

CCM Tanga kugawa matrekta 40 kusaidia wakulima
Tanga. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kinatarajia kugawa matrekta 40 katika wilaya mbalimbali za mkoa huo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kulima mashamba yao kwa gharama nafuu. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, amesema matrekta hayo yatatoa huduma ya kulimia wakulima watakaohitaji, ambao watachangia gharama za mafuta yatakayotumika katika shughuli hiyo.
Amesema mpango huo unalenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wakulima wengi kupata huduma ya matrekta katika maandalizi ya mashamba yao.
Rajabu alizungumza hayo jana Jumapili, Novemba 1, 2026, wakati wa hafla ya kujitambulisha kwa mlezi mpya wa CCM Mkoa wa Tanga, Rabia Abdallah.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, akihutubia wanachama wa chama hicho wakati wa hafla ya kumtambulisha mlezi mpya wa CCM Mkoa wa Tanga, iliyofanyika Novemba 1, 2026. Picha na Mbonea Herman
Kwa upande wake, Rabia alisema baadhi ya nchi na jumuiya za kimataifa zilizokuwa zikitishia kuiwekea Tanzania vikwazo na kuitenga zimeanza kubadili msimamo na kuiondoa katika tahadhari za usalama kwa raia wao wanaotaka kuitembelea.
Rabia, ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Idara ya Siasa na Mambo ya Nje (SUKI), alisema awali baadhi ya mataifa yalikuwa yakitoa tahadhari kwa wananchi wao dhidi ya kusafiri kwenda Tanzania, lakini sasa yameanza kuondoa tahadhari hizo na kuonesha imani kuhusu hali ya usalama nchini.
Mlezi mpya wa CCM Mkoa wa Tanga, Rabia Abdallah, akizungumza na wanachama wa chama hicho wakati wa hafla ya kujitambulisha rasmi mkoani Tanga. Picha na Mbonea Herman
“Zile nchi ambazo zilitishia kutuwekea vikwazo na kutususa zimeondoa. Kuna nchi za Umoja wa Ulaya zilizokuwa zimeweka tahadhari dhidi ya Tanzania, lakini zimeondoa na kusema Tanzania ni salama na kuna amani ya kutembelea,” alisema Rabia.
Aliongeza mabadiliko hayo yanaonesha kurejea kwa imani ya kimataifa kuhusu Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mahusiano na mataifa mengine.
Naye mwanachama wa CCM, Salma Abdallah, alisema mpango wa kugawa matrekta hayo ni hatua itakayowasaidia wakulima kupata huduma ya kulimiwa mashamba kwa kuchangia gharama za mafuta badala ya kutumia fedha nyingi katika maandalizi ya mashamba.
You may also like

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund

Mianya ya usajili inavyowalinda matapeli


Leave a Reply