

Baba, mpwa wake waagwa kwa utaratibu wa kipekee
Dar es Salaam. Miili ya Humphrey Msoka (66) na mpwa wake, Dickson Msoka (24), imewasili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kibwegere Adonai, kwa ajili ya ibada ya kuwaaga kabla ya kuzikwa katika Makaburi ya Kibwegere, Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo inayofanyika leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, waombolezaji wametumia utaratibu tofauti na ule wa kawaida wa kupita karibu na majeneza ili kuuaga mwili wa marehemu, badala yake wamekuwa wakitazama picha za marehemu zilizowekwa juu ya majeneza yao.
Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kanisani hapo kuwaaga wapendwa wao, huku wengi wakiwa na nyuso za huzuni na kuvaa mavazi meupe na meusi.
Majeneza yenye miili ya Hunfrey Msoka (kushoto) aliyedaiwa kuuawa kwa kupigwa mapanga na mtoto wa ndugu yake aitwaye Dickson Msoka ambaye nae aliuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira (jeneza la kulia), yakiwa yamewasili kwenye Kanisa la KKKT Dayosis ya Mashariki na Pwani Jimbo la Magharibi Mtaa wa Kibwegere eneo la Kibamba Shule Dar es Salaam. Picha na Said Powa
Hadi saa 7 mchana, waombolezaji walikuwa wakiendelea kuimba nyimbo za maombolezo, baada ya miili hiyo kuingizwa kanisani saa 6:30 mchana.
Humphrey alifariki baada ya kushambuliwa kwa panga na Dickson, ambaye alikuwa mpwa wake. Dickson naye alifariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi waliokasirishwa na tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi Oktoba 19, 2026, Herman Msoka, mtoto wa pili wa Humphrey, alisema tukio la kuuawa kwa baba yake lilitokea Oktoba 18, 2026, majira ya saa mbili usiku.
Kwa mujibu wa Herman, kabla ya tukio hilo, baba yake alimkumbusha Dickson umuhimu wa kunywa maji mengi kutokana na tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo (UTI) alilokuwa nalo.
Waombolezaji waliojitokeza kuaga miili ya Hunfrey Msoka (kushoto) aliyedaiwa kuuawa kwa kupigwa mapanga na mtoto wa ndugu yake aitwaye Dickson Msoka ambaye nae aliuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira (jeneza la kulia),
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Dickson alimwita baba yake mkubwa ndani ya nyumba, kisha akamshambulia kwa panga kichwani na mkononi.
Herman alieleza kuwa muda mfupi kabla ya tukio hilo, Dickson alikuwa akizungumza na Humphrey na kumwomba amsaidie kutupa simu yake chooni, kisha amchome kisu ili aende Kituo cha Polisi Segerea.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, aliyesema uchunguzi kuhusu chanzo cha tukio hilo unaendelea.
Kwa mujibu wa Muliro, Dickson alikuwa akiishi na baba yake mkubwa, Humphrey, ambaye alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa.
Dickson naye alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini kwa matibabu, baada ya kushambuliwa na wananchi waliokasirishwa na tukio hilo.
Miili ya wawili hao inatarajiwa kuzikwa katika Makaburi ya Kibwegere jijini Dar es Salaam.
Endelea kufuatilia Mwananchi
You may also like

Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade

Samia to inaugurate Sh700bn Government City on October 30


Leave a Reply