

Aliyehukumiwa kifo kwa kumuua mkewe aachiwa huru
Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imemwachia huru Michael Thomas aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya mkewe, Maria Raymond, baada ya kubaini kuwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani haukuthibitisha bila shaka ya msingi kuwa ndiye aliyemuua.
Imesema Mahakama Kuu ilikosea kutumia kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, kwa kuwa ushahidi haukuonyesha kuwa mrufani ndiye mtu wa mwisho kumuona mkewe akiwa hai.
Uamuzi uliobatilisha hukumu hiyo umetolewa Oktoba 23, 2026 na majaji watatu ambao ni Lilian Mashaka, Abraham Mwampashi na Mustafa Ismail waliokuwa wakisikiliza rufaa ya jinai iliyokatwa na Michael, aliyekuwa akipinga hukumu ya Novemba 29, 2024.
Awali, ilidaiwa Maria alipotea kwa siku nne kuanzia Julai 24, 2010 hadi Julai 28, 2010 ambapo mwili wake ulikutwa ukiwa umeanza kuharibika katika mashamba ya Kijiji cha Mtunungu, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kupatikana ilidaiwa mrufani alitoweka kijiji cha Mwena alipokuwa akiishi na mkewe (marehemu kwa sasa), ambapo alidaiwa kurejea miaka 12 baadaye (Juni 28, 2022) ambapo alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Shahidi wa kwanza ambaye alikuwa mtoto wa marehemu na mtoto wa kambo wa mrufani, alidai mama yake, alipotea kwa siku nne kabla ya mwili wake kupatikana Julai 28, 2010 katika mashamba ya Kijiji cha Mtunungu ukiwa umeanza kuharibika.
Mtoto huyo alidai siku ya tukio mama aliondoka nyumbani akiwaacha mama yake, mshtakiwa na ndugu wengine na kuwa aliporejea siku iliyofuata, hakumkuta mama yake na alipomuuliza mshtakiwa alipo, aliambiwa kuwa alikuwa ameenda shambani.
Baada ya siku tatu bila mama yake kurejea, alidai kuongozana na mrufani walikwenda shambani kumtafuta lakini hawakumpata.
Katika utetezi wake mbele ya Mahakama Kuu,Michael alikana kumuua Maria huku akikiri kuwa Maria alikuwa mke wake kuanzia mwaka 1999, lakini alidai walikuwa wameachana mwaka 2008.
Alieleza kuwa baada ya kutengana, alihama Kijiji cha Mwena na kwenda Mateko Nyamichinga, hivyo hakujua kuhusu kifo cha marehemu na kuwa aliporejea kijijini baada ya miaka 12 na kukaa huko kwa wiki moja, alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji.
Hata hivyo, Mahakama Kuu haikukubaliana na utetezi wake, ikamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Jaji Mwampashi, amesema Mahakama imebaini kuwa ushahidi wa kimazingira haukuwa na nguvu ya kumhusisha Thomas na mauaji hayo bila kuacha shaka ya msingi.
Amesema pia haikuthibitishwa kwamba Thomas alikuwa mtu wa mwisho kumuona marehemu akiwa hai, kwa sababu wakati mtoto wa marehemu alipoondoka nyumbani, Maria alikuwa pamoja na Thomas na ndugu wengine ambao hawakuitwa kutoa ushahidi.
“Ili kanuni hiyo itumike na mshtakiwa adhaniwe kuwa muuaji, ni lazima ithibitishwe bila kuacha shaka ya msingi kuwa ndiye mtu wa mwisho kumuona marehemu akiwa hai,” amesema
Mahakama pia ilikataa kuhusisha moja kwa moja kutoweka kwa Thomas kwa miaka 12 na mauaji hayo, ikizingatia kuwa kabla ya kutoweka kwake alishiriki kumtafuta marehemu na alimwomba ndugu yake msaada wa kumtafuta.
“Kwa kawaida, mtu aliyemuua mwingine asingetarajiwa kubaki nyumbani kwa siku nne, kushiriki katika msako na kuomba msaada wa ndugu wa marehemu.”
Kuhusu ushahidi wa kimazingira, Mahakama ilisema haukufikia kiwango kinachohitajika kisheria kwa sababu mazingira yaliyotegemewa na Mahakama Kuu yangeweza pia kuelezeka kwa namna inayolingana na kutokuwa na hatia kwa Thomas.
“Mazingira yaliyotegemewa na Mahakama ya awali yaliendana pia na uwezekano wa kutokuwa na hatia na yangeweza kuelezeka kwa namna nyingine,”
Kutokana na dosari hizo Mahakama ya Rufaa ilibatilisha hukumu,ikafuta adhabu ya kifo na kuamuru Thomas aachiwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.
You may also like

Nkasi kuweka mfumo wa kielektroniki kudhibiti utoro wa watumishi



Leave a Reply