu, mijadala ya majopo na majadiliano kuhusu mitazamo ya Kiafrika na Kimagharibi kuhusu maadili ya biashara, ukuaji endelevu wa uchumi na uongozi wenye maadili.
Mada nyingine ni ujasiriamali wenye maadili, falsafa ya Kiafrika ya Ubuntu na akili unde (AI), utalii, utawala bora na wajibu wa kampuni kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko na Kaimu Mkuu wa UDBS, Dk Robert Suphian amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kuandaa wahitimu wenye ujuzi na viongozi wenye maadili wanaoweza kukabiliana na changamoto za jamii.
Amesema chuo hicho kina heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuchangia juhudi za kuimarisha uongozi unaowajibika barani Afrika.
BEN-Africa, iliyoanzishwa mwaka 1999, huwakutanisha wasomi, viongozi wa biashara, watunga sera na asasi za kiraia kujadili changamoto za kimaadili.
Mkutano wa mwaka huu utakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, ukiwaleta pamoja viongozi wa Serikali, watendaji wa kampuni, wadhibiti, watafiti, wanafunzi na wataalamu wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
You may also like

DC avunja sherehe ya mahari ya mwanafunzi Bariadi

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola


Leave a Reply