

Hizi hapa fursa kwa vijana ziara za Rais Samia Uganda, Ethiopia
Dar es Salaam. Vijana wa Tanzania wanatarajiwa kunufaika na fursa mpya za ajira, biashara, mafunzo ya kitaaluma na masoko zitakazotokana na miradi ya reli na bandari, pamoja na ushirikiano katika teknolojia na ubunifu kwenye sekta ya afya.
Fursa hizo zinatokana na makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na uchukuzi kati ya Tanzania na Uganda, pamoja na nafasi ya Tanzania katika kuongoza ajenda ya kuboresha afya ya mama, mtoto mchanga, watoto na vijana barani Afrika.
Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kitaifa nchini Uganda Novemba 18 hadi 19, 2026, kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni, kabla ya kuelekea Ethiopia Novemba 22 hadi 23, 2026, ambako alishiriki mkutano wa tano wa kimataifa wa afya ya umma barani Afrika (CPHIA 2026) na uzinduzi wa mpango elekezi wa afya ya mama na mtoto.
Akizungumza leo, Jumanne, Novemba 24, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, amesema ziara hizo mbili zina malengo yanayokamilishana, yakilenga kupanua fursa za kiuchumi na kuimarisha afya za wananchi.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wakati walipotembelea Kiwanda cha Double Q Automotive Assembly Plant kilichopo Mpigi nchini Uganda, leo Novemba 19, 2026.
Amesema ziara ya Uganda ililenga kufungua fursa katika uchumi, biashara, viwanda na uwekezaji, huku ile ya Ethiopia ikijikita katika afya na ustawi wa watu kama msingi wa maendeleo ya kiuchumi.
“Ziara ya Uganda ililenga kupanua fursa za uzalishaji na biashara, wakati ziara ya Ethiopia ililenga kulinda na kuendeleza rasilimali muhimu zaidi ya taifa, ambayo ni watu wake,” amesema Machumu.
Akizungumzia manufaa ya kiuchumi, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema makubaliano kati ya Tanzania na Uganda yatafungua nafasi kwa vijana kushiriki katika miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwemo reli, bandari na usafirishaji wa mizigo.
Amesema mojawapo ya miradi iliyokubaliwa ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Isaka, kupitia Lusahunga hadi Uganda, yenye urefu wa kilomita 620.
Ameeleza kuwa mradi huo utaongeza mahitaji ya wataalamu wa uhandisi, ujenzi, uendeshaji na matengenezo, huku ukichochea shughuli za biashara katika maeneo utakayopita.
“Vijana wa Tanzania wanapaswa kuwa washiriki wakubwa katika maendeleo ya nchi yetu, wapate ajira, waanzishe biashara na kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa miradi mikubwa tunayotekeleza,” amesema.
Mbarawa amesema kuimarishwa kwa usafiri wa majini katika Ziwa Victoria na kuboreshwa kwa Bandari ya Port Bell nchini Uganda kutapanua ajira katika huduma za bandari, meli na usafirishaji wa mizigo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Afrika (AICC), jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo Jumatatu, Novemba 23, 2026.
Ameongeza kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya biashara kutarahisisha upatikanaji wa soko la Uganda kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania, hivyo kutoa nafasi kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo, usindikaji na biashara kuongeza uzalishaji na kipato.
Kwa upande wa Ethiopia, nafasi ya Rais Samia kuwa kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa afya ya mama na mtoto inatarajiwa kuongeza ushirikiano wa kitaaluma na kufungua fursa kwa taasisi za afya, vyuo, hospitali na watafiti wa Tanzania.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hatua inayofuata baada ya kuzinduliwa kwa mpango elekezi wa AU wa kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga, watoto na vijana (2026–2030), ni kuhakikisha ahadi za viongozi zinabadilishwa kuwa matokeo yanayopimika.
Amesema Tanzania itatoa mafunzo kwa wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kupitia programu za muda mfupi, mafunzo kwa vitendo katika vituo vya afya na ushauri wa kitaalamu.
Maeneo yatakayolengwa ni ukunga, uuguzi, malaria, huduma za dharura na huduma kwa watoto wachanga.
“Fursa hizi zinakusudia wataalamu wetu mbalimbali walioko kwenye sekta ya afya kuja pamoja kuongeza chachu ya maendeleo katika sekta ya afya, hasa katika vita dhidi ya vifo vya mama na watoto,” amesema.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wakati walipotembelea Kiwanda cha Double Q Automotive Assembly Plant kilichopo Mpigi nchini Uganda, leo Novemba 19, 2026.
Amesema ushirikiano huo utawezesha wataalamu wa Tanzania kwenda nchi nyingine kutoa mafunzo, huku wataalamu kutoka mataifa hayo wakija nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania.
Ameongeza kuwa sekretarieti ya mpango huo inatarajia kuandaa warsha za ngazi ya juu kuanzia Desemba 2026 na kuendelea mwanzoni mwa mwaka 2027, zitakazoshirikisha nchi wanachama, wataalamu na washirika wa maendeleo.
Vijana kunufaika na teknolojia
Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, amesema nafasi hiyo itafungua milango kwa vyuo, hospitali, taasisi za utafiti na sekta binafsi kushirikiana na mataifa mengine kuboresha huduma za afya.
Amesema vyuo vitapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha elimu ya afya, huku taasisi za utafiti zikipanua wigo wa tafiti kupitia ushirikiano wa kikanda.
Ameeleza kuwa sekta binafsi pia inaweza kunufaika kwa kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wakati walipotembelea Kiwanda cha Double Q Automotive Assembly Plant kilichopo Mpigi nchini Uganda, leo Novemba 19, 2026.
Kwa upande wa vijana, amesema watapata nafasi ya kushiriki katika maamuzi na ubunifu wa teknolojia za kidijitali zinazolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.
Amesisitiza kuwa vijana hawapaswi kuonekana kama walengwa wa huduma pekee, bali washirika muhimu katika kubuni, kutekeleza na kufuatilia maboresho ya mifumo ya afya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Milya, amesema ziara hizo zinaimarisha nafasi ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa na kuongeza uwezo wake wa kushirikiana na mataifa na taasisi mbalimbali.
Amesema nafasi ya Rais Samia katika ajenda ya afya ya mama na mtoto itatoa fursa kwa Tanzania kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) na washirika wengine wa maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, akizungumza wakati wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Afrika (AICC), jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo Jumatatu, Novemba 23, 2026.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo unaweza kuongeza upatikanaji wa utaalamu, teknolojia, dawa na vifaa tiba, pamoja na kufungua nafasi za ufadhili wa miradi ya afya na tafiti za kisayansi.
Aidha, amesema vijana, watafiti na kampuni changa za teknolojia zinaweza kunufaika kwa kupata mitaji, utaalamu na masoko ya kimataifa.
Ameongeza kuwa kuboresha afya ya mama na mtoto kuna manufaa ya kiuchumi kwa familia na taifa, kwa kuwa wanawake wenye afya bora wanapata nafasi zaidi ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji.
Hata hivyo, amesema manufaa ya ziara hizo yatategemea utekelezaji wa makubaliano, upatikanaji wa uwekezaji na ushiriki wa Watanzania katika fursa zitakazofunguliwa, ili diplomasia hiyo izalishe ajira, biashara, huduma bora za afya na maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi.
You may also like

Serikali yaandaa miradi ya maji kwa wawekezaji binafsi

Tanzania, Zambia na China zaweka mkakati mpya wa Tazara


Leave a Reply