

Wadau wa jinsia, Osha waonya unyanyasaji, hatari kazini
Kibaha. Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, ASP Eliud Malesa, amesema matumizi ya lugha chafu, kutongozana na vitendo vingine vinavyodhalilisha wafanyakazi ni miongoni mwa matendo ya unyanyasaji wa kijinsia kazini.
Amesema baadhi ya watu hutenda makosa hayo kwa kujua au bila kuelewa madhara ya kauli na matendo yao, akitolea mfano viongozi wanaowatamkia ‘lugha chafu’ watumishi wa chini yao wanapochelewa kazini au kushindwa kufikia malengo waliyopewa.
“Kiongozi anapotumia lugha chafu kwa mtumishi wa chini yake, mfano amechelewa au hajafikia lengo la kazi, anapewa maneno machafu yanayomsababishia mfadhaiko wa kiakili, anakuwa amefanyiwa unyanyasaji wa kisaikolojia,” amesema.
Malesa ameeleza kuwa unyanyasaji unaweza pia kujitokeza katika mahusiano ya kimapenzi kazini, ikiwemo pale kiongozi anapomtongoza mtumishi wake, mfanyakazi anapomtongoza kiongozi au wafanyakazi wanapofanyiana vitendo visivyokubalika.
Ametaja unyanyasaji wa kingono, kisaikolojia na kiuchumi, ubaguzi, matumizi mabaya ya teknolojia na kusambaza taarifa zinazodhalilisha wengine kwa njia mbalimbali ikiwemo makundi ya WhatsApp kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji tahadhari kazini.
Ameongeza kuwa migogoro ya kifamilia, malezi na mmomonyoko wa maadili ni baadhi ya vichocheo vya vitendo vya ukatili, akitoa wito kwa watumishi kutenga muda na familia zao na kujitathmini ili kuepusha nmatatizo hayo.
“Ukibahatika kupata kazi, fanya kazi bila kufanya ukatili kwa wenzako, unyanyasaji unaweza kuathiri afya ya akili na mahusiano kazini,” amesema.
Usalama na afya mahali pa kazi
Kwa upande wake, Mhandisi David Elisha, mhandisi wa majengo na afisa mkufunzi kutoka Osha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama na afya za wafanyakazi kwa kuzuia vihatarishi kabla havijasababisha ajali au madhara.
Amesema taasisi zinapaswa kuhakikisha njia za kupita hazina vizuizi, vimiminika vilivyomwagika vinasafishwa, nyaya zilizoharibika na usimamizi wa soketi za umeme ili kulinda usalama wa wafanyakazi.
“Ni muhimu pia kupanga meza na vifaa vya kazi katika mpangilio unaolinda mkao wa mwili, kupunguza uchovu, kudhibiti msongo wa mawazo na kuhakikisha wafanyakazi hawapati joto kali na kunywa maji ya kutosha Ofisini,” amesema.
Kwa watumiaji wa kompyuta, amesisitiza kanuni ya 20-20-20, akifafanua kwa kila baada ya dakika 20, inapaswa kutazama kitu kilicho umbali wa futi 20 kwa sekunde 20 ili kusaidia kupunguza uchovu wa macho kwa kuangalia kompyuta muda mrefu.
Elisha amesisitiza kuwa usalama ni jukumu la pamoja linalohitaji uongozi kutoa rasilimali na mafunzo, wasimamizi kurekebisha hali hatarishi na wafanyakazi kufuata taratibu, kutumia vifaa kinga na kuripoti vihatarishi.
“Kutambua hatari, kutathmini madhara, kuweka udhibiti, kurekodi hatua na kufanya mapitio ni muhimu katika kujenga mazingira salama Kazini,” ameongeza.
You may also like

Chadema, Magereza zatofautiana kuhusu mgomo wa kula kwa Lissu

Polisi Dodoma yawahakikishia usalama wanaofanya biashara usiku


Leave a Reply