

Teknolojia ya kupima viinitete yazindua ukurasa mpya wa huduma za uzazi
Dar es Salaam. Wanandoa wanaokabiliwa na changamoto za kupata watoto, kuharibikiwa na mimba mara kwa mara au hatari ya kurithisha watoto magonjwa ya vinasaba sasa wanaweza kunufaika na teknolojia ya uchunguzi wa viinitete kabla ya kupandikizwa kwenye mfuko wa uzazi.
Teknolojia hiyo, inayojulikana kama Preimplantation Genetic Testing (PGT), hutumika kuchunguza baadhi ya hitilafu za kromosomu na mabadiliko ya kijeni yanayoweza kusababisha magonjwa ya kurithi katika viinitete vinavyotengenezwa kwa njia ya urutubishaji wa mayai nje ya mwili (IVF).
Mkurugenzi wa Tiba wa kituo cha New Life Advanced Fertility Center, Dk Madhav Hiran, amesema teknolojia hiyo inaongeza chaguo za matibabu kwa wanandoa, hasa wale walio katika hatari ya kurithisha watoto wao magonjwa ya vinasaba.
Amesema baadhi ya wazazi wanaweza kuwa na mabadiliko ya kijeni yanayosababisha magonjwa bila kuonyesha dalili, hivyo uchunguzi unaweza kusaidia kutambua hatari hizo kabla ya kuchagua kiinitete kwa ajili ya kupandikizwa.
Dk Hiran amesema maendeleo hayo ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma za kisasa za uzazi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Uchunguzi kabla ya upandikizaji
Dk Sheila Ramadhani, wa kituo hicho kilichopo Msasani, Dar es Salaam, amesema uchunguzi wa PGT hufanyika baada ya mayai kurutubishwa maabara, lakini kabla ya kiinitete kuhamishiwa kwenye mfuko wa uzazi.
Amesema hitilafu za kromosomu ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia kuharibika kwa mimba, hususan katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.
“Kwa hiyo, ili kutatua tatizo hili kuna kipimo kinachoitwa Preimplantation Genetic Testing. Hiki kipimo hupima vinasaba katika hatua ya awali kabisa ya kiinitete kabla ya kukipandikiza,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Ramadhani, uchunguzi huo unaweza kubaini baadhi ya hitilafu za kromosomu zinazohusishwa na hali kama Down syndrome na Turner syndrome.
Hata hivyo, PGT haiwezi kubaini kila aina ya ugonjwa au kuhakikisha kuwa mtoto atakayezaliwa hatakuwa na matatizo ya kiafya. Matokeo yake hutegemea aina ya uchunguzi uliofanyika na hitilafu inayotafutwa.
Zaidi ya vipimo 800 vimefanyika
Dk Ramadhani amesema tangu huduma hiyo ianze kutolewa katika kituo hicho zaidi ya mwaka mmoja na nusu uliopita, vipimo zaidi ya 800 vimefanyika.
Amesema zaidi ya wanandoa 150 wameripotiwa kupata ujauzito na kujifungua baada ya kupata huduma hizo.
Takwimu hizo zinaeleza uzoefu wa kituo hicho katika utoaji wa huduma, ingawa hazimaanishi kuwa kila kipimo hutoa matokeo ya kupata ujauzito au kujifungua.
Teknolojia kusaidia familia
Kwa upande wake, Dk Hiran amesema teknolojia hiyo inaweza pia kuwa na nafasi katika kusaidia baadhi ya familia zenye watoto wanaougua magonjwa ya kurithi yanayohitaji matibabu maalumu.
Ametoa mfano wa utaratibu unaojulikana kama saviour sibling, unaoweza kuhusisha IVF, uchunguzi wa vinasaba na upimaji wa ulinganifu wa tishu za kinga, unaofahamika kama HLA.
Kupitia utaratibu huo, familia inaweza kutafuta kupata mtoto ambaye seli shina zake zinaweza kufaa kusaidia matibabu ya ndugu yake mwenye ugonjwa unaoweza kutibiwa kwa njia hiyo.
Hata hivyo, Dk Hiran amesema utaratibu huo unahitaji tathmini ya kitaalamu, huku usalama na masilahi ya watoto wote wanaohusika yakipewa kipaumbele.
Kwa ujumla, teknolojia ya PGT inaongeza uwezekano wa kupata taarifa muhimu za kijeni kabla ya upandikizaji wa kiinitete.
Hata hivyo, wataalamu wanapaswa kuwashauri wanandoa kuhusu manufaa, mipaka na hatari zinazoweza kuambatana na uchunguzi huo kabla ya kufanya maamuzi ya matibabu.
You may also like

DC avunja sherehe ya mahari ya mwanafunzi Bariadi

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola


Leave a Reply