

…Kamati yatilia shaka baadhi ya maeneo, yashauri
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Bajeti imehoji wingi wa vipaumbele vilivyowekwa katika Mpango wa Taifa wa mwaka 2027, ikieleza kuwa kutokuwepo kwa msisitizo katika maeneo machache ya kimkakati kunaweza kudhoofisha utekelezaji na kuzuia kupatikana kwa matokeo yaliyokusudiwa.
Kamati hiyo pia imeibua wasiwasi kuhusu rasilimali fedha zilizotengwa, ikionya kuwa changamoto zilizojitokeza katika mpango wa mwaka 2024/25 zinaweza kujirudia.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki amesema utekelezaji wa vipaumbele vingi kwa wakati mmoja unaweza kuwa mgumu, hasa pale rasilimali fedha na uwezo wa taasisi zinazohusika vinapokuwa na mipaka.
Amesisitiza umuhimu wa kuweka msisitizo katika maeneo machache yenye uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo na kuleta matokeo yanayopimika.
Ndaki ameeleza kuwa mageuzi katika sekta za kimkakati hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa taasisi zote za umma. Hivyo, ni muhimu kuweka utaratibu madhubuti wa kuratibu utekelezaji na uwajibikaji.
Vilevile, kamati hiyo imetilia shaka namna sekta za msingi zitakavyopata msukumo unaostahili, ikitaja kilimo, miundombinu, ardhi, viwanda, pamoja na maliasili na utalii kuwa maeneo ambayo hayajapewa kipaumbele cha pekee.
“Bado kumekuwa na changamoto zinazotokana na matumizi ya kadi za simu, ikiwemo kitambulisho cha mtu mmoja kutumika kusajili laini zinazotumiwa na watu wengine. Hadi kufikia Juni 2026, watu 27,374,283 walikuwa wamesajiliwa na Nida. Hata hivyo, simu za kiganjani zilizosajiliwa katika kipindi hicho ni 106,823,601,” amesema Ndaki.
Mbunge huyo amesema takwimu hizo zinaonyesha kuwa kuna watu waliosajili laini kwa kutumia vitambulisho vya watu wengine. Ameeleza pia kuwepo kwa ongezeko la uhalifu wa kimtandao na kuchelewa kwa mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya namba zinazotumiwa na wahalifu wa kimtandao.
“Kamati ina ushauri kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kwa kushirikiana na makampuni ya simu, ifanye tena uhakiki wa wamiliki wa kadi za simu na majina yaliyosajiliwa, iweke sharti la kusajili kadi katika duka la mtandao husika na kuboresha mifumo ya utambuzi wa matumizi ya kadi yasiyo ya kawaida,” amesema Ndaki.
Kamati hiyo pia imeeleza kuwa ucheleweshaji wa malipo ya madeni ya wakandarasi unachelewesha ukamilishaji wa miradi kwa wakati. Imeeleza kuwa madeni hayo yamezidi Sh6 trilioni, jambo ambalo imesema ni vyema likatazamwa.
Mbunge wa Mbagala, Kakulu Burchard, amesema umefika wakati kwa Serikali kutoa msukumo wa vitendo kwa sekta binafsi, hasa katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara. Amesema Serikali imekuwa ikisuasua kwa miaka 65 bila kufikia malengo yanayotakiwa kutokana na kuwa na vipaumbele vingi.
Kakulu amesema si kwamba Serikali haifanyi kazi kubwa, bali kuna wakati inazidiwa. Hivyo, ili kurahisisha kazi na kuendana na hali inayotakiwa, sekta binafsi inapaswa kupewa msukumo zaidi, akielekeza mapendekezo yake katika ujenzi wa barabara.
You may also like

Sirro aagiza uchunguzi moto ulioteketeza vibanda 13 Kigoma

Wadau: Wazazi, walezi wawasikilize watoto badala ya kuwahukumu

Leave a Reply