

Serikali yaandaa miradi ya maji kwa wawekezaji binafsi
Dar es Salaam. Pamoja na uwekezaji wa Sh1.8 trilioni uliofanywa na Serikali katika sekta ya maji vijijini, bado vijiji 1,575 havijafikiwa na huduma hiyo, huku mahitaji ya maji Dar es Salaam na Pwani yakizidi uwezo wa uzalishaji kwa zaidi ya mita za ujazo 167,000 kwa siku.
Hali hiyo imeifanya Serikali kutafuta ushirikiano na sekta binafsi katika kutekeleza miradi mikubwa ya maji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mipya, upanuzi wa mitambo ya uzalishaji na kupunguza upotevu wa maji.
Katika mkakati huo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imeainisha miradi mikubwa inayohitaji uwekezaji wa sekta binafsi, ikiwemo Mradi wa Maji wa Rufiji wenye thamani ya Sh4.6 trilioni.
Mradi huo unalenga kutumia maji kutoka bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere lililopo katika Mto Rufiji kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Akizungumza katika mkutano wa wahariri, taasisi za umma na wawekezaji ulioandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), ofisa mwandamizi wa Dawasa, Daniel Mauma amesema mradi huo utatekelezwa kwa awamu.
Amesema awamu ya kwanza inalenga kuchukua, kutibu na kusafirisha lita milioni 750 za maji kwa siku kupitia njia kuu mbili za mabomba.
“Mradi utakapokamilika kikamilifu, uwezo wa kusambaza maji utafikia mita za ujazo milioni 1.5 kwa siku, kiwango kitakachokidhi mahitaji ya Dar es Salaam na Pwani hadi baada ya mwaka 2050, huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza huduma hadi Mkoa wa Lindi,” amesema.
Miundombinu ya mradi huo itahusisha vituo vya kuchukua maji, mitambo ya kutibu maji, vituo viwili vya kusukuma maji na matenki sita yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 93.
Mbali na mradi huo, Dawasa inaendelea na maandalizi ya upanuzi na ukarabati wa mtambo wa Ruvu Chini unaogharimu Dola za Marekani milioni 111.5.
Mauma amesema mtambo huo kwa sasa unazalisha lita milioni 270 kwa siku, lakini ukarabati na upanuzi unaopangwa utaongeza uzalishaji kwa lita milioni 90 na kufikisha lita milioni 360 kwa siku.
“Chini ya mfumo wa ubia, wawekezaji binafsi watafadhili ukarabati na upanuzi wa mtambo huo, kisha kuuza maji yaliyotibiwa kwa Dawasa kwa ajili ya kuyasambaza kwa wananchi,” amesema.
Katika kukabiliana na changamoto za kukatika kwa umeme na gharama zake, mamlaka hiyo pia imeandaa mradi wa Sh114 bilioni wa kufunga mifumo ya nishati ya jua katika mitambo mikubwa ya uzalishaji na vituo vya kusukuma maji.
Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa umeme wa gridi ya Taifa, kuzuia kusimama kwa uzalishaji wakati umeme unapokatika na kupunguza gharama za uendeshaji.
Pamoja na kuongeza uzalishaji, Dawasa imeeleza kuwa inataka kutumia sekta binafsi kupunguza upotevu wa maji unaotokana na uvujaji wa mabomba na changamoto nyingine katika mfumo wa usambazaji.
Mauma amesema miradi ya majaribio inatarajiwa kuanza Kibaha kwa gharama ya Sh30 bilioni na Bagamoyo, ambapo kampuni binafsi zitawekeza katika teknolojia za kubaini na kurekebisha uvujaji wa mabomba.
Amesema malipo kwa kampuni hizo yatazingatia kiwango cha maji kitakachookolewa baada ya kufanya marekebisho.
Kwa sasa, Dawasa inazalisha mita za ujazo 553,000 za maji kwa siku, wakati mahitaji katika maeneo inayohudumia ni mita za ujazo 720,000, hivyo kuwa na upungufu wa zaidi ya mita za ujazo 167,000 kwa siku.
Mauma amesema mahitaji hayo yanatarajiwa kuongezeka hadi mita za ujazo milioni 1.3 kwa siku ifikapo mwaka 2050.
Ametaja ongezeko la gharama za umeme, kemikali na matengenezo kuwa miongoni mwa changamoto zinazokwamisha uwekezaji katika miundombinu ya maji, akibainisha kuwa nauli za maji hazijabadilika tangu mwaka 2010.
Pia, amesema ujenzi wa barabara, hususan katika eneo la Tegeta, umekuwa ukisababisha uharibifu wa mabomba ya maji yaliyofukiwa ardhini.
Aidha, mabomba ya zamani katika maeneo ambayo nyumba za kawaida zinabadilishwa na majengo ya ghorofa yanaongeza hatari ya uvujaji wa maji na kuingia katika mifumo ya majitaka.
Hata hivyo, amesema Dawasa inaendelea kutumia fedha zake na za Serikali kukabiliana na upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuchimba visima tisa Kimbiji na kuendeleza vyanzo vingine vya maji Temeke na Kigamboni.
Kwa upande wa maeneo ya vijijini, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) umeandaa mradi wa majaribio wa Sh152 bilioni mkoani Dodoma, unaolenga kupima uwezo wa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi, ufadhili, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.
Mhandisi wa rasilimali za maji na mtaalamu wa huduma za kiufundi wa wakala huo, Davis Rweyemamu, amesema Ruwasa imeandaa mradi huo kwa kuzingatia uzoefu wa Senegal na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2025.
Amesema Ruwasa inasimamia huduma za maji katika mikoa 25 na wilaya 128 za Tanzania Bara, hivyo mafanikio ya mradi wa majaribio yatatoa mwongozo wa kupanua mfumo huo katika maeneo mengine.
Amesema hadi Desemba mwaka jana, upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa umefikia asilimia 85.2 kutokana na uwekezaji wa Serikali wa jumla ya Sh1.8 trilioni.
“Licha ya mafanikio hayo, bado vijiji 1,575 havijafikiwa na huduma ya maji safi. Tunahitaji ushirikiano na sekta binafsi ili kufikia lengo la huduma kwa wote ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Ameongeza kuwa uwekezaji wa sekta binafsi unaweza kupunguza gharama kubwa za kujenga miundombinu katika maeneo ya vijijini ambako makazi ya wananchi yametawanyika, pamoja na kuimarisha taasisi za kijamii zinazohusika na usimamizi wa huduma za maji.
Rweyemamu amesema mpango huo pia unalenga kuongeza matumizi ya mita za maji ili kuboresha upimaji wa matumizi, utozaji wa bili na ukusanyaji wa mapato.
Amesema upatikanaji wa mapato ya uhakika na matengenezo ya mara kwa mara ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maji inaendelea kufanya kazi hata baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Katika mkakati huo, Ruwasa pia imebainisha fursa za kupata fedha kupitia miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikitolea mfano wa mradi mkoani Manyara unaozalisha mapato ya mabilioni ya fedha kupitia biashara ya hewa ukaa.
Rweyemamu amesema upatikanaji wa maji safi unapunguza ulazima wa wananchi kukata miti kwa ajili ya kuni za kuchemshia maji, hivyo kusaidia kupunguza uharibifu wa misitu na wakati huohuo kuanzisha chanzo kingine cha mapato.
Sekta binafsi kupewa nafasi
Akifungua mkutano huo Jumatatu, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja.
Amesema Serikali haiwezi kutegemea rasilimali zake pekee kugharamia mahitaji yote ya miundombinu yanayohitajika kufikia malengo hayo.
“Maelekezo ya Dira 2050 ni kuwa sekta binafsi ichangie asilimia 70 katika kufanikisha malengo ya maendeleo. Hivyo, ushiriki wake ni muhimu katika kufikia malengo hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa ongezeko la kasi la idadi ya watu linaongeza mahitaji ya uwekezaji katika sekta za nishati, afya, maji na usafiri ili kuimarisha uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
You may also like

Hizi hapa fursa kwa vijana ziara za Rais Samia Uganda, Ethiopia

Tanzania, Zambia na China zaweka mkakati mpya wa Tazara


Leave a Reply