
Utafiti: Nishati ya jua kutumika kupikia

Unguja. Utafiti mpya katika sekta ya nishati safi unaonyesha uwezekano wa kuanza kutumia nishati ya jua kwa ajili ya kupikia, hatua inayotajwa kuwa itakuwa mkombozi kwa jamii hususani wanawake.
Hayo yamebainishwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), anayeshughulikia masuala ya utafiti, Profesa Nelson Boniface kwenye kongamano la tisa la kimataifa la Mechanical and Industrial Engineering, lililofanyika katika Taasisi ya Sayansi za Bahari visiwani Zanzibar.
Kongamano hilo lililofanyika kwa siku mbili Oktoba 22 na 23, liliwakutanisha wahandisi na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi kujadili tafiti na ubunifu katika masuala ya viwanda na ufundi mitambo.
Profesa Boniface amesema moja ya machapisho yaliyowasilishwa na kuvutia zaidi ni hilo la kutumia nishati jua kupikia.
“Ingawa kwa sasa nishati ya jua inatumika zaidi kutoa mwanga na joto la hita za maji majumbani, tafiti za awali zilizofanywa na watafiti zimeonyesha uwezekano mkubwa wa kuitumia nishati hiyo katika majiko ya kupikia,” amesema Profesa Boniface.
Amesema maendeleo haya ya kitafiti ni fursa ya kipekee kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kutokana na uwepo wa jua la kutosha kila siku.
Ili kufanikisha azma hiyo, Profesa Boniface ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono tafiti hizo ili zivuke hatua ya maabara na kupelekwa kwenye uzalishaji wa vifaa vya kupikia vitakavyoweza kutumiwa moja kwa moja na jamii.
Aidha, amewahimiza wahandisi na watafiti kuchapisha kazi zao kwa njia na lugha rahisi inayowezesha mtumiaji wa kawaida kuzielewa na kuzitumia.
Katika kutilia mkazo suala hilo, mtaalamu wa uhandisi wa umeme, Dk Avit Mushi amebainisha kuwa tafiti zilizowasilishwa zilionyesha uwezekano wa kutumia nishati ya jua kwa ajili ya kupikia, jambo linalounga mkono msukumo wa Rais katika kukuza nishati safi ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Ameeleza kuwa nishati ya jua ni safi na haichafui mazingira, hivyo itasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa yanayozalisha moshi mwingi na hewa ya ukaa.
“Utaratibu huu utasaidia kupunguza magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa wapishi na watoto wadogo, huku ikitunza mazingira na kuimarisha afya za Watanzania,” amesema Dk Mushi.
Mkuu wa Idara ya Uhandisi Mitambo na Viwanda Chuo Kikuu ch Dar es Salaam (UDSM), Dk Peresi Bulemo ameeleza kuwa mkutano huo ulikuwa fursa ya kushirikisha uvumbuzi unaoendelezwa na chuo hicho ili kuchochea maendeleo ya nchi.
Amebainisha kuwa utafiti na matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati, ikiwemo jotoardhi na jua, ni hatua muhimu ya kupunguza nishati zinazoharibu mazingira na kufikia malengo ya taifa ya ufanisi mkubwa wa nishati.
“Washiriki kutoka nchi za Scandinavia, zikiwemo Norway na Denmark, waliwasilisha mada zikionyesha mafanikio makubwa waliyoyapata katika matumizi ya nishati mbadala kama suluhisho la utunzaji wa mazingira,” amesema Dk Bulemo.
You may also like

Nkasi kuweka mfumo wa kielektroniki kudhibiti utoro wa watumishi


Leave a Reply