

Chadema, Magereza zatofautiana kuhusu mgomo wa kula kwa Lissu
Dar es Salaam. Taarifa zinazokinzana kuhusu hali ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, zimeibuka baada ya chama hicho kudai ameanza mgomo wa kula akiwa mahabusu, huku Jeshi la Magereza likikanusha na kusema yupo salama na mawakili wake wanaruhusiwa kumtembelea kwa mujibu wa taratibu.
Chadema inadai Lissu alianza mgomo wa kula Oktoba 26, 2026, ikiwa ni hatua ya kupinga kile inachodai kuwa ni kuingiliwa kwa haki yake ya kupata msaada wa kisheria na kuzungumza na mawakili wake kwa faragha akiwa Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jeshi la Magereza, kupitia msemaji wake, Elizabeth Mbezi limekanusha madai hayo katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 27, 2026, likisema taarifa zilizosambazwa kuhusu Lissu kugoma kula na mawakili wake kuzuiwa kumwona si za kweli.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu Oktoba 26, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia mawakili watatu wa Lissu, Dickson Matata, Doris Kafuku na Neema Massame, walikwenda gerezani siku hiyo kwa lengo la kumwona na kuwasiliana naye, lakini walizuiwa kuingia.
“Chadema inaeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuzuiwa kwa mawakili hao kumwona Mwenyekiti wa chama, hasa wakati huu ambapo tayari ameanza mgomo wa kula. Hali hii inazua maswali mazito kuhusu upatikanaji wa huduma za kisheria na namna haki za Tundu Lissu zinavyolindwa akiwa gerezani,” alisema.
Chama hicho kilizitaka mamlaka husika kuhakikisha mawakili hao wanaruhusiwa kumwona Lissu bila vikwazo visivyo na msingi wa kisheria, kikisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kulinda usalama na ustawi wake.
Akijibu madai hayo katika taarifa kwa umma leo, Mbezi amesema taarifa zinazosambazwa mitandaoni kuhusu Lissu kugoma kula na mawakili wake kuzuiwa kuingia gerezani ni za upotoshaji na zinaweza kuleta taharuki katika jamii.
“Jeshi la Magereza linapenda kuujulisha umma kwamba mahabusu Tundu Lissu yupo salama na hayupo katika mgomo wa kula chakula kama ilivyoripotiwa,” amesema.
Kuhusu mawakili wake, Mbezi amesema wameendelea kuruhusiwa kukutana na mteja wao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo, baada ya kuthibitisha kuwa ni mawakili wake halali.
Amesema jeshi hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kupokea, kuhifadhi na kurekebisha watu wanaoshikiliwa magerezani, huku likizingatia usalama wao katika kipindi chote wanachokuwa chini ya ulinzi wake.
Mbezi pia alitoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa ambazo jeshi hilo linazieleza kuwa si za kweli, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwa kosa kisheria.
Madai ya faragha ya mawakili
Oktoba 24, 2026, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, alisema Lissu alikuwa anatarajia kuanza mgomo wa kula na kuacha kutumia dawa anazotumia kutokana na matatizo yake ya kiafya, akipinga kile chama hicho kilichodai kuwa ni ukiukaji wa amri ya Mahakama Kuu kuhusu haki yake ya kuzungumza na mawakili wake kwa faragha.
Dk Nshala alisema maofisa wa Magereza waliendelea kusimamia mazungumzo ya Lissu na mawakili wake licha ya hukumu iliyotolewa Oktoba 16, 2026, katika shauri namba 7300, ambayo amesema ilielekeza mazungumzo hayo yafanyike bila maofisa kuwasikiliza, ingawa wangeweza kuwaona kwa ajili ya usalama.
Alisema mawakili wa Lissu walimtembelea gerezani Oktoba 17 na 18, lakini hawakuruhusiwa kuzungumza naye kwa faragha, hali hiyo ilijirudia Oktoba 23 alipokwenda mwenyewe kumtembelea.
You may also like

CRDB yavuna faida ya Sh962 bilioni, Dk Nsekela atoa mwelekeo

Polisi Dodoma yawahakikishia usalama wanaofanya biashara usiku


Leave a Reply