

Kamera za kisasa kudhibiti ukatili watoto majumbani
Mbeya. Wazazi wanaotumia muda mwingi kazini au katika shughuli za biashara wanaweza kufuatilia mazingira ya watoto wao wakiwa mbali kupitia kamera za kisasa zinazo unganishwa na simu janja, hatua inayoweza kusaidia kubaini mapema matukio yanayohitaji uangalizi.
Kwa upande wa familia, kamera zinaweza kuwa nyenzo ya ziada ya kufuatilia mazingira ya watoto, hasa wanapokuwa chini ya uangalizi wa watu wengine wakati wazazi wanapokuwa kazini.
Stella Mathew anasema teknolojia hiyo inamwezesha kuona picha na kusikia sauti za eneo husika, jambo linalo msaidia kufahamu kinachoendelea nyumbani akiwa nje.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Oktoba 26, 2026, Stella anasema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuwa na manufaa kwa wanawake na wazazi wanaotumia muda mwingi katika shughuli za kujipatia kipato.
Hata hivyo, ufuatiliaji wa watoto kwa kutumia kamera unapaswa kwenda sambamba na mawasiliano ya karibu, malezi bora na hatua za haraka pale dalili za ukatili zinapobainika.
Anasisitiza umuhimu wa kuzingatia faragha na usalama wa familia wakati wa kutumia mifumo hiyo, ili kulinda watoto bila kuvunja haki za watu wengine.
Mbali na matumizi ya majumbani, teknolojia hiyo imeanza kuwasaidia baadhi ya wakulima kufuatilia shughuli za uzalishaji wakiwa mbali na mashamba yao.
Teodora Thobias, mkazi wa Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, anasema kamera hizo zimemsaidia kuboresha usimamizi wa shamba lake la mpunga katika misimu miwili ya uzalishaji.
Anasema mfumo huo umemwezesha kufuatilia shughuli za vibarua, mahitaji ya maji na hatua za ukuaji wa zao bila kulazimika kufika shambani kila mara.
“Awali nilikuwa naona hazina umuhimu, lakini katika misimu miwili ya uzalishaji wa mpunga nimepata matokeo mazuri ya ufuatiliaji, hususan shughuli za vibarua, mahitaji ya maji na kujua zao limefikia hatua gani,” anasema.
Thobias anasema awali shamba lake la ekari moja lilikuwa likizalisha kati ya gunia 10 na 15 za mpunga kwa msimu, lakini sasa anapata kati ya gunia 30 na 35.
Naye Salma Ahmad, mjasiriamali wa vipodozi katika eneo la Uyole, Mbeya, anasema jamii inapaswa kujifunza kutumia teknolojia za kisasa kuimarisha usalama wa watu na mali zao.
Anasema mifumo hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa wakulima na wachimbaji wa madini wanaohitaji kufuatilia shughuli za uzalishaji na ulinzi wa maeneo yao wakiwa mbali.
Picha na AI
“Teknolojia hii inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima na wachimbaji, lakini elimu inahitajika ili wananchi wafahamu namna ya kuitumia kuongeza tija na kuimarisha usalama,” anasema.
Meneja wa Kampuni ya CCTV Point mkoani Mbeya, Gift Joshua, anasema kamera hizo zinaweza kufungwa katika makazi ya watu, mashambani na maeneo ya migodi kulingana na mahitaji ya mteja.
Anasema mifumo hiyo inaweza kuhusisha kamera, umeme wa jua, vifaa vya kuhifadhi picha na video pamoja na mawasiliano ya intaneti yanayomwezesha mtumiaji kufuatilia eneo husika kupitia simu janja.
Kwa mujibu wa Joshua, baadhi ya mifumo ina uwezo wa kutoa tahadhari kwa mtumiaji inapotambua tukio lililowekwa kwenye mipangilio yake, huku uwezo wa kufuatilia picha na sauti ukitegemea aina ya kifaa na ubora wa mtandao.
“Tumekwenda mbali zaidi ya suala la ulinzi dhidi ya uhalifu. Kuna mifumo ambayo mteja anaunganishiwa kupitia simu janja na inaweza kutumia umeme wa jua, huku ikiwa na vifaa vya kuhifadhi taarifa na mawasiliano ya intaneti,” anasema.
Joshua anasema wateja wengi ni watu binafsi wanaotaka kuimarisha ulinzi wa makazi yao, wakiwamo wafanyakazi na wafanyabiashara wanaohitaji kufuatilia mazingira ya familia zao wanapokuwa nje.
Kuhusu gharama, Joshua anasema hutegemea ukubwa wa eneo, mahitaji ya mteja aina ya vifaa ambavyo anahitaji kufungiwa ambapo mafundi hufika kufanya tathmini kabla ya kutoa makadirio ya gharama za ufungaji, iwe ni nyumbani, shambani na uchimbaji wa madini.
Akizungumzia uzoefu wa kampuni hiyo, anasema imekuwa ikitoa huduma za mifumo ya kamera kwa miaka 19, ikilenga kusaidia taasisi na watu binafsi kuimarisha ulinzi wa watu na mali zao.
Hata hivyo, matumizi ya kamera majumbani yanahitaji kuzingatia faragha za watoto na watu wengine, kulinda nywila za mifumo na kuhakikisha taarifa zinazorekodiwa zinatunzwa kwa usalama.
You may also like


Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha


Leave a Reply