

Chatanda awatahadharisha wananchi ahadi za vyama Chamwino
Chamwino. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amewataka wananchi wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma kuwa makini na ahadi za vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge, akisisitiza umuhimu wa kutathmini uwezo wa vyama kutekeleza mipango ya maendeleo.
Chatanda ametoa kauli hiyo Oktoba 22, 2026, wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Netho Ndilito, katika mikutano ya ndani iliyofanyika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Amesema baadhi ya makundi yanawaomba wananchi kura bila kuwa na uwezo wa kusimamia mipango ya maendeleo kupitia Serikali.
Baadhi ya wanachama na wananchi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakimsikiliza mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia CCM, Dk Netho Ndilito, kwenye kampeni zinazoendelea jimboni humo
“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa chama kinachoomba kura kina wajibu wa kuonyesha uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo,” amesema.
Amesisitiza kuwa CCM ina Ilani ya Uchaguzi inayobainisha mikakati ya kushughulikia changamoto za wananchi na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika mkutano huo uliofanyika Kata ya Msanga, Kijiji cha Msanga, Chatanda amesema mgombea huyo amekabidhiwa faili lenye changamoto za jimbo hilo pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayobainisha mikakati ya kuzitatua.
“Faili la changamoto za Jimbo la Chamwino limekabidhiwa kwa Dk Netho Ndilito, likiwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayoainisha mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema.
Amesema faili hilo lilikabidhiwa kwa Dk Ndilito na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ambaye awali alikuwa Mbunge wa Chamwino kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Baadhi ya wanachama na wananchi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakimsikiliza mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia CCM, Dk Netho Ndilito, kwenye kampeni zinazoendelea jimboni humo
Chatanda amewataka wanachama wa CCM na wananchi wengine kujitokeza kwa wingi Novemba 4, 2026, kushiriki uchaguzi huo na kumpigia kura Dk Ndilito ili kupata ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.
Aidha, ameurudia wito huo katika mikutano iliyofanyika Kitongoji cha Chichinka, Kata ya Segala, na Kijiji cha Solou, Kata ya Itiso, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki uchaguzi.
Naye, Dk Ndilito amewaomba wanaChamwino wampe imani yao na kumchagua kuwawakilisha na kwamba hatawaangusha katika kuwaletea maendeleo ya kweli.
Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Ndejembi baada ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na CCM, vyama vingine vilivyotajwa kushiriki uchaguzi huo ni UDP kilichomsimamisha Nasma Judi Hamisi, na Chama cha Wakulima (AAFP), kinachomsimamisha Exavery Mapunda.
You may also like

Nkasi kuweka mfumo wa kielektroniki kudhibiti utoro wa watumishi



Leave a Reply