

CRDB yavuna faida ya Sh962 bilioni, Dk Nsekela atoa mwelekeo
Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeongeza faida baada ya kodi kwa asilimia 29.1 hadi Sh672.07 bilioni katika kipindi cha miezi tisa kilichoishia Septemba 2026, ikichangiwa na ukuaji wa mikopo, amana za wateja na ufanisi wa uendeshaji.
Faida kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 28.9 hadi Sh962.24 bilioni, huku jumla ya mali za kundi ikikua kwa asilimia 34.2 hadi Sh27.45 trilioni.
Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa leo Jumanne, Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa mikopo halisi imeongezeka kwa asilimia 43.7 hadi Sh18.44 trilioni, huku amana za wateja zikikua kwa asilimia 26.5 hadi Sh17.79 trilioni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kundi la Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema matokeo hayo yanaonesha uimara wa mkakati wa muda mrefu wa benki hiyo na mchango wake katika maendeleo ya uchumi.
Amesema uwezo wa kifedha wa benki hiyo unaiwezesha kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia ufadhili wa sekta za uzalishaji na upanuzi wa huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela amesema matokeo hayo yametokana na utekelezaji wa mkakati wa benki, uwekezaji katika ubunifu na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kifedha.
Amesema ukuaji wa mikopo unaimarisha uwezo wa benki kufadhili biashara, minyororo ya thamani na uwekezaji, huku ikiendelea kupanua huduma za kidijitali na shughuli zake katika masoko ya kikanda.
Licha ya ukuaji huo, benki imeendelea kudumisha ubora wa mikopo, huku uwiano wa mikopo chechefu ukiwa asilimia 2.27 na gharama kwa mapato asilimia 41.42.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Kundi hilo, Fredrick Nshekanabo amesema benki imeendelea kusawazisha ukuaji, faida na nidhamu ya kifedha.
Katika kipindi hicho, benki ililipa kodi ya mapato ya Sh267.9 bilioni na gawio la Sh228.44 bilioni. Pia, ilitumia Sh360.39 bilioni kwa mishahara na mafao ya wafanyakazi 4,811.
Benki hiyo pia ilitunukiwa tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka 2026 na jarida la Global Finance.
You may also like

Chadema, Magereza zatofautiana kuhusu mgomo wa kula kwa Lissu

Polisi Dodoma yawahakikishia usalama wanaofanya biashara usiku


Leave a Reply