

Vijana watakiwa kutumia vipaji, teknolojia kujiletea maendeleo
Dar es Salaam. Vijana nchini wametakiwa kutambua na kukuza vipaji vyao, kutumia teknolojia na kujifunza ujuzi mbalimbali ili kujitengenezea fursa za ajira na ujasiriamali badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Oktoba 24, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wanawake Wafanyabiashara Jumuiya ya Afrika Mashariki, Janice Kimaro, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana la ‘ Tawen Youth’ Mkoa wa Dar es Salaam.
Janice amesema kila kijana ana kipaji na uwezo wa kipekee unaoweza kuchangia maendeleo yake na taifa kwa ujumla, akiwataka kutokata tamaa kwa sababu ya kukosa elimu ya juu au sifa fulani, bali kutumia uwezo walionao kujiletea maendeleo.
Amesema pia elimu ya ujasiriamali inapaswa kupewa kipaumbele kuanzia shule za msingi ili kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kutengeneza ajira.
“Pia, ni vema vijana kusoma na kuelewa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kutambua nafasi na wajibu wao katika kufikia malengo ya taifa,”amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Amina Salum Ali akiwasili kwenye Mkutano wa uzinduzi wa mtandao wa Vijana wa taasisi hiyo ‘TAWEN Youth’s jijini Dar es Salaam leo, Octoba 24,2026 akiwa na Junice Kimaro Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwa la Wanake Wafanyabiashara Afrika Mashabiki (kushoto) wakipokelewa na Mwenyekiti wa TAWEN Mkoa wa Dar es Salaam, Tariq Ninga. Picha na Said Powa
Janice amesisitiza kuwa kuwawezesha vijana ni kuwekeza katika maendeleo ya taifa la kesho, hivyo wanapaswa kujengewa uwezo, kupewa mwongozo na kuunganishwa na fursa zinazopatikana ndani na nje ya nchi.
“Pamoja na hayo pia vijana ni muhimu kuwa na washauri na walezi wa kitaaluma (mentors) watakaowasaidia kukuza ujuzi, kufanya maamuzi sahihi na kupiga hatua katika shughuli zeni,”amesisitiza.
Kuhusu teknolojia, Janice amesema vijana wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kujifunza na kupata maarifa badala ya kutumia muda mwingi kutazama maudhui yasiyowaongezea ujuzi.
Amesema mabadiliko ya teknolojia yanawataka vijana kujifunza matumizi ya teknolojia mpya, ikiwemo akili unde, ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Pia, amewahimiza kufuatilia fursa zinazotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, zikiwemo mitandao ya vijana, majukwaa ya biashara na programu za kuwawezesha wanawake na vijana.
Amesema Tawen inapaswa kuwa na mpango mkakati unaopimika ili utekelezaji wa shughuli zake utathminiwe na matokeo yaonekane katika maisha ya vijana na jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tawen, Balozi Amina Said Ali, amesema vijana ni muhimu katika maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kupewa nafasi, kuungwa mkono na kushirikishwa katika ujenzi wa Tanzania.
Balozi Amina amesema ujana unaambatana na majukumu ya kitaifa, hivyo kila kijana anapaswa kuelewa wajibu wake na kuutekeleza kwa manufaa ya jamii.
“Ninafahamu kuwa bado kuna mambo mengi ya kufanya, lakini nina matumaini kwamba kupitia ushirikiano, hatua zitachukuliwa moja baada ya nyingine ili kuwasaidia vijana kufikia malengo yao,” amesema.
Ameongeza kuwa Tawen inaweza kuwa chombo cha kuelimisha jamii na vijana, kuhamasisha kujitolea na kuhimiza kazi zinazochangia maendeleo ya taifa na dunia.
Awali, Mwenyekiti wa Tawen Mkoa wa Dar es Salaam, Tariq Ninga, amesema jukwaa hilo linalenga kuwaunganisha vijana kutoka taasisi mbalimbali, vyuo, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo ili kujadili changamoto zao na kutafuta suluhisho.
Ninga amesema pia linalenga kujenga ushirikiano kati ya vijana, Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na elimu pamoja na mashirika ya maendeleo ili kupanua fursa za ajira na uwekezaji.
Kuhusu mazingira, amesema jukwaa hilo linashirikiana na wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhamasisha usafi, uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo, amesema wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa rasilimali na vifaa, uelewa mdogo wa baadhi ya wadau kuhusu masuala ya vijana na ukosefu wa ofisi ya tawi mkoani humo.
Kutokana na hali hiyo, amewaomba wadau kusaidia kuimarisha jukwaa hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
You may also like

Nkasi kuweka mfumo wa kielektroniki kudhibiti utoro wa watumishi


Leave a Reply