

Aliyehukumiwa kwa kujaribu kumuua mke mwenza aachiwa
Arusha. Mahakama ya Rufani imemwachia huru Khadija Shaaban Ali, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kujaribu kumuua mke mwenza, Maimuna Said Suleiman, kwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia kisu.
Khadija alitiwa hatiani na Mahakama Kuu Zanzibar, baada ya kukutwa na hatia ya kujaribu kusababisha kifo cha Maimuna, tukio lililodaiwa kutokea Februari 9, 2025, Chukwani, Zanzibar, alipodaiwa kumshambulia maeneo mbalimbali kwa kisu, ikiwemo uso, shingo na mikono.
Hukumu iliyobatilisha uamuzi huo wa Mahakama Kuu ilitolewa Oktoba 21, 2026 na majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Rehema Kerefu, Benhajj Shaaban Masoud na Cyprian Mkeha.
Majaji hao walikuwa wakisikiliza rufaa hiyo namba 2/2026 iliyokatwa na Khadija, aliyekuwa akipinga hukumu ya Januari 30, 2026 iliyotolewa na Mahakama Kuu Zanzibar.
Jaji Masoud amesema baada ya kupitia mwenendo na rufaa, wamebaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha bila kuacha shaka kuwa Khadija alikuwa na nia ya kumuua Maimuna.
Amesema nia ya kumuua mtu ni kiungo muhimu katika kosa la kujaribu kuua na iwapo hakijathibitishwa, viungo vingine vya kosa hilo haviwezi kuthibitisha shtaka.
Amesema Mahakama, baada ya kupitia upya ushahidi, ilibaini tukio hilo lilihusisha mapambano kati ya Khadija na Maimuna, ambao wote walipata majeraha, huku kukiwa hakuna ushahidi thabiti wa shahidi aliyeona namna kisu kilivyotumika kumjeruhi Maimuna.
“Nia ya kumuua mtu ndiyo kiungo muhimu zaidi katika kosa la kujaribu kuua na ikiwa nia hiyo haijathibitishwa, Mahakama haiwezi kuendelea kuchunguza viungo vingine,” ameeleza.
Jaji huyo amesema Mahakama hiyo pia iliondoa kisu ambacho kilikuwa kielelezo cha tatu katika kesi hiyo baada ya kubaini mapungufu katika mnyororo wa utunzaji wake.
Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukutimiza wajibu wake wa kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka na kukubali rufaa hiyo, hivyo kuamuru Khadija achiliwe mara moja kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, ilidaiwa mrufani na Maimuna ni wake wenza wa Suleiman Shaaban Chasama, ambao walikuwa wakisafiri kwa gari kutoka Mbweni kuelekea Chukwani.
Maimuna, aliyekuwa akiendesha gari hilo, alidai Khadija na Suleiman walikuwa wamekaa siti za nyuma za gari na kuwa walipofika nyumbani kwa Khadija, alikataa kushuka na kutaka kwenda nyumbani kwa Maimuna.
Alidai walipofika nyumbani kwake, Khadija aliendelea kukataa kushuka kwenye gari, ambapo Suleiman alipoingia ndani kujisaidia, Maimuna alijaribu kumshawishi Khadija ashuke lakini hakufanikiwa na kuwa ghafla alianza kumshambulia kwa kisu, hali iliyosababisha ugomvi kati yao.
Mashahidi wa pili na nane, walioshuhudia tukio hilo, walidai kuwaona wakiwa chini wakipambana huku Khadija akiwa na kisu na mwenzake akiwa na majeraha sehemu mbalimbali.
Walidai walijaribu kuingilia ugomvi huo na Khadija aliachia kisu hicho baada ya kuombwa na shahidi wa tatu, ambapo Maimuna alipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Katika utetezi wake, Khadija alikana kutenda kosa hilo na kudai ugomvi baina yao ulisababishwa na Maimuna baada ya kukataa kushuka kwenye gari.
Alidai baada ya mume wao kushuka kwenye gari, Maimuna alifungua mlango wa nyuma wa gari alipokuwa amekaa na kumtaka ashuke, lakini alipokataa, Maimuna alianza kumpiga na kumng’ata na kudai Maimuna ndiye aliyekuwa na kisu.
Aliiambia Mahakama kuwa ugomvi wao ulisitishwa baada ya mafundi waliokuwa wakifanya kazi eneo la karibu kuwaamua na kuwa alichokifanya ilikuwa ni kujilinda, si kumuua Maimuna.
Shahidi wa pili wa utetezi alimwambia Mahakama kuwa Khadija, ambaye alipatiwa matibabu, alikuwa na alama za kung’atwa mgongoni, mkononi, mbavuni na begani, ushahidi uliotumika kuunga mkono utetezi wa Khadija.
You may also like

Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha

Waziri Ulega awataka watendaji kutumia madaraka kwa uadilifu


Leave a Reply