

Ridhiwani ampa mzabuni siku tatu kuongeza kasi, huku akimpa tahadhari
Chalinze. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amempa siku tatu mzabuni anayejenga vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Kidogozero, Wilayani Chalinze, Mkoa wa Pwani, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akionya kuwa anaweza kuchukuliwa hatua ikiwamo kuondolewa.
Ridhiwani ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, alipokuwa anakagua miradi ya maendeleo katika sekta za afya na elimu katika Kata ya Vigwaza, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kasi ndogo ya ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni.
Mradi huo unaotekelezwa na mzabuni James Denis una miezi mitatu, lakini viongozi wa Kata ya Vigwaza wamesema maendeleo yake hayaridhishi.
Wamedai kuwa wamepoteza imani na mzabuni huyo kutokana na kasi ndogo ya kazi, ikiwamo kushindwa kukamilisha msingi licha ya zaidi ya miezi miwili kupita tangu kusaini mkataba.
Diwani wa Kata ya Vigwaza, Ramadhani Kirumbi amesema mzabuni huyo hafanyi kazi kwa uwajibikaji unaotarajiwa, badala yake anatekeleza majukumu kwa utaratibu wake bila kuzingatia matarajio ya wananchi.
Amesema hali hiyo imeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa mradi kukamilika kwa wakati, akieleza kuwa kasi ya kazi inayofanyika sasa haiendani na muda uliowekwa kwenye mkataba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Vigwaza, Athumani Kimui amesema mzabuni huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, akipendekeza mkataba wake uvunjwe kutokana na kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi.
Kutokana na malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Posi amemweleza mbunge changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi huo, hatua iliyomfanya amwite mzabuni na kumuuliza sababu za kazi kusuasua.
Hata hivyo, majibu ya mzabuni huyo hayakumridhisha Ridhiwani ambaye amesisitiza kuwa hataki kuona kazi ikiendelea kwa kasi ileile.
Ametoa siku tatu kuhakikisha kuna mabadiliko yanayoonekana katika utekelezaji wa mradi huo.
Mbunge huyo amesema atarejea katika eneo la mradi Jumamosi, Oktoba 24, 2026, mapema asubuhi kukagua maendeleo ya ujenzi na kuhakikisha maagizo yake yametekelezwa.
Amesisitiza kuwa anatarajia kukuta mabadiliko ya wazi, akionya kuwa hatua zitachukuliwa endapo mzabuni huyo atashindwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa.
Aidha, mbunge huyo alimwelekeza Denis kubaki katika eneo la mradi ili kusimamia kazi kwa karibu na kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kuulizwa kuhusu maelekezo hayo, Denis amesema ameyayapokea na atayafanyia kazi.
You may also like


Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha


Leave a Reply