

Watano mbaroni Tanga kwa tuhuma za mauaji
Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika wilaya za Muheza na Handeni, huku tukio moja likidaiwa kuchochewa na wivu wa mapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Oktoba 23, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema katika tukio la kwanza, wanamshikilia Mbaraka Athumani Mkomwa, mwenye umri wa miaka 28, kwa tuhuma za kumuua Jennifer Elias Kipingu, aliyekuwa mpenzi wake.
Amesema mwili wa marehemu ulikutwa Septemba 23, 2026, katika bonde la Mto Mission, Kata ya Mlingano, Wilaya ya Muheza, huku mauaji hayo yakidaiwa kuchochewa na wivu wa mapenzi.
Katika tukio la pili, Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kumuua Athuman Juma Said, katika tukio lililoripotiwa Oktoba 21, 2026, Wilaya ya Handeni.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 22, 2026, katika Kitongoji cha Kwedigasu, Kijiji cha Mkata Mashariki, Kata ya Mkata, kufuatia msako uliofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi wenye uelewa wa mazingira ya eneo hilo.
“Watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi huku taratibu za uchunguzi zikiendelea kukamilishwa,” amesema Mchunguzi.
Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Aidha, amewataka wananchi kutatua tofauti zao kwa njia za amani na kuepuka vitendo vya ukatili vinavyoweza kusababisha vifo, huku akiwahimiza kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vyake kwa Jeshi la Polisi ili kulinda amani na usalama katika jamii.
“Tunawahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vyake,” amesema Mchunguzi.



Leave a Reply