

Daladala Moro zakubali kurejea barabarani, Serikali ikitoa ahadi
Morogoro. Huduma za usafiri wa daladala katika Manispaa ya Morogoro zimeanza kurejea baada ya madereva kusitisha mgomo wa siku mbili uliosababishwa na kutoridhishwa na eneo waliloelekezwa kupakia abiria na madai ya bajaji kuingilia njia zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Daladala katika Manispaa ya Morogoro, Ramadhani Khasim amesema huduma hiyo imeanza kurejea taratibu asubuhi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, kufanya mazungumzo na madereva, wataalamu wa halmashauri, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na wadau wengine wa usafirishaji.
Akizungumza kwa niaba ya madereva, Khasim amesema mgomo huo ulilenga kuishinikiza Serikali kutenga eneo kubwa na lenye miundombinu rafiki kwa ajili ya stendi ya daladala, akieleza kuwa eneo waliloelekezwa kutumia ni finyu na haliwezi kutosheleza idadi ya magari hayo.
“Mwanzoni tulikuwa tukipakia abiria pale Ghorofa Chafu na Masika, lakini ghafla tulipewa agizo la kuhama maeneo hayo na kuambiwa twende tukapaki kwenye viwanja vya Soko la Fire. Ukiangalia lile eneo ni finyu na lina shughuli nyingi. Jambo hili madereva wengi hawakukubaliana nalo, ndiyo maana wakaamua kugoma,” amesema Khasim.
Amesema sababu nyingine iliyochangia mgomo huo ni bajaji kuingilia njia zinazotumiwa na daladala na kupakia abiria katika maeneo hayo, hali iliyowakera madereva wa daladala.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kumaliza mgomo huo, Kilakala amesema Serikali imekubaliana na madereva kuhusu utaratibu wa kurejesha huduma, ikiwemo kuwaruhusu kutumia tena stendi ya Ghorofa Chafu, waliyokuwa wakitumia awali.
Hata hivyo, amesema daladala zitatakiwa kutumia maeneo ya Ghorofa Chafu na Fire, huku akipiga marufuku matumizi ya eneo la Masika kama stendi ya daladala.
Eneo la Masika Manispaa ya Morogoro abiria wakisubiri usafiri baada ya madereva wa daladala kugoma kutoa huduma kwa kile wanachodai kuondolewa katika eneo hilo na kupelekwa kwenye stendi mpya ya fire. Picha Hamida Shariff
“Pale kwenye eneo la Masika walipofanyia stendi, kwa sasa hatutaki kuona daladala hata moja. Tunataka daladala ziende Ghorofa Chafu na Fire. Dereva yeyote atakayekaidi agizo hili atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Kilakala.
Amesema Serikali pia imeanza mikakati ya kutenga eneo rasmi kwa ajili ya stendi ya kudumu, ambapo eneo la Kikundi, lililo karibu na Soko Kuu la Kingalu, limependekezwa na madereva wenyewe pamoja na wadau wa usafirishaji.
Kwa mujibu wa Kilakala, tayari amewaagiza wataalamu wa halmashauri kufanya upembuzi wa kitaalamu ili kubaini namna bora ya kuboresha miundombinu ya eneo hilo, akilenga kuhakikisha stendi hiyo inaanza kufanya kazi mwaka 2027.
Amesema ujenzi wa stendi hiyo eneo la Kikundi utasaidia pia kuchangamsha Soko la Kingalu, ambako wafanyabiashara wengi wameacha vizimba vyao wazi na kuhamishia biashara nje ya soko hilo wakidai kuwa wateja ni wachache.
Kuhusu malalamiko ya madereva wa daladala dhidi ya bajaji kuingilia njia zao, Kilakala amewataka madereva wa bajaji kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na Latra.



Leave a Reply