
Wataka boti ya doria kudhibiti wizi, kuimarisha uhifadhi
Unguja. Kikundi cha Uimarishaji na Uhifadhi Majongoo cha Unguja Ukuu Kaepwani, Wilaya ya Kati Unguja, kimeeleza dhamira yake ya kuendelea kutunza mazingira ya bahari ili kukuza biashara endelevu na utalii.
Mwenyekiti msaidizi wa kikundi hicho, Soud Faki Hamad ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi kuwapatia boti, hata kama ni ya mkopo, kwa ajili ya kufanya doria katika eneo la ufugaji ili kupunguza changamoto ya wizi.
“Hapa kuna wizi mkubwa, tunaomba kupatiwa boti ya kufanya doria, jambo litakalopunguza uhalifu huo,” amesema Faki mbele ya maofisa wa wizara katika eneo la kikundi hicho Oktoba 23, Mkoa wa Kusini Unguja.
Naye, mjumbe wa kikundi hicho, Asha Faki Kadi amesema uhifadhi wa mikoko baharini una mchango mkubwa katika kuongeza mazalia ya samaki, majongoo na kaa tope, jambo linaloleta tija kwa wafugaji na Serikali kwa ujumla.
“Sisi tupo tayari kutunza mazingira kwa ajili ya kukuza biashara, uhifadhi na utalii,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Ufugaji wa Viumbe vya Baharini kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Thomas Raphael, amewashauri wafugaji hao kukarabati mabwawa ya ufugaji ili yaendane na mazingira ya viumbe hao ili kupata uzalishaji wenye tija.
Pia, amewataka wanakikundi kuchukua vifaranga vya majongoo kutoka Kituo cha Hatchery kilichopo Bet-ras, ili kufuga kwa utaalamu zaidi na kuvuna kwa wakati.
Kwa upande wake, Ofisa Ushirika kutoka Wilaya ya Mjini Unguja, Hassan Ali Mbarouk amesema ni muhimu kwa kikundi kuwa na hati ya umiliki wa eneo hilo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Ziara hiyo ya kikazi imeandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar kwa kushirikiana na Wilaya ya Mjini Unguja.
You may also like


Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha

Leave a Reply