

Ulemavu, ukata wakwamisha ndoto ya James kuendelea na elimu ya juu
Mbeya. Alipohitimu kidato cha sita, Mei mwaka huu, James Kilasi (22) aliamini kuwa amepiga hatua muhimu katika safari yake ya elimu, licha ya changamoto za kiafya zinazomkabili.
Hata hivyo, ndoto yake ya kuendelea na elimu ya juu sasa inakabiliwa na kikwazo cha ukosefu wa fedha za kukamilisha taratibu za kujiunga na chuo kikuu.
James, mkazi wa Mtaa wa Chemchem, Kata ya Igawilo jijini Mbeya, anasema amepata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha CUOM Mbeya kusomea Shahada ya Masoko na Uhusiano wa Umma (Marketing and Public Relations), lakini ameshindwa kukamilisha mahitaji ya kifedha yanayohitajika ili kuanza masomo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, James amesema anahitaji msaada wa fedha kwa ajili ya usajili, ada na mahitaji mengine ya chuoni. Anahofia kupoteza nafasi hiyo iwapo atashindwa kuripoti kwa wakati.
“Ndoto yangu ni kupata elimu ya juu ili niweze kujitegemea maishani. Nimejitahidi kusoma licha ya hali yangu ya afya, lakini sasa nimefika mahali ambapo uwezo wa kifedha wa familia yangu umekuwa kikwazo,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, anaiomba Serikali, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na wadau wa elimu na Watanzania wenye uwezo, kumsaidia kupata fedha za masomo ili asipoteze fursa aliyoipata.
Maisha ya kumtegemea mama kwa mahitaji ya msingi
Mbali na changamoto ya fedha za masomo, James anakabiliwa na changamoto ya kiafya inayomfanya ashindwe kutembea na kujihudumia mwenyewe, hivyo kutumia muda mwingi akiwa ndani ya nyumba yao ya kupanga.
Amesema kwa sasa anamtegemea mama yake mzazi kwa mahitaji mbalimbali ya kila siku, ikiwemo kumsaidia anapotaka kwenda chooni.
“Nikihitaji kwenda chooni, siwezi kutoka mwenyewe. Inabidi nimwite mama anisaidie. Hata ninapopata haja kubwa, mama ndiye anayenisaidia kwa kutumia ndoo,” amesema.
Licha ya kuwa na kiti cha magurudumu, bado anahitaji msaada wa kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuwekwa katika mkao unaofaa. Pia, anahitaji kusaidiwa kuuweka vizuri mkono wake wa kushoto kutokana na hali yake ya kiafya.
Changamoto hizo zimeongeza majukumu kwa mama yake, ambaye anajishughulisha na biashara ya kuuza matunda katika kituo cha daladala ili kukidhi mahitaji ya familia.
Pamoja na hali hiyo, James anasema changamoto zake hazijamfanya aachane na matumaini ya kupata elimu ya juu na kutimiza malengo yake ya maisha.
Alivyoanza kupoteza uwezo wa kutembea
James amesema dalili za tatizo lake zilianza mwaka 2016 alipokuwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mlowo, wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe.
Amesema awali alitembea kwa namna tofauti na watoto wengine, lakini kadiri muda ulivyopita, uwezo wake wa kutembea ulipungua na kuanza kutembea taratibu.
Mwaka 2022, alipokuwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kantalamba, mkoani Rukwa, hali yake ilizidi kuwa mbaya na akaanguka. Anasema tukio hilo lilikuwa mwanzo wa kushindwa kutembea na kujihudumia mwenyewe, ingawa aliendelea kufanya vizuri darasani.
Mwaka 2024, alihitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kwambinde. Baadaye alipata fursa ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda na Hospitali ya Ikonda ili kubaini chanzo cha tatizo lake.
Licha ya changamoto hizo, James hakukata tamaa. Aliendelea na safari yake ya elimu kwa kujiunga na kidato cha tano na sita, akijitahidi kutimiza ndoto yake ya kupata elimu ya juu.
Amesema alifanya mitihani ya kidato cha sita akiwa katika hali ngumu ya kiafya na kufanikiwa kuhitimu Mei 2026.
Baada ya kuhitimu, alikwenda kwa mama yake mdogo, Mlowo, mkoani Songwe. Mama yake mzazi alipopata taarifa kuhusu hali yake, alimchukua ili aendelee na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda.
Kwa mujibu wa James, vipimo vilivyofanyika vilibaini kuwa alikuwa na kifua kikuu, hivyo akaanza kutumia dawa kwa ajili ya matibabu.
Katika jitihada za kutafuta fedha za kujiunga na chuo kikuu, James amesema aliomba mkopo wa elimu kupitia utaratibu uliowekwa kwa watu wenye ulemavu, lakini alikumbana na changamoto wakati wa kuingiza namba katika mfumo wa maombi.
Amesema baada ya kusaidiwa kuwasilisha maombi kupitia utaratibu mwingine, alifanikiwa kupata mkopo wa Sh730,000.
Hata hivyo, kiasi hicho hakitoshi kugharamia mahitaji yote ya masomo, yakiwemo ada, malazi na gharama nyingine za chuoni.
Amesema anahitaji zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mwaka kwa ajili ya masomo, huku gharama za bweni zikielezwa kufikia zaidi ya Sh1.3 milioni.
Kutokana na hali hiyo, anawaomba wadau kujitokeza kumsaidia kukamilisha mahitaji ya kifedha ili aweze kuripoti chuoni na kuanza masomo.
“Naomba Watanzania na Rais wetu Samia Suluhu Hassan wanisaidie ili niweze kuendelea na elimu. Nimejitahidi kufika hapa nilipo licha ya hali yangu, lakini bila msaada wa kifedha ninaweza kushindwa kujiunga na chuo,” amesema.
Mama Mzazi wa James Kilasi, Hellberitha Ephraim, akimsaidia kusukumu kitimwendo cha umeme mara baada ya kukabidhiwa na Taasisi ya Tulia Trust kwa niaba ya Mbunge wa Uyole Dk Tulia Ackson. Picha na Hawa Mathias
Mama ndiye tegemeo la familia
James amesema yeye ndiye mtoto wa kwanza katika familia yao, akifuatiwa na mdogo wake aliyemaliza darasa la saba na anayetarajia kujiunga na kidato cha kwanza.
Amesema baba yao alifariki walipokuwa wadogo, hali iliyomfanya mama yao kubeba jukumu la kuwalea na kuwahudumia.
Mama yake ametegemea kipato kinachotokana na biashara ndogo ya kuuza matunda, ambacho anakitumia kugharamia mahitaji ya familia.
Hali hiyo inafanya iwe vigumu kwake kukidhi mahitaji ya kila siku na wakati huohuo kutafuta fedha za kumwezesha James kuendelea na elimu ya juu.
James ameomba wasamaria wema watakaoguswa na hali yake kumsaidia kwa kuchangia kupitia namba ya simu 0748368479.
Dk Tulia amsaidia kiti mwendo cha umeme
Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson ametoa msaada wa kiti cha magurudumu cha umeme kwa James ili kumrahisishia kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Msaada huo unatarajiwa kumsaidia katika shughuli zake za kila siku na kumwezesha kufuatilia ndoto yake ya kuendelea na elimu ya juu.
Mama mzazi wa James, Hellberitha Ephraim, amemshukuru Dk Tulia kwa kutimiza ahadi hiyo na kumsaidia mwanaye kupata kiti hicho.
“Mimi ni mama na baba wa familia. Nimekuwa kila kitu kwa wanangu wawili, akiwemo James, mzaliwa wangu wa kwanza. Pamoja na ulemavu wake, bado ana kiu ya kuendelea na elimu ya juu. Naomba Serikali na wadau wanisaidie kurejesha matumaini yaliyopotea,” amesema.
Aidha, Hellberitha ameomba msaada wa mtaji ili kuendeleza biashara yake ya matunda na kumudu mahitaji ya familia, ikiwemo kupata choo kinachofaa kwa ajili ya kumhudumia mwanaye mwenye ulemavu.
You may also like

Jeshi la Polisi laonya wanaohamasisha kufanyika vurugu

Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha


Leave a Reply