

Maji ya shingo kwa Netanyahu akipambania uwaziri mkuu
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anakabiliwa na ushindani mkali wa kisiasa katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana, Oktoba 27, 2026, huku matokeo ya awali yakionyesha hakuna upande uliohakikisha kupata wingi wa viti unaohitajika kuunda serikali.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyoripotiwa hadi sasa na Times of Israel, chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kimepata viti 54, kikifuatiwa na chama Yashar cha mpinzani wake, Gadi Eisenkot, kilichopata viti 47.
Hata hivyo, wakati takribani nusu ya kura zikiwa zimehesabiwa, hakuna kundi la vyama lililoonekana kufikia viti 61 kati ya 120 vya Bunge la Israel, maarufu kama Knesset, vinavyohitajika kuunda Serikali yenye wingi wa wabunge. Matokeo hayo yanaweka mashaka kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Netanyahu, ambaye amekuwa kiongozi mwenye muda mrefu zaidi katika historia ya Israel, akiwa madarakani kwa vipindi tofauti tangu mwaka 1996.
Uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika nchini humo tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, yaliyoanzisha vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza, pamoja na mapigano yaliyofuata katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.
Masuala yaliyotawala kampeni ni pamoja na usalama wa taifa, namna serikali ilivyoshughulikia mashambulizi hayo, huduma ya lazima ya kijeshi kwa jamii ya Wayahudi wa Kiorthodoksi, mageuzi ya mahakama na athari za vita kwa uchumi na hadhi ya Israel kimataifa.
Netanyahu amesisitiza mafanikio ya kijeshi ya serikali yake na kuahidi kuendelea kukabiliana na Iran. Kwa upande wake, Eisenkot amejipambanua kama kiongozi anayeweza kuleta umoja wa kitaifa na mabadiliko ya kisiasa.
Pamoja na matokeo ya awali, bado kuna uwezekano wa mazungumzo ya kuunda muungano wa vyama kuchukua muda kabla ya serikali mpya kupatikana.
Akizungumza na Mwananchi Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Innocent Shoo amesema uchaguzi huo si mashindano ya kawaida ya vyama vya siasa. Ni kipimo cha imani ya wananchi kwa uongozi wao, tathmini ya namna serikali ilivyoshughulikia changamoto za kiusalama na uamuzi kuhusu mwelekeo wa taifa hilo katika Mashariki ya Kati.
“Katika mazingira hayo, ushindani kati ya Netanyahu na wapinzani wake, akiwamo Eisenkot, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), unaibua maswali muhimu kuhusu uwajibikaji, usalama na mustakabali wa amani ya kikanda,” amesema.
Iwapo Netanyahu atashindwa kufikia viti 61, njia yake kuu itakuwa kufanya mazungumzo na vyama vidogo, hasa vya mrengo wa kulia na vya kidini, ili kuunda serikali ya muungano.
Anaweza pia kujaribu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa kushirikiana na baadhi ya wapinzani wake. Hata hivyo, ikiwa mazungumzo yatakwama, uwezekano wa uchaguzi mwingine utaendelea kuwepo.
Kwa hiyo, hatima ya Netanyahu haitategemea idadi ya viti vya chama chake pekee, bali pia uwezo wake wa kupata washirika na kukubaliana nao kuhusu sera na mgawanyo wa madaraka.
Eisenkot na changamoto ya uongozi mpya
Katika ushindani huu, Eisenkot anawakilisha changamoto inayogusa eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa muhimu katika siasa za Israel: usalama wa taifa. Akiwa na uzoefu wa kuongoza IDF, ana nafasi ya kujadili kwa kina masuala ya kijeshi na namna nchi hiyo inavyopaswa kukabiliana na vitisho vya kikanda.
“Uzoefu huo unaweza kuvutia wananchi wanaotaka tathmini mpya ya matukio yaliyotangulia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, na namna serikali ilivyoshughulikia vita vilivyofuata Gaza.
“Hata hivyo, kuongoza jeshi na kuongoza serikali ni majukumu tofauti. Eisenkot atalazimika kuonyesha pia uwezo wa kuunganisha vyama vya upinzani, kusimamia uchumi na kuandaa sera zinazoweza kutekelezeka,” amesema Shoo.
Hivyo, changamoto yake si kumkosoa Netanyahu pekee, bali kuonyesha namna uongozi mbadala utakavyoweza kushughulikia matatizo yale yale ambayo yamegawa jamii ya Israel.
Je, Netanyahu anapoteza nguvu ya kisiasa?
Shoo anasema kushindwa kupata wingi wa viti kunaweza kuonyesha kupungua kwa uwezo wa Netanyahu kuunda serikali, lakini si lazima kumaanishe amepoteza kabisa uungwaji mkono wa wananchi. Bado ana wafuasi wanaothamini uzoefu wake wa kisiasa na msimamo wake kuhusu usalama wa Israel.
Hata hivyo, uchaguzi unaweka wazi tofauti kati ya kuwa na wafuasi wengi na kuwa na uwezo wa kuendesha serikali. Katika mfumo wa bunge, kiongozi anaweza kuwa na ushawishi mkubwa lakini akashindwa kupata washirika wa kutosha kuunda serikali.
Kwa hiyo, tathmini ya nguvu ya Netanyahu inahitaji kuangalia si matokeo ya chama chake pekee, bali pia ukubwa wa kambi yake, uwezo wa wapinzani kuungana na matokeo ya mazungumzo ya kuunda serikali.
Gaza na Oktoba 7: mtihani wa uwajibikaji
Shoo anasema hakuna mjadala wa uchaguzi wa Israel unaoweza kukamilika bila kuzingatia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, na vita vilivyofuata Gaza. Mashambulizi hayo yaliibua maswali mazito kuhusu uwezo wa mifumo ya ujasusi na usalama ya Israel kuzuia tishio, pamoja na uwajibikaji wa viongozi wa kisiasa.
Kwa Netanyahu, vita vimekuwa mtihani wa uongozi. Wakosoaji wake wanahoji kuhusu kushindwa kuzuia mashambulizi na gharama za vita, huku wafuasi wake wakisisitiza umuhimu wa kuilinda Israel dhidi ya Hamas na vitisho vingine vya kikanda.
Masuala haya yanaweza kuathiri uamuzi wa wapigakura kwa namna tofauti. Familia za mateka, wananchi walioathiriwa na mashambulizi na wakazi waliolazimika kuhama makazi yao wanaweza kutathmini uongozi kwa kuzingatia usalama na uwajibikaji. Wengine wanaweza kuweka mkazo katika operesheni za kijeshi na uwezo wa serikali kuzuia mashambulizi mengine.
Athari kwa Mashariki ya Kati
Akiendelea kufafanua Shoo anasema matokeo ya uchaguzi yatakuwa na umuhimu zaidi ya mipaka ya Israel. Serikali itakayoundwa italazimika kufanya uamuzi kuhusu Gaza, Iran, hali ya usalama katika mpaka wa Lebanon na mahusiano na mataifa ya Kiarabu.
Kuendelea kwa Netanyahu au kuingia kwa uongozi mpya kunaweza kuathiri namna masuala hayo yanavyoshughulikiwa. Hata hivyo, mabadiliko ya waziri mkuu pekee hayahakikishi mabadiliko ya sera, kwa kuwa uamuzi wa Israel pia huathiriwa na muundo wa muungano wa serikali, masuala ya usalama na misimamo ya vyama vinavyoshiriki madarakani.
Kwa ujumla, uchaguzi wa Israel ni kipimo cha uhusiano kati ya uongozi, usalama na uwajibikaji wa kisiasa. Netanyahu anaweza kuendelea kuwa na ushawishi, lakini uwezo wake wa kubaki madarakani utategemea kupata wingi wa kura unaohitajika bungeni.
Kwa upande mwingine, Eisenkot na wapinzani wake wanakabiliwa na jukumu la kuonyesha kwamba wanaweza kuunda serikali imara na kutoa majibu yanayoeleweka kwa changamoto za taifa.
Historia ya uchaguzi Israel
Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka huu unaongeza sura nyingine katika historia ya misukosuko nchini Israel, ambayo kati ya mwaka 2019 na 2022 ilifanya chaguzi tano za bunge kutokana na kushindwa kwa vyama kupata makubaliano ya kuunda serikali yenye uthabiti.
Katika uchaguzi wa Aprili 2019, chama cha Likud cha Netanyahu na chama cha Blue and White cha Benny Gantz vilipata viti 35 kila kimoja. Hata hivyo, Netanyahu alishindwa kuunda serikali, hali iliyosababisha bunge kuvunjwa na uchaguzi mwingine kuitishwa Septemba mwaka huohuo.
Katika uchaguzi wa Septemba 2019, Blue and White kilipata viti 33, huku Likud ikipata 32. Matokeo hayo nayo hayakuwezesha upande wowote kupata muungano wenye uwezo wa kuunda serikali imara.
Uchaguzi mwingine ulifanyika Machi 2020, ambapo Likud ilipata viti 36 dhidi ya 33 vya Blue and White. Baadaye, Netanyahu na Gantz walikubaliana kuunda serikali ya umoja, lakini serikali hiyo ilisambaratika ndani ya mwaka mmoja.
Machi 2021, Israel ilifanya uchaguzi mwingine, ambapo Likud ilipata viti 30 na chama cha Yesh Atid cha Yair Lapid kikapata 17.
Matokeo hayo yaliwezesha vyama vinane vyenye mitazamo tofauti kuunda muungano ulioongozwa na Naftali Bennett, ambaye alishika nafasi ya waziri mkuu kabla ya Lapid kuchukua uongozi wa serikali ya mpito. Muungano huo ulimaliza miaka 12 mfululizo ya Netanyahu akiwa waziri mkuu, lakini nao ulidumu kwa takribani mwaka mmoja.
Netanyahu arejea madarakani
Novemba 1, 2022, Israel ilifanya uchaguzi wa tano ndani ya takribani miaka mitatu na nusu. Katika uchaguzi huo, Likud ilipata viti 32, huku Yesh Atid ikipata 24.
Likud na washirika wake wa vyama vya mrengo wa kulia na vya kidini walipata jumla ya viti 64, na hivyo kumpa Netanyahu nafasi ya kurejea madarakani kwa kuunda serikali yenye msimamo mkali zaidi wa mrengo wa kulia katika historia ya nchi hiyo.
You may also like

Sirro aagiza uchunguzi moto ulioteketeza vibanda 13 Kigoma

Wadau: Wazazi, walezi wawasikilize watoto badala ya kuwahukumu


Leave a Reply